KAMPUNI YA KICHINA YAPANIA KUKUZA AJIRA NCHINIKampuni ya Kichina ya kuhuisha plastiki,  inayofanya shughuli zake jijini Dar es Salaam ya Fusun Investment United Limited  ina mpango wa kutanua shughuli zake kwa kuwekeza zaidi nchini na kuongeza ajira zaidi kwa Watanzania.
Ilisema hayo jana wakati wa ziara ya waandishi wa habari katika kiwanda cha kampuni hiyo kilichopo Kurasini,  ambacho tayari kimetoa ajira zaidi ya 300 hadi sasa.
"Wakati biashara yetu ikiendelea kutanuka, kuna uwezekano mkubwa wa sisi kuweza kuajiri watu wengi zaidi," alisema Mkurugenzi wa kampuni hiyo,  Jiang Jiaxing.
Alisema kuwa kampuni hiyo, iliyoanzishwa tangu Desemba mwaka 2010 inakusanya tani 700 za chupa za plastiki kutoka mtaani kwa wananchi kila mwezi na kuzisaga kuwa chakavu na kuzisafirisha  kwenda China, kutengeneza vifaa vya plastiki vipya.
Pia, alisema kampuni yake imefungua viwanda viwili katika maeneo ya Mabibo na Mikocheni jijini Dar es Salaam na mipango inafanyika ya kupanua shughuli zake katika mikoa mingine vijijini.
"Tumechangia katika uchumi wa Tanzania kwa njia nyingi, kama vile kuingizia nchini fedha za kigeni, mapato kwa njia ya malipo ya kodi na ushuru na kuunga mkono jitihada za serikali za utunzaji wa mazingira kwa kukusanya plastiki zinazozagaa ovyo kisha kuhuisha," alisema na kuongeza: "Hebu tafakari, nini kingeweza kutokea endapo tani 700 za chupa chakavu za plastiki, zingeachwa zikizagaa mitaani? Ingelikuwa ni tatizo kubwa".

No comments: