HOMA YA DENGUE YAZIDI KUTIKISA DAR

Hospitali za jiji la Dar es Salaam zimeendelea kupokea wagonjwa wa homa ya dengue na jana wamepokewa wagonjwa wapya 36 katika hospitali za Temeke, Kinondoni na Ilala.
Ofisa Ufuatiliaji wa Magonjwa wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alex Mkamba aliliambia gazeti hili jana, baadhi walitibiwa na kuruhusiwa na wengine kutokana na hali zao kutoridhisha, walilazwa.
Alisema, Hospitali ya Temeke walipokea wagonjwa wanane,  Ilala wagonjwa 11, Kinondoni wagonjwa 17, Sinza mgonjwa mmoja na Kinondoni kwa Dk Mvungi mgonjwa mmoja.
"Mgonjwa baada ya kufika hospitali na kufanyiwa vipimo, daktari ndiye anayeona kama mgonjwa ana hali nzuri anaruhusiwa kurudi nyumbani lakini kama hali hairidhishi basi analazwa, lakini hata hivyo anapoendelea vizuri huruhusiwa pia," alisema Mkamba.
Aidha alisema juzi  walipokea wagonjwa  27 ambao  11 ni kutoka Kinondoni, wanane wa Ilala na weliobaki ni wa Temeke.
Alisema tayari vifaa vya kupima ugonjwa huo, vimesambazwa katika hospitali zote za jiji la Dar es Salaam. Pia wameanza operesheni ya kupuliza dawa  katika maeneo mbalimbali kuua mazalia ya mbu.
“Tunapuliza dawa katika mazalia  ya mbu ambapo mpaka sasa katika kata 78 tumeshapuliza katika mabonde na mifereji, pia tumepuliza katika shule, taasisi mbalimbali na nyumba za kulala wageni," alisema Mkamba.
Mkamba alisema uhamasishaji unaendelea kufanyika kupitia kamati za kudumu za afya za kata kukabili ugonjwa huo kwa kuwajengea uelewa na namna ya kujilinda.
Ugonjwa huo uliolipuka hivi karibuni jijini Dar es Salaam, hauna tiba maalumu wala chanjo na njia pekee ya kuukabili, ni kutambua dalili zake kama vile homa, kupungukiwa maji au damu, kuumwa kichwa, maumivu ya viungo na uchovu. Mgonjwa anaweza kupoteza maisha endapo atachelewa kupatiwa matibabu.
Wananchi wameaswa kuchukua hadhari juu ya ugonjwa wa dengue ambao dalili zake ziko sawa na  za malaria. Kwa mujibu wa Mkamba, takwimu zinaonesha hadi jana, watu 905 wameugua ugonjwa huo tangu ulipoanza mwanzoni mwa mwaka huu.
Hivi karibuni, Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Afya na Dharura, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Elias Kessy alisema ugonjwa huo, umeanza kusambaa kwa kasi mikoani.
Kwa sasa wagonjwa wapya 50, wamegundulika huku ikielezwa wengi ni waliotoka nao mkoani Dar es Salaam. Wengi wa wagonjwa hao, walikuwa wamesafiri kutoka Dar es Salaam kwenda mikoa husika.

No comments: