MAMENEJA BARCLAYS KORTINI KWA TUHUMA ZA WIZI WA MILIONI 479/-

Watu saba wakiwemo mameneja wawili wa Benki ya Barclays, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashitaka ya wizi wa zaidi ya Sh milioni 479 katika benki hiyo.
Washitakiwa hao, walifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka mawili na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Tumaini Kweka akisaidiwa na Wakili Mwanaamina Kombakono mbele ya Hakimu Mkazi, Nyigulila Mwaseba.
Washitakiwa hao ni Meneja wa benki hiyo Tawi la Kinondoni, Alune Kasililika (28) na Meneja Neema Batchu. Wengine ambao ni wafanyabiashara ni Kakamie Julius (32), Iddy Khamis (32), Sezary Massawe (31), Boniphace Muumba (29) na Ruth Macha (30).
Wakili Kweka alidai kuwa muda na siku isiyofahamika, jijini Dar es Salaam, washitakiwa hao walipanga njama za kutenda kosa.
Alidai kuwa Aprili 15 mwaka huu katika Benki ya Barclays tawi la Kinondoni, washitakiwa hao waliiba Sh 390,220,000, dola 55,000 za Marekani na Euro 2,150 za Ulaya, mali ya benki hiyo.
Wakili Kweka alidai kuwa kabla na baada ya wizi huo, washitakiwa walitumia silaha kuwatishia wafanyakazi wa benki hiyo, Anifa Ahmad na Anna Tegete ili wachukue fedha hizo bila pingamizi.
Washitakiwa walikana mashitaka. Upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo, haujakamilika na uliomba tarehe ya kutajwa.
Hakimu Mwaseba alisema mashitaka yanayowakabili watuhumiwa hao, hayana dhamana, hivyo watakuwa chini ya ulinzi hadi Mei 15 mwaka huu, kesi hiyo itakapotajwa tena.

No comments: