KAGERA WASHAURIWA KULIMA VIAZI VITAMU KIBIASHARA


Wananchi wa mkoa wa Kagera wameshauriwa kuingia katika kilimo cha biashara kwa kulima zao mbadala la viazi vitamu ili kuongeza kipato na chakula kutokana na zao kuu la biashara na chakula la mkoa huo ambalo ni ndizi kukumbwa na ugonjwa wa unyanjano. 
Ushauri huo ilitolewa jana na Germinus Nyeho kutoka kituo cha utafiti wa kilimo Maruku wakati wa mafunzo kwa wakulima na maofisa ugani 60  kutoka Wilaya za Bukoba na Missenyi waliyoyapata juu ya uzalishaji wa mbegu bora za viazi. 
Nyeho alisema wananchi wa mkoa wa Kagera wamekuwa na dhana kuwa zao la ndizi ndio zao pekee linaloweza kuliwa na kuwaongezea kipato, jambo ambalo amesema ni vyema wakatambua kuwa zao hilo kwa sasa limekumbwa na ugonjwa wa unyanjano na kufanya upatikanaji wake kuwa mgumu. 
Aliongeza kuwa kama kituo chao cha utafiti waliamua kulichagua zao hilo na kuwashauri wananchi kulifanya zao mbadala pia lina virutubisho vingi ikiwemo kuongeza vitamin A, protini ambapo itasaidia kupunguza utapiamlo kwa watoto wadogo. 
Dorothy Lusheshanija ambaye alikuwa mwezeshaji katika semina hiyo kutoka jijini Mwanza katika ofisi ya Afya ya mimea na kituo cha kimataifa cha viazi, alisema kwa sasa wakulima wanashauriwa kupanda mbegu bora za malando zinazotoa mazao mengi na kustahimili magonjwa  kwa kufuata ushauri wa kitaalamu.

No comments: