KINANA AKEMEA WANAOPOTOSHA KATIBA MPYA

Siku moja baada ya viongozi wa kile kinachoitwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kuondoka Pemba, wakidai kuelezea sababu za wao kususa Bunge Maalumu la Katiba, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimewataka Watanzania kutoamini hadaa za watu wasioitakia mema Tanzania.
Chama hicho kimesema watu hao watengeneza chokochoko kupitia kigezo cha mchakato wa uandikaji wa Katiba mpya, na kusema Katiba hiyo si mwarobaini wa matatizo yaliyopo sasa hapa nchini.
Katibu Mkuu CCM, Abdulrahman Kinana, aliyasema hayo jana alipokuwa akihutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Gombani ya Kale visiwani hapa jana, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku 2 katika visiwa vya Unguja na Pemba kukagua utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM mwaka 2010/2015 na kuhamasisha shughuli za maendeleo kwa wananchi.
Katika mkutano huo alizungumzia matukio yanayoendelea kutokea nchini, hasa upotoshaji unaoendelea hivi sasa, ambapo aliwatoa hofu watanzania kuwa, hayazuii kupatikana kwa Katiba hiyo.
Alisisitiza kuwa Katiba inayopigiwa kelele na kila makundi haisaidii kumfanya mtu ambaye hana uhakika wa fedha mfukoni apate ghafla, wala haimfanyi mtu anayeishi kwenye nyumba ya kupanga kuamka na kumiliki nyumba bali katiba ni sheria mama ambayo inaandikwa na inapokamilika huwekwa kabatini na maisha kuendelea.
“Katiba si miujiza, itapatikana na kuzinduliwa kwa shangwe, lakini naomba niwatahadharishe kuwa kupatikana kwa Katiba hii haimaanishi kuwa matatizo yetu yataisha hapo hapo, kila kitu kinakwenda kwa utaratibu wake, haina haja ya kuvutana kama tunataka kitu kizuri,” alisisitiza.
Alifafanua kuwa kuna baadhi ya nchi duniani ambazo zina Katiba bora sana kama vile Afrika Kusini na Namibia lakini katiba hizo hazijasaidia kuboresha maisha ya wananchi wake, kwa kuwa utekelezaji wa kuboresha maisha ya wananchi unakwenda hatua kwa hatua.
Alisema kinachoendelea kwa sasa bungeni ni wazi kuwa baadhi ya watu kutoka vyama vya upinzani akili zao zimejikita katika uroho wa madaraka na ndio maana wanang’ang’ania mfumo wa Serikali tatu wakiwa na imani kuwa huenda zikipatikana wataongeza nafasi ya kupata madaraka.
Naye Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema Ukawa ni kikundi cha wachumia tumbo ambacho kinategemea fedha za wasioitakia mema Tanzania kuvuruga amani iliyopo.
Alisema Ukawa ni genge la wataka madaraka na kwamba hiyo ni janja ya baadhi ya wanakikundi hicho ambao ni Chadema ambao wanawaburuza wanasiasa uchwara wasiojitambua.
Alifafanua kuwa wapinzani nchini walizoea vya kunyonga na baada ya kukosa agenda za msingi sasa wamebakia kuwahadaa wananchi kwa hoja zisizo na msingi.
Nape alisisitiza kuwa huu si wakati wa kupigizana kelele na watu wanaoungana bila kuwa na malengo mahususi, badala yake aliwaambia wananchi kuwakataa kwani hawana nia ya kuungana kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi, badala yake ni kwa malengo ya kuboresha maisha yao wenyewe na watoto wao.
Aliwataka Chadema akiwemo Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe kujibu kwanini hakuwaingiza wapinzani wenzake katika Baraza Kivuli la Mawaziri? Kama sio ujanja wa kuwahadaa wenzake baada ya kugundua kuwa wanapenda vyeo vya dezo.
Chadema, baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 iliingia bungeni na kuunda Kambi ya Upinzani bila kushirikisha vyama vingine kikiwemo CUF chenye wabunge wengi. NCCR –Mageuzi, TLP vyenye wabunge, navyo viliwekwa kando.
Lakini katika Bunge Maalumu la Katiba, vyama vingine viliingiwa katika `uswahiba’ na Chadema na kuunda Ukawa kwa lengo la kuongeza nguvu ya ushawishi dhidi ya CCM chenye wabunge wengi, ikiaminika kuwa kwa wingi wao wangewaburuza wengine katika maamuzi.
Na hata baada ya wote kususa bunge hilo katika siku za mwisho za kikao chake kilichoketi kwa siku 70 hadi Aprili 25, mwaka huu, lakini kikaahirishwa hadi Agosti 5, mwaka huu kwa lengo la kupitisha Bunge la Bajeti linaloanza vikao vyake keshokutwa.
Katikati ya wiki, viongozi wa Ukawa wakiwa katika mkutano wa hadharani mjini Pemba, Mbowe alikaririwa akisema anakusudia kuvunja baraza la mawaziri kivuli ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili aingize wa vyama vingine, ikiwa ni ishara ya kuendeleza mshikamano baina ya vyama vya upinzani katika bunge hilo.

No comments: