MAWAKILI WAOMBA FUIME KUFUTIWA KESI YA MAUAJI



Mawakili wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Gabriel Fuime (61), wameiomba  Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kufuta kesi ya mauaji ya watu 27  inayomkabili Fuime na wenzake 11.
Wakiwasilisha hoja hiyo  jana mbele ya Hakimu Mkazi Devotha Kisoka, Wakili John Mhozya na Ndurumah Majembe waliiomba Mahakama kuangalia kwa makini hati ya mashitaka  kwa kuwa madai yaliyomo ni batili, hayakidhi matakwa ya sheria.
Wakili Mhozya alidai kuwa, sheria inataka hati ya mashitaka  iwe na viashiria vya kosa  ambalo mshitakiwa anashitakiwa nalo, aliongeza kuwa Fuime ameshitakiwa  kwa mauaji lakini hati iliyopo mahakamani haina viashiria vinavyoonesha  kosa hilo.
Awali alipoanza kuwasilisha hoja, Hakimu Kisoka alisema jalada la kesi hiyo lipo Mahakama  Kuu, hata hivyo Mhozya aliomba kuendelea kuwasilisha hoja hiyo kwa kuwa jambo lililosababisha lipelekwe huko halimhusu Fuime.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Benard Kongola  alipinga  kwa madai kuwa  Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza wala kusuluhisha chochote kwa sababu kesi imefunguliwa hapo kwa taratibu za awali tu.
Hata baada ya Mhozya kupewa nafasi ya kusikilizwa, Wakili Kongola alizidi kupinga na kudai kuwa hata jibu chochote na anaweza kutoka nje ya Mahakama wakati kesi hiyo ikiendelea. 
Wakili Majembe aliiomba Mahakama kuzuia uvunjifu wa sheria na kudai katika kusoma kwake  na uzoefu aliokuwa nao hajawahi kuona kitu kinachodaiwa na upande wa mashitaka.
Aliongeza kuwa Mahakama ina uwezo wa kuangalia kwa makini kosa ili kujiridhisha kwa kuwa uhuru wa mtu ni muhimu na jela ni mbaya; “leo Fuime ameshitakiwa kwa kosa la mauaji kesho anaweza kubadilishiwa likawa la kutakatisha fedha na baadaye hata kubaka."
 Hakimu  Kisoka  aliahirisha kesi hiyo hadi  Mei 19, mwaka huu Mahakama hiyo itatoa uamuzi kama inauwezo wa kufanya hivyo.
Mbali na Fume washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni mfanyabiashara Laza Radha, Diwani katika Manispaa ya Kinondoni, Ibrahim Mohamed (59), vigogo wa Manispaa ya Ilala ambao ni Mhandisi Mkuu, Charles Ogare (48), Mhandisi wa Majengo Godluck Sylivester (35) na Mkurugenzi Mkuu wa Mkaguzi wa Majengo, Willibrod Mugyabuso (42).
Wengine ni Mhandisi Mohamed Abdurkarim (61), Mhandisi Mshauri, Zonazea Oushoshaodaga Hema (59), Msajili Msaidizi AQRB, Albert Mnuo na Ofisa Mkuu Mtekelezaji OQRB, Joseph Ringo (60), Mkadiriaji Ujenzi, Vedasto Ruhale (59), Msanifu Majengo, Michael.
 Inadaiwa kuwa Machi 29 mwaka jana, katika mtaa wa India Gandhi Ilala, Dar es salaam kwa makusudi washitakiwa waliwaua watu 27 kutokana na kuporomoka kwa jengo la ghorofa 16.

No comments: