BUNGE LASISITIZA JENGO LA GHOROFA 16 DAR LIVUNJWE

Bunge limesisitiza kuwa jengo la ghorofa 16 lililoko katika Mtaa wa Indira Gandhi, Dar es Salaam ambalo liliagiza mwaka jana livunjwe, agizo hilo litekelezwe.
Aidha, imeishauri Serikali kutaifisha maeneo yote makubwa yasiyoendelezwa na kuyagawa kwa wananchi kwa matumizi mengine.
Hayo yamo katika taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira kuhusu bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya (CCM) akisoma taarifa hiyo bungeni jana, alisema, “suala hili tuliliagiza katika bajeti iliyopita na tunazidi kusisitiza utekelezaji huu ufanyike mara moja.”
“Kamati inasikitikishwa kwamba agizo hili halijatekelezwa. Kamati inaiagiza Serikali kulifikisha suala hili kwa Rais haraka ili lipatiwe ufumbuzi kabla ya madhara kutokea,” alisema Bulaya.
Kuhusu ardhi, ilishauri Serikali kuondoa mianya inayotoa fursa na ushawishi mbovu kwa viongozi na watu wachache wasio na nia njema kwa maslahi ya Taifa, bali kujilimbikizia mali kwa maana ya Taifa kwa kutumia mgongo wa Serikali.
“Aidha, Kamati inaishauri Serikali kutaifisha maeneo yote makubwa yasiyoendelezwa na kuyagawa kwa wananchi kwa matumizi mengine,” alisema Bulaya.
Kuhusu Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Kamati iliishauri Serikali kupitia Wizara ya Fedha ione umuhimu wa kuondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa nyumba zinazojengwa na shirika kwa ajili ya kuuza kwa wananchi wa kipato cha chini na kati.
Pia, ilisema licha ya Serikali kuondoa VAT na ushuru wa Forodha kwa shirika NHC kwa vifaa vya ujenzi inavyoagiza nje, inaishauri kuliondolea pia shirika hilo VAT kwa vifaa vya ujenzi vinavyozalishwa nchini.
Aidha, imeitaka Serikali kulipa deni lililobaki la Sh 4,226,957,203.65 kwa NHC kutokana na madeni ya Wizara, Taasisi na Idara za Serikali.

No comments: