MGODI WA BUZWAGI KUFUNGWA NDANI YA MIAKA MIWILI IJAYO



Mgodi wa dhahabu wa Buzwagi uliopo Kahama mkoani Shinyanga, huenda ukafungwa ndani ya miaka miwili ijayo ili kuiepushia hasara kampuni inayochimba dhababu katika eneo hilo, African Barrick Gold.
Meneja mgodi huo, Muganda Mutereko alisema hali hiyo itatokea endapo bei ya dhahabu itaendelea kushuka zaidi ya ilivyo sasa.
 “Lakini kwa sababu bei inashuka kila mara, ni lazima tukae na kuangalia mwenendo wake ili kuamua kama tuendelee au tusiendelee na uchimbaji. Ikiwa ndani ya miaka miwili hali itakuwa hivi katika bei, tutalazimika kuufunga mgodi ndani ya miaka miwili kuanzia sasa,”Mutereko alisema.
Alifafanua kuwa fedha wanazozitumia kuchimba madini ni nyingi hivyo ni afadhali wakafunga maeneo mengine kuruhusu yaendelee yenye faida na mafanikio makubwa.
“Dhahabu inayotoka katika mgodi huu huwezi kuilinganisha na ya North Mara, ile ni nyingi na ni bora zaidi, hivyo bei zinapozidi kuporomoka ni afadhali unaendelezwa zaidi ule wenye faida kubwa na kufunga mingine. Hilo tutalijua baadaye, ngoja tutazame mabadiliko ya bei sokoni,” alisema.

No comments: