BAJETI YA OFISI YA MAKAMU WA PILI WA RAIS


HOTUBA YA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI
YA OFISI YA MAKAMU WA PILI WA RAIS
KWA MWAKA WA FEDHA
 2014/2015

UTANGULIZI
1.0       Mheshimiwa Spika, naomba kutoa Hoja kwamba Baraza lako Tukufu likae kama Kamati ya Mapato na Matumizi ili lipokee, lijadili na hatimae liidhinishe Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya   Makamu   wa Pili wa Rais kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2014/2015.

2.0       Mheshimiwa Spika, tumekutana tena katika kikao hiki cha nne cha Bajeti ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye Muundo wa Umoja wa Kitaifa kwa mwaka wa fedha 2014/2015 kwa ajili ya kuzungumzia mipango na masuala muhimu ya nchi yetu kwa nia ya kuleta maendeleo ya nchi na wananchi wake.  Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uwezo huu wa kukutana tena na ninamuomba aendelee kutupa afya njema na kutuwezesha kuendesha kikao chetu hiki kwa hekima, busara na uadilifu mkubwa. Ni imani yangu kuwa tutamaliza kikao hiki tukiwa tunaendelea kubakia wamoja na wenye mshikamano mkubwa katika kuendeleza nchi yetu.

3.0       Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kumshukuru kwa dhati Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein kwa kuiongoza nchi yetu kwa umahiri na umakini mkubwa. Sote ni mashahidi kuwa chini ya uongozi wa Dkt.  Ali Mohamed Shein, nchi yetu imeendelea kupata mafanikio makubwa katika nyanja zote za kiuchumi, kijamii na kisiasa. Aidha, nchi yetu imeendelea kuwa katika hali ya amani na utulivu mkubwa hali ambayo imetoa nafasi kwa wananchi kuendelea na shughuli zao za maisha za kila siku bila bughudha wala usumbufu wowote. Namuomba Mwenyezi Mungu aendelee kumpa afya njema na umri mrefu yeye na familia yake, amzidishie hekima na busara ili aendelee kutuongoza katika hatua za kuiletea nchi yetu maendeleo zaidi.

4.0       Mheshimiwa Spika, vilevile, nachukua nafasi hii kumshukuru kwa dhati Mheshimiwa Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad kwa kuendelea kumsaidia na kumshauri vyema Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapindunzi na  kwa  mashirikiano yake mazuri kwa Ofisi yangu.

5.0       Mheshimiwa Spika, pongezi za pekee nazitoa kwako wewe mwenyewe binafsi Mheshimiwa Spika kwa jinsi unavyoliendesha Baraza letu hili kwa umahiri na umakini mkubwa kwa kufuata sheria na kanuni za Baraza. Uongozi wako wa busara kwa hakika umeimarisha demokrasia ndani ya Baraza na kulipa Baraza letu mafanikio makubwa katika kutekeleza majukumu yake. Tunakuombea kwa Mwenyezi Mungu akuzidishie uwezo na hekima katika kutekeleza majukumu yako makubwa katika Taifa letu.  Pia napenda kuwapongeza kwa dhati Naibu Spika Mhe. Ali Abdalla Ali Mwakilishi wa Jimbo la Mfenesini na Wenyeviti wa Baraza Mhe.  Mgeni Hassan Juma, Mwakilishi wa Viti Maalumu na Mhe. Mahmoud Mohamed Mussa, Mwakilishi wa Jimbo la Kikwajuni kwa namna wanavyokusaidia katika kuliendesha Baraza letu hili.

6.0       Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii pia kuwashukuru Wenyeviti na Wajumbe wa Kamati za Kudumu za Baraza la Wawakilishi kwa kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa malengo na maagizo mbalimbali wanayoyatoa kwa Wizara wanazozisimamia. Aidha, natoa shukrani maalum kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa Mhe. Hamza Hassan Juma, Mwakilishi wa Jimbo la Kwamtipura, Makamu Mwenyekiti Mhe. Saleh Nassor Juma Mwakilishi wa Jimbo la Wawi na Wajumbe wote wa Kamati hiyo kwa kuyapitia Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais na kutupa ushauri unaotuongoza na kutusaidia katika utekelezaji wa malengo na majukumu ya Ofisi yetu.

7.0       Mheshimiwa Spika, pia nawapongeza wajumbe wote wa Baraza hili Tukufu kwa kuipitisha Bajeti ya Serikali iliyowasilishwa na Mheshimiwa Waziri wa Fedha. Bajeti hiyo ndiyo itakayotuwezesha kuendesha kazi za Serikali katika kipindi cha mwaka wa fedha 2014/2015.

HALI YA SIASA

8.0       Mheshimiwa Spika, tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kuijaalia nchi yetu amani na utulivu. Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2013/2014 hakukua na matukio makubwa ya uvunjifu wa amani yaliyotokea katika nchi yetu. Hali hii inatokana na wananchi wengi kuzidi kuelewa umuhimu wa amani na kushirikiana na Serikali yao kudumisha amani na utulivu kwa maendeleo ya Taifa letu na Ustawi wa jamii.   

9.0       Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2013/2014, nchi yetu imefanya chaguzi ndogo mbili (2) ambazo zilihusisha Uchaguzi wa Mwakilishi wa Jimbo la Kiembesamaki Wilaya ya Magharibi Unguja na Uchaguzi wa Diwani Wadi ya Kiboje Wilaya ya Kati Unguja. Tunavishukuru vyama vyote vya siasa vilivyoshiriki katika chaguzi hizo ambazo ziliendeshwa kwa haki, uwazi, amani na utulivu mkubwa. Aidha, tunawapongeza sana viongozi walioshinda katika chaguzi hizo na tunawatakia mafanikio katika kuwatumikia wananchi waliowachagua na nchi yetu kwa ujumla. Vilevile, nachukua nafasi hii kuwashukuru na kuwapongeza sana wananchi wa Jimbo la Kiembesamaki  na wananchi wa Wadi ya Kiboje kwa kuweza kutumia demokrasia yao vizuri kuwachagua viongozi wao kwa imani ya kuwaletea maendeleo katika maeneo yao.

MAADHIMISHO YA SHEREHE ZA MIAKA 50 YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR

10.0   Mheshimiwa Spika, katika mwaka huu wa fedha, nchi yetu imeadhimisha Miaka 50 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. Maadhimisho ya Sherehe hizo yalizinduliwa rasmi tarehe 15 Agosti, 2013 na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein na kufikia kilele chake tarehe 12 Januari, 2014, Uwanja wa Amani, Zanzibar.

11.0   Mheshimiwa Spika, kwa muda wote wa maadhimisho haya hadi siku ya kilele tumeshuhudia shughuli na matukio mbalimbali ambayo wananchi na viongozi walishiriki kikamilifu katika maeneo yote ya Unguja na Pemba. Miongoni mwa matukio hayo ni Maonesho ya Miaka 50 ya Mapinduzi yaliyofanyika katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Taifa (SUZA), Kampasi ya Beit el Ras kuanzia tarehe 2 – 5 Januari, 2014; Maonesho ya Fensi; Maonesho ya Biashara yaliyofanyika katika viwanja vya Maisara; Utoaji wa Nishani kwa viongozi na wananchi mbalimbali waliotoa mchango wao katika Mapinduzi ya Januari 12, 1964 pamoja na waliochangia katika maendeleo ya Zanzibar kwa jumla; Matamasha ya Michezo na Burudani, Ujenzi wa Mnara wa Kumbukumbu ya Miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar hapo Michenzani, Uwekaji wa jiwe la msingi na uzinduzi wa miradi ya maendeleo na maonesho mbalimbali yaliyofanywa siku ya kilele katika Uwanja wa Amani.
12.0   Mheshimiwa Spika, sote ni mashahidi wa namna sherehe zetu hizi zilivyokuwa zimefana sana na kuleta haiba kubwa kwa nchi yetu. Hii imeonesha jinsi gani wananchi wetu wanavyothamini Mapinduzi yetu ya Januari 1964 pamoja na maendeleo wanayoyaona kutokana na Mapinduzi hayo.

13.0   Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako napenda kutoa pongezi na shukurani zangu za dhati kwa wananchi na viongozi wote walioshiriki kwa njia moja au nyengine katika kufanikisha Maadhimisho ya Sherehe hizo. Ni matumaini yangu kuwa sote kwa umoja wetu tutaendelea kudumisha Mapinduzi haya ili kuendeleza amani na maendeleo katika nchi yetu.

14.0   Mheshimiwa Spika, pamoja na kutoa pongezi hizo, naomba kutoa masikitiko yangu kuona kwamba hadi leo hii wapo watu wachache miongoni mwetu ambao wanauliza uhalali wa Mapinduzi Matukufu ya Mwaka 1964. Ni dhahiri kwamba hata hawa wanaohoji uhalali wa Mapinduzi kwa kiasi kikubwa wamefaidika na Mapinduzi haya.  Mwenye macho haambiwi tazama kwani baada ya Mapinduzi ya 1964 ndio nchi hii imeshuhudia mafanikio makubwa ya maendeleo katika nyanja zote. Hivyo hatuna budi kuyalinda na kuyaendeleza Mapinduzi yetu kwa manufaa yetu na vizazi vijavyo.

15.0   Mheshimiwa Spika, dhana ya Mapinduzi ilikuwa ni kuleta maisha bora kwa kila Mzanzibari na kuondoa ubaguzi wa aina zote na kuleta umoja na maendeleo na ndio kilichofanyika. Haya mengi ambayo leo tunayaona hayakuwepo kabla ya Mapinduzi ambayo ni pamoja na kuwepo kwa nyumba bora za kuishi, kuimarika kwa huduma za elimu, afya na kupatikana kwa maendeleo makubwa katika Sekta ya Miundombinu, Kilimo, Maji na Umeme, Uchumi na Biashara, na kuwepo kwa uhuru wa kushiriki shughuli za siasa.

16.0   Mheshimiwa Spika, naomba tuelewe kwa nini tunatoa kipaumbele katika kuweka kumbukumbu za Mapinduzi hasa katika maadhimisho yake. Kwa kweli ni jambo la ajabu kuona miongoni mwetu bado wapo watu wanaohoji umuhimu wa Sherehe za Mapinduzi au kuweka vielelezo vya Mapinduzi. Tunasema tutaendelea kuenzi na kuheshimu kazi nzuri iliyofanywa na Wazee wetu ya kutukomboa na kutupatia Uhuru wa nchi yetu.

17.0   Mheshimiwa Spika, kwa ajili ya kuweka kumbukumbu ya kutimiza miaka 50 ya Mapinduzi, Serikali kwa makusudi imefanya uamuzi wa kujenga Mnara katika eneo la Michenzani. Hii inatokana na historia ya eneo hilo katika harakati za kuikomboa nchi yetu. Aidha, Serikali ina dhamira ya dhati ya kuendeleza azma ya Marehemu Mzee Abeid Amani Karume ya kuendeleza eneo hilo na kulifanya kuwa eneo la biashara na kuwa kivutio kwa wageni, watalii na wananchi kwa ujumla.

18.0   Mheshimiwa Spika, mnara unaoendelea kujengwa utakuwa pia ni kituo kwa wananchi na wageni kusoma historia ya Mapinduzi na waanzilishi wake kwani kutakuwa na maktaba maalum. Katika eneo hilo kutakuwa na mkahawa na bustani ya mapumziko ambayo itasaidia sana kupunguza msongamano katika maeneo ya Forodhani hasa wakati wa sikukuu. Naomba wananchi waelewe kuwa mnara huo unajengwa kwa Fedha za Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (ZSSF) na utaendeshwa kibiashara na kwa faida.

MASUALA YA MUUNGANO

19.0   Mheshimiwa Spika, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar hivi sasa umetimiza miaka 50 (Nusu Karne) tangu ulipoasisiwa tarehe 26 Aprili, 1964. Sherehe za kutimiza Miaka 50 ya Muungano wetu zilizinduliwa rasmi hapa Zanzibar na Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi tarehe 01 Machi, 2014 katika Ukumbi wa Salama, Hoteli ya Bwawani na kilele chake kilifanyika Dar es salaam tarehe 26 Aprili, 2014. Kipindi cha miaka 50 ni kirefu na nchi yetu ina kila sababu za kujivunia kutokana na kuudumisha Muungano wetu kwa kipindi chote hicho. Yapo mafanikio mengi yanayotokana na Muungano, lakini makubwa kati ya mafanikio hayo ni kuwa na amani na utulivu katika nchi yetu. Aidha, Muungano huu umeweza kutoa fursa ya kuendeleza na kuimarisha mahusiano ya kidugu yaliyopo kati ya wananchi wa Tanzania Bara na Zanzibar.

20.0   Mheshimiwa Spika, licha ya kuwa na mafanikio hayo, Muungano wetu huu umekuwa na changamoto katika baadhi ya maeneo ambazo zimekuwa zikipigiwa kelele na wananchi wa pande zote mbili za Muungano. Juhudi kubwa tayari zimechukuliwa na viongozi wetu katika kuzitafutia ufumbuzi changamoto hizo ili kuimarisha Muungano wetu huu wa kihistoria. Mambo ambayo mpaka sasa yameshapatiwa ufumbuzi kupitia Kamati Maalumu inayoongozwa na Mhe, Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ni kama yafuatayo:-
·      Utekelezaji wa Sheria ya Haki za Binaadamu.
·      Utekelezaji wa “Merchant Shipping Act” katika Jamhuri ya Muungano na uwezo wa Zanzibar kujiunga na Shirika la Kimataifa la Usafiri Baharini [International Maritime Organisation (IMO)].
·      Misamaha ya mikopo ya fedha kutoka IMF.
·      Uwezo wa Zanzibar kukopa ndani na nje nchi.
·      Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo wa SMT.
·      Kodi ya Mapato (Mgao wa Mapato yatokanayo na PAYE).

21.0   Mheshimiwa Spika, pamoja na mambo ambayo yameshapatiwa  ufumbuzi  kuna mambo ambayo yapo katika hatua nzuri ya kupatiwa ufumbuzi,  mambo hayo ni kama yafuatayo:-
·      Mgawanyo wa mapato yatokanayo na faida ya Benki Kuu.
·      Utafutaji na uchimbaji mafuta na gesi asili.
·      Ushirikiano na Zanzibar na Taasisi za nje.
·      Ajira kwa watumishi wa Zanzibar katika Taasisi za Muungano.
·      Usajili wa vyombo vya moto.
·      Tume ya pamoja ya fedha.
·      Ushiriki wa Zanzibar katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

HALI YA UCHUMI NA MIPANGO YA SERIKALI YA KUIMARISHA UCHUMI

22.0   Mheshimiwa Spika, Uchumi wa Zanzibar umeendelea kuonesha mwenendo mzuri na umeendelea kukua kwa asilimia 7.4 mwaka 2013 kutoka asilimia 7.1 mwaka 2012. Uchumi huu umekua kwa kipindi cha miaka minne (4) kutoka asilimia 6.4 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 7.4 mwaka 2013. Pato la Taifa kwa bei za miaka husika limefikia jumla ya Sh. 1,442.8 bilioni kwa mwaka 2013 kutoka Sh. 1,342.6 bilioni kwa mwaka 2012.

23.0   Mheshimiwa Spika, mwaka 2013 pato la kila mtu limeongezeka kufikia wastani wa Sh. 1,077,000 (USD 667) kutoka wastani wa Sh. 1,030,000 (USD 656) kwa mwaka 2012 sawa na ongezeko la asilimia 4.3. Ukuaji huu mkubwa wa Uchumi umechangiwa na mambo yafuatayo:-

                   i.     Kuimarika kwa Sekta ya Kilimo, Misitu na Uvuvi ambayo imekua kutoka asilimia 2.0 mwaka 2012 hadi asilimia 3.6 mwaka 2013.
                 ii.     Kuimarika kwa baadhi ya Sekta ya Viwanda kulikochangiwa na ongezeko la ukuaji wa Sekta ndogo ya uzalishaji viwandani kutoka asilimia 0.1 kwa mwaka 2012 hadi asilimia 3.2 mwaka 2013.
               iii.     Kuimarika kwa Sekta ya huduma kulikochangiwa na ongezeko la ukuaji wa Sekta ndogo za Hoteli na Mikahawa kutoka asilimia 0.2 mwaka 2012 hadi asilimia 6.5 mwaka 2013, Sekta ya Utawala wa Umma kutoka asilimia 0.3 mwaka 2012 hadi asilimia 3.4, mwaka 2013 na Sekta ya Elimu kutoka asilimia 1.2 mwaka 2012 hadi asilimia 3.5 mwaka 2013.
               iv.     Kuongezeka kwa idadi ya Watalii wanaoingia nchini kutoka Watalii 169,223 mwaka 2012 hadi kufikia Watalii 181,301 mwaka 2013 sawa na ongezeko la asilimia 7.1.

24.0   Mheshimiwa Spika, mafanikio ya kukua kwa Uchumi yanatokana pamoja na sababu zilizotajwa hapo  juu,  na  hali ya utulivu, amani na mshikamano wa wananchi ambayo imejenga mazingira mazuri ya kuwekeza na kufanyakazi kunakoleta tija kwa nchi.

UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI

25.0   Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kuwainua wananchi kiuchumi, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeshazindua Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi.  Mfuko huo wenye thamani ya shilingi 1.1 bilioni utatoa mikopo kwa wananchi wa makundi mbalimbali yakiwemo kundi la vituo vya kutotolea wajasiriamali, kundi la watu wenye ulemavu, kundi la wanawake na kundi la vijana waliomaliza masomo katika vyuo na Skuli za Sekondari. Pamoja na uzinduzi wa Mfuko huu juhudi nyengine za Serikali katika kuwawezesha wananchi kiuchumi ni kuanzisha kituo cha kulelea na kutotoa wajasiriamali (Incubator Centre), kuendeleza Kongano (Clusters) sita (6) zilizopo na kuanzisha Kongano nyengine tofauti.

26.0   Mheshimiwa Spika, natoa wito kwa wananchi waache ile taabia ya kuona kuwa ajira ni ile ya serikalini. Hivyo basi tunawaomba watumie fursa zilizopo ili kuweza kujiajiri wenyewe na kuendeleza maisha yao ya kila siku.

SEKTA YA HUDUMA ZA KIUCHUMI

27.0   Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha huduma za kiuchumi Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya uimarishaji wa miundombinu ya usafiri ikiwemo miundombinu ya barabara, Bandari na Viwanja vya Ndege. Kwa upande wa barabara, Serikali inaendeleza ujenzi wa barabara mbalimbali Unguja na Pemba pamoja na kutafuta rasilimali kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara zinazoingia ndani ya mji wa Zanzibar.

28.0   Mheshimiwa Spika, kuhusu kuimarisha usafiri wa anga Serikali inaendelea na kukiimarisha Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha  Abeid Amani Karume Unguja na Uwanja wa Ndege wa Pemba kwa upanuzi wa njia za kurukia na kuegeshea ndege na ujenzi wa majengo mapya ya abiria pamoja na uwekaji wa taa katika kiwanja cha Pemba. Kwa upande wa Sekta ya Mawasiliano, Serikali imekamilisha kuandaa Sera ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Zanzibar (TEHAMA) ambayo itatoa muongozo wa matumizi mazuri ya TEHAMA kwa Zanzibar. Aidha, Serikali inaendelea kuziunganisha Wizara na Taasisi za Serikali   katika Mkonga wa Mawasiliano na hadi sasa jumla ya Wizara na Taasisi 56 kati ya 83 zimeshaunganishwa na Mkonga huo.

29.0   Mheshimiwa Spika, kukamilika kwa Mradi wa kulaza waya mpya wa umeme wenye uwezo wa kuchukua “MegaWatts” 100 na mradi wa uimarishaji wa miundombinu ya ndani ya umeme imeimarisha   upatikanaji wa huduma za umeme nchini na kutoa muelekeo kwa kuendelea kukua kwa uchumi wa Zanzibar kwani uwekezaji hasa katika maeneo ya Viwanda, Utalii na Biashara utaongezeka kwa kuwepo umeme wa uhakika. Pamoja na hatua hii iliyofikiwa ya kupatikana kwa umeme, Serikali kwa kushirikiana na Washirika wa Maendeleo inafanya uchambuzi yakinifu (Feasibility Study) katika masuala ya nishati mbadala ikiwemo umeme. Pia, hivi sasa Serikali imo katika kuandaa wataalam wa gesi na mafuta ili kuweza kukabiliana na upungufu wa wataalam wa fani ya nishati ikiwemo utafutaji na uchimbaji wa mafuta hapa nchini.

SEKTA YA HUDUMA ZA JAMII
30.0   Mheshimiwa Spika, maji ni rasilimali ya kimaumbile na ya msingi ambayo ni muhimu kwa kuendeleza maisha.  Umuhimu wa matumizi yake unaonekana kwenye mahitaji ya majumbani, viwandani na matumizi mengine mbalimbali ya kijamii.  Serikali inaendelea na mipango ya kuwapatia wananchi maji safi na salama. Mipango hiyo ni pamoja na uhuishaji, upanuzi na usambazaji wa maji mijini na vijijini inayohusisha uchimbaji wa visima zaidi ya 50, ujenzi wa matangi ya maji, ununuzi na uwekaji wa pampu mpya, ulazaji wa mabomba, ujenzi wa vibanda vya kuwekea pampu za maji na ufungaji wa mita kwa wateja.

31.0   Mheshimiwa Spika, katika kuendeleza upatikanaji na utoaji wa huduma ya maji kwa wananchi, Serikali inaendelea na mipango yake ya kulinda na kuhifadhi vyanzo vya maji kwa kujenga uzio katika vyanzo mbalimbali vya maji na kusogeza karibu huduma za malipo ya maji kwa wananchi kwa kujenga vituo vya kulipia maji katika sehemu mbalimbali nchini.

32.0   Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuwaomba wananchi kuthamini mipango mbalimbali ya kuimarisha upatikanaji wa maji kwa kuongeza ulinzi kwenye miundombinu ya maji na uhifadhi wa vyanzo vya maji kwa kupanda miti.

33.0    Mheshimiwa Spika, kwa upande wa sekta ya Elimu, Serikali inaendelea na juhudi zake za kuwapatia elimu bora wananchi wa Zanzibar. Juhudi hizo ni pamoja na kujenga majengo ya kisasa kwa skuli za Sekondari na Msingi katika Wilaya za Unguja na Pemba, kuajiri walimu zaidi ya 700 walio na Shahada na Stashahada katika masomo ya Sayansi kwa mwaka 2014/2015. Aidha, Serikali inaendelea kutoa mafunzo kazini kwa Walimu yakiwemo ya matumizi ya Lugha ya Kiingereza kwa kufundishia na mafunzo ya matumizi ya Kompyuta. Vilevile Serikali itanunua Vifaa vya Maabara kwa Skuli 100 za Sekondari na Kompyuta kwa Skuli mbili zenye Mchepuo wa Sayansi ya Kompyuta. Pia, juhudi hizo za kuimarisha ubora wa elimu ni pamoja na kuandika na kuchapisha Vitabu vya kiada na Miongozo ya Walimu wa Madarasa ya Tano hadi Darasa la Saba. Serikali vilevile imepanga kuimarisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika elimu kwa kuziunganisha Taasisi za elimu na Mkonga wa Taifa na kuendelea na juhudi za kutumia Teknolojia hii kama nyenzo ya kufundishia na kujifunza.

34.0    Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Sekta ya Afya, Serikali inaendelea na azma yake ya kuhakikisha wananchi wa Zanzibar wanapata huduma bora ya afya ili kufikia malengo ya Dira ya mwaka 2020. Katika kufikia azma hiyo, Serikali imeweka mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuimarisha mifumo ya utoaji wa huduma za afya kwa kuzingatia makundi maalum, kutumia mfumo mpya wa ununuzi wa dawa kupitia Mfumo wa Ununuzi wa Dawa kwa Awamu (Framework Contract).  Aidha, Serikali imepanga kuongeza juhudi za kupata madaktari bingwa katika magonjwa mbalimbali na kuwa na vifaa tiba vya kutosha ili kuweza kutoa huduma zinazohitajika.

MIGOGORO YA ARDHI
35.0   Mheshimiwa Spika, Serikali bado inaendelea kulitafutia ufumbuzi wa kudumu suala la migogoro ya ardhi. Kwa kiasi kikubwa hali hii inatokana na tabia ya wananchi na baadhi ya viongozi kuuza au kukodisha ardhi bila kufuata sheria na taratibu ziliopo nchini. Mhe. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi tayari amelitolea maagizo mara kadhaa suala hili kwa kuwataka viongozi na wananchi kutojihusisha na mambo yoyote yanayopelekea kuwa na migogoro ya ardhi.

36.0   Mheshimiwa Spika, hata hivyo, Serikali inaendelea kuchukua juhudi mbalimbali ili kuhakikisha kuwa migogoro ya ardhi inapatiwa ufumbuzi wa kudumu kupitia vyombo vyake mbalimbali ikiwemo Mahakama ya Ardhi pamoja na Ofisi ya Mrajis wa Ardhi inayoshughulikia usajili wa ardhi na kuwatambua wenye haki ya matumizi ya ardhi husika. Naomba kusisitiza kwa kuwasihi viongozi katika ngazi zote na wananchi kwa ujumla kuacha kujiingiza katika mambo ambayo yanasababisha kutokea kwa migogoro ya ardhi.

MASUALA MTAMBUKA

UKIMWI
37.0   Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na juhudi za kupambana na maradhi ya UKIMWI. Kwa kupitia Mipango na Programu mbalimbali juhudi zinaelekezwa katika kutoa elimu na kudhibiti maambukizi mapya. Aidha, Serikali inaendelea kuwaelimisha wananchi kuacha kuwanyanyapaa wale wote ambao kwa bahati mbaya tayari wameshapata maambukizi ya virusi vinavyosababisha UKIMWI.

Watu Wenye Ulemavu
38.0   Mheshimiwa Spika, Serikali inasimamia utekelezaji wa Mkakati wa kuwapatia haki watu wenye ulemavu na kuwajumuisha katika masuala mbalimbali ya kiuchumi, kijamii na kisiasa. Kwa sasa kumezuka wimbi kubwa la ubakaji wa watu wenye ulemavu. Serikali itahakikisha kuwa wale wote wanaohusika na vitendo hivi vya udhalilishaji wanapatikana na kuchukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria. Watu wenye ulemavu ni binaadamu kama binaadamu wengine hivyo wanastahiki haki na usawa katika jamii kwa nyanja zote. Tusisahau kuwa na sisi pia ni walemavu watarajiwa.

Mapambano Dhidi ya Dawa za Kulevya
39.0   Mheshimiwa Spika, madawa ya kulevya ni moja ya matatizo makubwa ya kiuchumi na kijamii duniani kwa sasa kutokana na athari wanazozipata watumiaji wa dawa hizo ambao wengi wao ni vijana. Zanzibar nayo inakabiliwa na tatizo kubwa la uingizwaji na matumizi ya dawa za kulevya. Janga hili limewakumba vijana wengi ambao ni tegemeo la nchi katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Serikali itasimamia utekelezaji wa Sheria ya Dawa za Kulevya na kudhibiti njia zote za uingizwaji wa dawa hizo na kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wote wanaohusika na uingizaji na utumiaji wa dawa hizo. Aidha, Serikali itaendelea kutoa elimu kwa wananchi wote juu ya madhara ya matumizi ya dawa za kulevya na kuwasaidia wale wote walioacha matumizi ya dawa hizo. Serikali inazidi kutoa wito kwa wananchi kuachana na tabia ya kuingiza na kutumia dawa za kulevya ili kuinusuru nchi na janga hili.

Mazingira
40.0   Mheshimiwa Spika, suala la kutunza mazingira lina umuhimu mkubwa sana katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii na kupunguza umasikini wa wananchi. Suala la mabadiliko ya tabianchi pia limeendelea kuleta athari mbalimbali za kimazingira katika maeneo yetu. Katika kuendeleza juhudi ya kukabiliana na hali ya uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi, Serikali itasimamia sheria na kanuni za utunzaji wa maliasili zisizorejesheka, kutoa elimu juu ya utunzaji wa mazingira na kusimamia utekelezaji wa mkakati wa mabadiliko ya tabianchi ikiwa ni pamoja na masuala ya mabadiliko ya tabianchi kuingizwa katika mipango ya maendeleo  ya sekta mbalimbali nchini.

41.0   Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa Programu ya upandaji miti katika maeneo mbalimbali ikiwemo katika vyanzo vya maji, misitu ambayo imeathirika na ukataji miti na maeneo ya wazi yaliyoathirika na ukataji wa miti ovyo. Ni vyema wananchi wakazingatia suala zima la utunzaji wa mazingira kwani athari zake kwa  nchi ya kisiwa kama Zanzibar ni kubwa.

SEKTA YA UTUMISHI NA MASLAHI YA WAFANYAKAZI
42.0    Mheshimiwa Spika, Moja ya vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Saba (7) ni kuimarisha sekta ya utumishi wa umma na maslahi ya wafanyakazi ikiwa na lengo la kuwepo kwa ufanisi na uwajibikaji katika utendaji wa shughuli za utumishi, uadilifu na usimamizi mzuri wa rasilimali za umma. Ili kufikia lengo hili serikali imetekeleza mageuzi makuu ya msingi yakiwemo mageuzi ya utumishi wa umma na kuimarisha serikali katika masuala ya uwajibikaji na uongozi.

43.0   Mheshimiwa Spika, mageuzi haya yamejumuisha mambo yafuatayo:
                   i.     Kufanya tathmini na ufuatiliaji wa utekelezaji wa Miundo ya Utumishi wa Wizara, Idara na Taasisi zote za Serikali.
                 ii.     Kuimarisha utendaji wa taasisi za umma ikiwemo miundombinu, mifumo ya utoaji huduma, kusimamia na kuendeleza watumishi wa umma pamoja na mageuzi ya Serikali za mitaa.
               iii.     Kufanya Tathmini ya Uchambuzi wa Kazi na Madaraja (Job Evaluation and Grading).
               iv.     Kufanya tathmini ya idadi ya watumishi wa umma na majukumu yaliyopo.
                 v.     Kuandaa Mpango Mkakati wa Sera ya Malipo na Sera ya Uhifadhi Kumbukumbu na Nyaraka.

44.0   Mheshimiwa Spika, pamoja na mipango hiyo Serikali itaendelea kutoa umuhimu kwa mafunzo kwa Watumishi wa Umma kwa kuwapatia mafunzo ya muda mrefu, muda mfupi na semina elekezi ili kuwajengea uwezo wafanyakazi katika kutekeleza majukumu yao. Aidha, Serikali imefanya marekebisho makubwa ya mishahara, kwa kuongeza mishahara ya wafanyakazi kwa mujibu wa viwango vya elimu na uzoefu kazini.


MWELEKEO WA VIPAUMBELE VYA OFISI YA MAKAMU WA PILI WA RAIS KWA MWAKA WA FEDHA 2014/2015

45.0   Mheshimiwa Spika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais katika kutekeleza majukumu yake katika mwaka wa fedha 2014/2015 imejipangia kutekeleza vipaumbele vifuatavyo:
                        i.         Kuimarisha huduma za usafiri na makaazi ya Mheshimiwa Makamu wa Pili wa Rais.
                      ii.         Kuongeza hadhi katika Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa.
                    iii.         Kujenga uwezo wa kiutendaji kwa wafanyakazi wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais kwa kuwapatia mafunzo na vitendea kazi.
                    iv.         Kujenga uwezo wa jamii katika kujikinga, kukabiliana na kuhimili majanga na maafa.
                      v.         Kushughulikia malalamiko na migogoro ya wananchi kwa kushirikiana na Sekta husika.
                    vi.         Kusimamia masuala ya utafiti kwa kuzingatia vipaumbele vya Taifa vya Utafiti (National Research Agenda).
                  vii.         Kuweka Muundo mpya wa Kitaasisi na Kiutumishi wa Ofisi ya Uratibu wa Shughuli za Serikali Dar es Salaam utakaoongeza ufanisi na tija.
                viii.         Kuongeza mapato yatokanayo na kuongezeka kwa huduma za upigaji chapa.
                    ix.         Kuandaa mazingira bora kwa ajili ya kufanikisha Uchaguzi Mkuu wa 2015, ikiwemo kutoa elimu ya Wapiga Kura, kufanya uchunguzi wa idadi, majina na mipaka ya majimbo na kufanya mapitio ya Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
                      x.         Kuendesha mikutano ya Baraza la Wawakilishi na kusimamia kazi za Kamati za Kudumu za Baraza.

UTEKELEZAJI WA MALENGO KWA MWAKA WA FEDHA 2013/2014 NA MALENGO YALIYOPANGWA KWA MWAKA WA FEDHA 2014/2015

46.0   Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/2014, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais na Taasisi zake ilikadiriwa kutumia jumla ya Sh.  30,066,506,000. Kati ya hizo Sh. 22,094,970,000 ni kwa kazi za kawaida na Sh. 7,971,536,000 ni kwa kazi za maendeleo. Hadi kufikia mwezi Machi 2014, Ofisi iliingiziwa Sh. 19,416,893,755 (sawa na asilimia 65). Kati ya hizo Sh. 15,837,895,300 ni kwa kazi za kawaida (sawa na asilimia 72) na Sh. 3,578,998,455 kwa kazi za maendeleo (sawa na asilimia 45). [Kiambatanisho Nam. 1A na 1B].

47.0   Mheshimiwa Spika, baada ya kutoa taarifa za jumla za utekelezaji kifedha kwa mwaka 2013/2014, sasa naomba kutoa taarifa za utekelezaji kwa kila idara na taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais.


OFISI YA FARAGHA YA MAKAMU WA PILI WA RAIS

48.0   Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Faragha ina jukumu la kutoa huduma zote muhimu kwa Mhe.  Makamu wa Pili wa Rais na familia yake pamoja na kutunza makaazi ya Makamu wa Pili wa Rais yaliyoko Mazizini Unguja, Dar es Salaam na Dodoma.

49.0   Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2013/2014 Baraza lako Tukufu liliidhinisha jumla ya Sh. 780,034,000 kwa Idara ya Faragha.  Hadi kufikia mwezi Machi, 2014 Idara iliingiziwa jumla ya Sh. 317,824,974 kwa ajili ya kazi za kawaida ambazo ni sawa na asilimia 41.

50.0   Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014 Ofisi ya Faragha imetekeleza kazi zifuatazo:-
                 i.     Ofisi imefanya ununuzi wa vifaa muhimu vya kuendeshea ofisi, matengenezo ya magari na vifaa na kulipia huduma ya simu na faksi.
               ii.     Matengenezo madogo madogo yamefanywa kwa makaazi ya Mhe. Makamu wa Pili wa Rais ya Dar es Salaam na kulipia huduma muhimu kwa makaazi ya Unguja, Dares-Salaam na Dodoma.
             iii.     Ofisi imeratibu mikutano ya Mheshimiwa Makamu wa Pili wa Rais na Mabalozi na Wanadiplomasia 11 ikiwemo Marekani, Kenya, Israel, Malaysia, Nigeria, India, China waliopo nchini Tanzania na ujumbe wa Serikali ya Oman.
             iv.     Ofisi imeratibu ziara 15 za ndani ya nchi [Pemba saba (7), Dar-es-Salaam tano (5), Dodoma moja (1) na Arusha mbili (2)] na ziara mbili (2) za nje (Marekani na Falme za Nchi za Kiarabu) za Mheshimiwa Makamu wa Pili wa Rais.
               v.     Ofisi imeratibu mazungumzo ya upatanishi wa migogoro ya wananchi ambapo mgogoro wa mpaka wa wananchi wa Donge Muwanda tayari umetatuliwa.  Aidha, mgogoro wa wananchi wa Kiombamvua na muwekezaji wa hoteli ya Sea Cliff iliyopo Kama Wilaya ya Kaskazini “B” umefikia katika hatua nzuri ambapo bado Serikali inaendelea kuufanyia kazi kutokana na matatizo mapya yaliyojitokeza kwa utaratibu maalum.
             vi.     Ofisi imeratibu na kufuatilia ahadi 11 zilizotolewa na Mheshimiwa Makamu wa Pili wa Rais kati ya hizo ahadi saba (7) zimetekelezwa

51.0   Mheshimiwa Spika katika mwaka wa fedha 2014/2015 Ofisi ya Faragha imepanga kutekeleza malengo yafuatayo:-

               i.         Kuimarisha Ofisi ya Faragha ya Makamu wa Pili wa Rais kwa ununuzi wa gari moja, samani na vifaa vya ofisi.
             ii.         Kuratibu ziara 20 za ndani ya nchi na mbili za nje ya nchi za Mheshimiwa Makamu wa Pili wa Rais.
           iii.         Kuwajengea uwezo wafanyakazi wawili (2) wa Idara kwa kuwapatia mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu pamoja na kulipa stahiki za likizo kwa wafanyakazi wanne (4).
           iv.         Kuimarisha makaazi ya Mheshimiwa Makamu wa Pili wa Rais kwa kuzifanyia matengenezo nyumba za Mazizini, Dar es Salaam na Dodoma.
             v.         Kuimarisha uhusiano na ushirikiano na nchi na taasisi mbalimbali za ndani, kikanda na kimataifa.

52.0    Mheshimiwa Spika, ili Ofisi ya Faragha iweze kutekeleza malengo yake kwa mwaka wa fedha 2014/2015 naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe jumla ya Sh 483,116,224 kwa matumizi ya Ofisi. Kati ya hizo Sh 330,616,224 kwa malipo ya mishahara, posho za wafanyakazi na michango ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii na Sh 152,500,000 kwa matumizi mengineyo.IDARA YA UENDESHAJI NA UTUMISHI

53.0   Mheshimiwa Spika, Idara ya Uendeshaji na Utumishi ina wajibu wa kusimamia stahiki za watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais na kusimamia mafunzo kwa wafanyakazi. Aidha, Idara ina jukumu la kusimamia usalama na mazingira bora ya kazi pamoja na uendeshaji wa kazi za kila siku za Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais.

54.0   Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2013/2014 Baraza lako Tukufu liliidhinisha jumla ya Sh. 1,004,880,000 kwa Idara ya Uendeshaji na Utumishi. Hadi kufikia mwezi Machi, 2014 Idara iliingiziwa jumla ya Sh.  577,298,515 kwa kazi za kawaida ambazo ni sawa na asilimia 57.

55.0   Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2013/2014 Idara ya Uendeshaji na Utumishi imetekeleza kazi zifuatazo:-
                      i.  Idara imeendelea kuratibu na kuwalipia ada na gharama nyengine za masomo kwa wafanyakazi 66 wanaoendelea na masomo ndani na nje ya nchi. (Kiambatanisho Nam. 2)
                    ii.  Kulipia stahiki za wafanyakazi zikiwemo likizo kwa wafanyakazi saba (7), malipo baada ya saa za kazi na kutayarisha mafao kwa watumishi sita (6) waliostaafu.
                  iii.  Idara imefanya semina elekezi kuhusu Sheria ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2011 na elimu ya kujikinga na maambukizi mapya ya UKIMWI.
                  iv.  Idara imenunua vifaa vya kufanyia kazi ikiwemo mashine ya kurudufia (photocopy) na “projector” moja kwa lengo la kujenga mazingira bora ya kazi.
                    v.  Idara imeweza kudhamini wafanyakazi 46 kupata  mikopo ya kifedha yenye thamani ya Sh. 202,137,540 katika taasisi mbali mbali za kifedha.

56.0   Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2014/2015 Idara ya Uendeshaji na Utumishi imepanga kutekeleza malengo yafuatayo:-
                   i.       Kuweka mazingira mazuri ya kazi za idara kwa ununuzi wa vifaa vya ofisi, samani pamoja na kulipia gharama za umeme na mawasiliano na utunzaji wa majengo.
                 ii.       Kuwajengea uwezo wafanyakazi kumi (10) wa idara kwa kuwapatia mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu pamoja na kulipa stahiki za likizo kwa wafanyakazi tisa (9).
               iii.       Kuufanyia mapitio Mpango wa Mafunzo kwa wafanyakazi pamoja na kuandaa utaratibu wa kutathmini utendaji kazi (Staff Appraisal System) na upandishaji vyeo wafanyakazi kwa kufuata muundo wa utumishi (Scheme of Service).
               iv.       Kusimamia matumizi bora ya fedha na vifaa vya ofisi kwa kuandaa vikao vinne (4) vya Kamati ya Uongozi, vikao vinne (4) vya Bodi ya Zabuni, Vikao vinne (4) vya Kamati ya Ukaguzi wa ndani na kulifanyia mapitio Daftari la Mali za Serikali (Asset Registry).

57.0   Mheshimiwa Spika, ili idara ya Uendeshaji na Utumishi iweze kutekeleza    malengo yake kwa mwaka wa fedha 2014/2015 naliomba Baraza lako tukufu liidhinishe jumla ya Sh. 704,166,316. Kati ya hizo Sh. 514,166,316  ni kwa malipo ya mishahara, posho na mchango wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii na Sh. 190,000,000 ni kwa matumizi mengineyo.

IDARA YA MIPANGO, SERA NA UTAFITI
58.0   Mheshimiwa Spika, Idara ya Mipango, Sera na Utafiti inaendelea na jukumu la kusimamia masuala ya mipango, bajeti, sera na utafiti.  Pia Idara hii ina jukumu la kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na kutayarisha ripoti za utekelezaji wa shughuli za kawaida na miradi ya maendeleo kwa kipindi cha miezi mitatu, miezi sita, miezi tisa  na mwaka mzima.

59.0   Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2013/2014 Baraza lako Tukufu liliidhinisha jumla ya Sh. 295,240,000 kwa Idara ya Mipango, Sera na Utafiti. Hadi kufikia mwezi Machi, 2014 Idara iliingiziwa jumla ya Sh. 125,771,732 kwa kazi za kawaida ambazo ni sawa na asilimia 43.

60.0   Mheshimiwa Spika, Idara ya Mipango, Sera na Utafiti katika mwaka wa fedha wa 2013/2014 imetekeleza kazi zifuatazo:-

                   i.       Idara imelipa stahiki za wafanyakazi wanne (4) waliokwenda likizo.
                 ii.       Idara imefanya semina ya siku mbili kwa wafanyakazi juu ya Sheria ya Utumishi wa Umma.
               iii.       Idara imenunua vifaa vya kufanyia kazi ikiwemo Projekta moja (1), Printa moja (1) na vifaa vya kuandikia.
               iv.       Idara imefanya ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo iliyo chini ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais.
                 v.       Idara imeratibu utekelezaji wa Miradi ya Mfuko wa Dunia (Global Fund) ya Kupambana na UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria.
               vi.       Idara imeandaa Mpango Mkakati wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais.
             vii.       Idara imeandaa Bajeti na Hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais kwa mwaka wa fedha 2014/2015.
           viii.       Idara imeandaa ripoti za utekelezaji kwa shughuli za kawaida na Miradi ya maendeleo kwa robo mwaka, nusu mwaka na miezi tisa. Pia imefanya vikao vya kupitia na kutathmini ripoti hizo.
               ix.       Idara imetoa vibali 110 vya kufanya utafiti katika sekta za mazingira, historia, kilimo, maliasili, misitu na elimu. Aidha, Idara imeratibu vikao vinne; viwili vya Kamati ya Taifa ya Utafiti na viwili kwa Kamati ya Wataalamu ya Kutafiti Rasilimali za Asili.
                 x.       Idara kwa kushirikiana na COSTECH imetekeleza kazi zifuatazo:-
§   Imeratibu kikao cha Kamati ya Taifa ya Wataalamu ya Rasilimali za Asili juu ya kupitia vipaumbele vya utafiti   (National Research Agenda).
§   Imeratibu mkutano wa siku tatu wa mashirikiano baina ya Afrika ya Kusini na Tanzania juu ya masuala ya Utafiti.
§   Idara kwa kushirikiana na COSTECH, SUZA na Chuo Cha Sayansi ya Afya imeratibu na kushiriki Siku ya Utafiti na Ugunduzi ikiwa ni moja ya shughuli za maadhimisho ya sherehe za Miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

61.0   Mheshimiwa Spika, Kwa mwaka wa fedha wa 2014/2015 Idara ya  Mipango, Sera na Utafiti imepanga kutekeleza malengo yafuatayo:-
                   i.       Kuweka mazingira mazuri ya kazi za idara kwa ununuzi wa vifaa vya ofisi na samani.
                 ii.       Kuwajengea uwezo wafanyakazi 11 wa idara kwa kuwapatia mafunzo ya muda mfupi na wafanyakazi watatu (3) kwa mafunzo ya muda mrefu na kulipa stahiki za likizo kwa wafanyakazi watatu (3)
               iii.       Kuufanyia mapitio Mpango Mkakati wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais na kutayarisha Miradi mitatu ya Maendeleo
               iv.       Kuandaa Bajeti  kwa Mwaka wa Fedha 2015/2016 na kufanya ziara nne (4) za ufuatiliaji wa kazi za Wizara na  utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais
                 v.       Kuandaa vikao 12 vya Kamati ya Kisekta  ya kuidhinisha Tafiti mbalimbali  na Vikao vinne  vya Kamati ya Taifa ya Kutafiti Rasilimali za Asili
               vi.       Kwa kushirikiana na COSTECH  kuwajengea uwezo watafiti wa wizara za SMZ kwa kuandaa warsha mbili pamoja  na kuweka  utaratibu mzuri wa utoaji wa vibali vya Utafiti
             vii.       Kuratibu utekelezaji wa Miradi ya Mfuko wa Dunia (Global Fund) ya Kupambana na UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria

62.0   Mheshimiwa Spika, Ili Idara ya Mipango, Sera na Utafiti iweze kutekeleza malengo yake katika mwaka wa fedha 2014/2015 naliomba Baraza lako Tukufu kuidhinisha jumla ya Sh 184,007,400 kwa matumizi ya Idara.  Kati ya hizo Sh. 100,718,400 kwa ajili ya malipo ya mishahara, posho za wafanyakazi na mchango wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii na Sh. 83,289,000 kwa matumizi mengineyo.IDARA YA URATIBU WA SHUGHULI ZA SERIKALI

63.0   Mheshimiwa Spika, Idara ya Uratibu wa Shughuli za Serikali ina jukumu la kuratibu Shughuli za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Shughuli za Muungano ndani ya Zanzibar.

64.0   Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2013/2014 Baraza lako Tukufu liliidhinisha jumla ya Sh. 397,530,000 kwa Idara ya Uratibu wa Shughuli za Serikali. Hadi kufikia mwezi Machi, 2014 Idara iliingiziwa jumla ya Sh. 223,282,110 kwa kazi za kawaida ambazo ni sawa na asilimia 56. Aidha, Idara iliidhinishiwa Sh. 840,000,000 kwa kazi za maendeleo ikiwa ni mchango wa SMZ. Kati ya hizo Sh. 80,000,0000 ni kwa Mradi wa TASAF na Sh. 760,000,000 kwa Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo. Hadi kufikia Machi, 2014, Idara imeingiziwa Sh. 25, 000,000 kwa mradi wa TASAF, sawa na asilimia 31.

65.0   Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014 Idara imetekeleza kazi zifuatazo:-

                   i.       Idara imefuatilia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2010 – 2015 katika Wizara za SMZ na Mikoa yote ya Unguja na Pemba na kuandaa taarifa ya utekelezaji kwa kipindi cha mwaka mmoja (Oktoba 2012 – Septemba 2013).
                 ii.       Idara imetoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kukusanya na kuandaa taarifa za utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi kwa Maafisa viungo wa Wizara, Maafisa Mipango wa Mikoa pamoja na Waratibu wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais.
               iii.       Idara imepokea na inaendelea kuyafuatilia malalamiko 15 (10 yanayohusiana na ardhi na 5 mambo mengine) yaliyowasilishwa na wananchi.
               iv.       Idara imeendelea kufuatilia utekelezaji wa ahadi nane (8) za Viongozi Wakuu wa Kitaifa zilizotolewa katika maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba wakati wa ziara zilizofanywa na viongozi hao.
                 v.        Idara imefuatilia vikao vitatu (3) vya Baraza la Wawakilishi vilivyofanyika katika  mwezi wa Oktoba  Mkutano wa 14, Disemba Mkutano wa 15 na Januari Mkutano wa 16,  Katika Mikutano hiyo jumla ya masuali 221 ya msingi yaliulizwa na kujibiwa. Pia, miswada Saba (7), Ripoti moja ya Kamati Teule na hoja binafsi moja ziwasilishwa.
               vi.       Idara imeratibu vikao saba (7) vya mashirikiano baina ya Wizara za SMZ na SMT ambapo vikao vitatu (3) vimefanyika baina ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali SMZ na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi SMT, vikao vitatu (3) baina ya Wizara ya Kilimo na Maliasili SMZ na Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika SMT, kikao kimoja (1) baina ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu SMZ na SMT.  
             vii.       Idara imeendelea kulipia ada na gharama nyengine za masomo ya muda mrefu kwa wafanyakazi sita (6) na masomo ya muda mfupi kwa wafanyakazi watatu (3) ndani na nje ya nchi.
           viii.       Idara imesimamia utekelezaji wa mradi wa TASAF Awamu ya Tatu (Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini) na kaya masikini 2,675 kwa Unguja na Kaya 4,084 kwa Pemba  zimepatiwa malipo kwa awamu mbili (Januari na Machi 2014). Jumla ya Sh. 432,259,000 zimelipwa kwa Unguja na Pemba. (Kiambatanisho Nam. 3A-3F) 
               ix.       Idara iliandaa semina kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa lengo la kuwapatia uwelewa wajumbe hao kuhusu utekelezaji wa Mradi wa TASAF awamu ya Tatu.
                 x.       Idara imeratibu ziara za mafunzo kwa  Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya zote wa Unguja na Pemba pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Baraza la Wawakilishi ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa waliotembelea eneo la mfano la utekelezaji wa Mradi wa  TASAF awamu  ya Tatu huko Bagamoyo - Tanzania Bara.
               xi.       Idara imetoa mafunzo maalumu kwa wawezeshaji 120 kutoka Wilaya zote za Unguja na Pemba (Unguja 60 na Pemba 60) wa kuibua kaya masikini.
             xii.       Idara imeandaa Rasimu ya Kanuni ya Sheria ya Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo.
           xiii.       Idara imefuatilia utekelezaji wa miradi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo kwa Majimbo yote 50 ya Unguja na Pemba.   Katika ufuatiliaji huo Kamati za kusimamia miradi hiyo zimehimizwa kufanya marejesho ya utekelezaji wa miradi hiyo.
           xiv.       Idara imetoa mafunzo kuhusu utekelezaji wa Sheria ya Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo ya mwaka 2012 kwa Makatibu wa Kamati za Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo kwa  majimbo yote 18 ya Pemba pamoja na Maafisa Mipango wa Mikoa na Wilaya za Pemba.
             xv.       Idara inaendelea kukiimarisha Kitengo cha Habari, Mawasiliano na Elimu (ICE) kwa kununua vifaa na kutoa mafunzo kwa watendaji wa Kitengo hicho.
           xvi.       Tovuti ya Serikali imeimarishwa kwa kuwekwa taarifa mbali mbali za Mawizara na matukio muhimu ikiwemo maadhimisho ya Sherehe mbali mbali za kitaifa na hotuba za Viongozi Wakuu.

66.0    Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2014/2015 Idara imepanga kutekeleza malengo   yafuatayo:-
                        i.   Kuweka mazingira mazuri ya kazi za Idara kwa ununuzi wa vifaa vya ofisi na samani.
                      ii.   Kuwajengea uwezo wafanyakazi wanne (4) wa Idara kwa kuwapatia mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu pamoja na kulipa stahiki za likizo kwa wafanyakazi saba (7).
                    iii.   Kufuatilia  utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kuandaa Taarifa ya utekelezaji kwa kipindi cha Miaka miwili kuanzia Oktoba 2012 – Septemba 2014
                    iv.   Kufuatilia utekelezaji wa Ahadi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa kwa kila robo mwaka
                      v.   Kupokea na kufuatilia malalamiko ya wananchi na kusimamia utatuzi wa migogoro katika jamii.
                    vi.   Kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa Miradi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo katika majimbo 50 ya Unguja na Pemba ambayo yamepatiwa fedha.
                  vii.   Kufuatilia mijadala na utekelezaji wa Ahadi za Serikali zinazotolewa katika vikao vya Baraza la Wawakilishi.
                viii.   Kuratibu vikao  saba (7) vya mashirikiano kati ya Wizara za SMZ na SMT
                    ix.   Kuratibu vikao vinne (4) vya Mawaziri na Makatibu wakuu wa SMZ na SMT na vikao vinne (4) vya Sekretarieti ya Kamati ya Pamoja ya Mambo ya Muungano
                      x.   Kusimamia utoaji wa fedha (Cash Transfer) kwa Kaya masikini za Unguja na Pemba zinazotolewa kupitia Mpango wa TASAF awamu ya Tatu.
                    xi.   Kuimarisha kitengo cha ICE kwa ununuzi wa vifaa vipya na kutoa mafunzo kwa watendaji sita wa Kitengo.

67.0   Mheshimiwa Spika, Ili Idara iweze kutekeleza majukumu yake kwa mwaka 2014/2015 naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe jumla ya Sh. 344,638,000. Kati ya fedha hizo Sh. 247,053,000 kwa malipo ya mishahara, posho za wafanyakazi na mchango wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii na Sh. 97,585,000 kwa matumizi mengineyo. Kwa upande wa Miradi ya Maendeleo naliomba Baraza lako Tukufu kuidhinisha jumla ya Sh. 1,060,000,000. Kati ya hizo Sh. 1,010,000,000 kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo na Sh.  50,000,000 mchango wa Serikali kwa ajili ya Miradi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii – TASAF awamu ya Tatu.

IDARA YA URATIBU WA SHUGHULI ZA SMZ- DAR ES SALAAM.

68.0   Mheshimiwa Spika, Idara ya Uratibu wa Shughuli za SMZ Dar es Salaam imehamishiwa rasmi katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais tangu mwezi wa Septemba 2013. Kabla ya hapo Idara hii ilikuwa chini ya Iliyokuwa Wizara ya Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo.

69.0   Mheshimiwa Spika, Idara hii inajukumu la kuratibu kazi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar huko Tanzania Bara.  Aidha, Idara inaratibu masuala ya SMZ na Ofisi za Balozi mbalimbali zilizopo Tanzania, Wadau wa Maendeleo pamoja na Mashirika ya Kimataifa yenye ofisi zao Dar es Salaam.

70.0   Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2013/2014 Baraza lako Tukufu liliidhinisha jumla ya Sh. 326,970,000 kwa Idara ya Uratibu wa Shughuli za SMZ Dar es Salaam. Hadi kufikia mwezi Machi, 2014 Idara iliingiziwa jumla ya Sh. 119,053,550 kwa kazi za kawaida ambazo ni sawa na asilimia 36.

71.0   Mheshimiwa Spika, Idara ya Uratibu wa Shughuli za SMZ - Dar es Salaam katika mwaka wa fedha 2013/2014 imetekeleza kazi zifuatazo:-
                        i.   Idara ilishiriki kwenye Mkutano wa Nane wa Tume ya pamoja ya Ushirikiano wa kiuchumi, kiufundi na Sayansi baina ya Tanzania na India.  Ambapo India iliahidi kuipatia msaada SMZ katika kuimarisha huduma za Afya.
                      ii.   Idara ilishiriki katika kikao cha mashauriano baina ya Tanzania na Japan, ambapo Zanzibar iliwasilisha mapendekezo ya miradi saba kupitia Tume ya Mipango Tanzania Bara kwa ajili ya kuombewa misaada kutoka Serikali ya Japan (TICAD V).
                    iii.   Idara imeshiriki katika kikao cha wadau kuhusiana na mpango mpya wa ushirikiano baina ya Tanzania na Saudi Arabia, lengo likiwa ni kujenga ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.
                    iv.   Idara ilishiriki katika vikao vya maandalizi ya Mkutano wa Wakuu wa nchi za Afrika na Ufaransa, lengo ilikuwa ni kujadili mabadiliko ya tabianchi, ulinzi na usalama pamoja na mashirikiano ya kiuchumi.
                      v.   Idara ilishiriki katika kikao cha wadau kuhusu mpango mpya wa ushirikiano kati ya Tanzania na Uingereza, lengo kuu ni kujadili sera iliyotolewa na Serikali ya Uingereza na kupendekezwa kuundwa kwa ubia wenye ustawi kati yake na Tanzania “Tanzania – United Kingdom Partnership in Prosperity” kwenye maeneo ya: Nishati Jadilifu (renewable enegy), kilimo na mazingira ya biashara.
                    vi.   Idara ilishiriki katika matayarisho ya Mkutano Mkuu wa Mawaziri unaojadili masuala ya kiuchumi ambao ulifanyika nchini Kenya.

72.0   Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha wa 2014/2015 Idara ya Uratibu wa shughuli za SMZ Dar es Salaam imepanga kutekeleza malengo yafuatayo:-
                        i.   Kuweka mazingira mazuri ya kazi za Idara kwa ununuzi wa vifaa vya ofisi na samani
                      ii.   Kuwajengea uwezo wafanyakazi watatu (3) wa Idara kwa kuwapatia mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu pamoja na kulipa stahiki za likizo kwa wafanyakazi tisa (9).
                    iii.   Kuandaa Muundo mpya wa Kitaasisi na Kiutumishi wa Idara utakaoleta ufanisi zaidi na tija.
                    iv.   Kuimarisha mashirikiano baina ya Idara na Taasisi za SMZ na Taasisi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Ofisi za Kibalozi na Taasisi za Kimataifa.

73.0   Mheshiwa Spika, ili Idara ya Uratibu wa Shughuli za SMZ Dar es Salaam iweze kutekeleza malengo yake katika mwaka wa fedha 2014/2015 naliomba Baraza lako Tukufu kuidhinisha jumla ya Sh. 353,178,160.   Kati ya hizo Sh. 208,178,160 kwa ajili ya malipo ya mishahara, Posho za wafanyakazi na mchango wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii na Sh. 145,000,000 kwa matumizi mengineyo.

IDARA YA KUKABILIANA NA MAAFA

74.0   Mheshimiwa Spika, Idara ya kukabiliana na Maafa ina jukumu la kuratibu masuala ya maafa hapa Zanzibar, kama ilivyoelezwa katika Sheria ya Kukabiliana na Maafa Nam. 2 ya mwaka 2003.

75.0   Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2013/2014 Baraza lako Tukufu liliidhinisha jumla ya Sh. 262,528,000 kwa Idara ya Kukabiliana na Maafa kwa kazi za kawaida. Hadi kufikia mwezi Machi, 2014 Idara iliingiziwa jumla ya Sh. 112,283,620 kwa kazi za kawaida ambazo ni sawa na asilimia 43. Kwa upande wa miradi ya maendeleo Idara iliidhinishiwa Sh. 340,000,000. Kati ya hizo Sh. 70,000,000 ni mchango wa Serikali na Sh. 270,000,000 ni mchango kutoka kwa Washirika wa Maendeleo na hadi kufikia mwezi wa Machi 2014, Idara imeingiziwa Sh.10,000,000 kutoka mchango wa Serikali sawa na asilimia 14. na Sh. 175,176,000 kutoka  kwa Washirika wa Maendeleo sawa na asilimia 65.

76.0   Mheshimiwa Spika, Idara ya Kukabiliana na Maafa katika mwaka fedha wa 2013/2014 imetekeleza kazi kama ifuatavyo: -
                        i.   Idara imepatiwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) gari moja, redio za mawasiliano 10, pikipiki tatu (3) na kompyuta (laptop) nne (4).
                      ii.   Idara imetayarisha na kurusha vipindi 18 vya kukabiliana na maafa kwa lengo la kuelimisha jamii kupitia ZBC Radio.
                    iii.   Idara imetoa mafunzo ya kukabiliana na maafa kwa Shehia 36 zilizofanyiwa tathmini ya kujua uwezo wa kukabiliana na maafa katika Wilaya za Magharibi, Mjini na Kaskazini ‘A’. Mafunzo hayo ni muendelezo wa mafunzo kwa Wilaya zilizopata fursa ya kutengeneza Mpango wa Dharura wa Kukabiliana na Maafa ambapo wilaya za Micheweni na Wete Pemba tayari zimeshatengeneza Mipango na kupatiwa mafunzo. (Kiambatanisho Nam. 4A & 4 B)
                    iv.   Idara imekamilisha Mipango ya Kujiandaa na Kukabiliana na Maafa kwa Wilaya za Mjini, Magharibi na Kaskazini ‘A’.  Mipango kama hii imeshakamilika kwa Wilaya za Wete na Micheweni Pemba.
                      v.   Idara imetoa huduma ya operesheni za uokozi kwa abiria waliopata ajali ya kudondoka katika meli ya MV. Kilimanjaro II iliyotokea katika bahari ya Nungwi tarehe 5 Januari 2014.
                    vi.   Idara imeendesha makongamano mawili (2) ya kukabiliana na maafa kwa wadau wa maafa nchini.
                  vii.   Idara imeandaa Mwongozo wa Mafunzo kwa Wafanyakazi wa Idara ya Kukabiliana na Maafa pamoja na Mkakati wa Kutafuta Nyenzo za Kukabiliana na Maafa wa Zanzibar.
                viii.   Idara imetoa elimu ya kukabiliana na maafa kwa watu wenye ulemavu 100 na wanafunzi wa skuli za msingi na Sekondari (1,200) katika Wilaya za Mjini na Kaskazini ‘A’ Unguja na Chakechake na Mkoani Pemba.
                    ix.   Idara imefanya mikutano miwili (2) Unguja na Pemba ya kuelimisha wadau juu ya Mwongozo wa Kukabiliana na Maafa Zanzibar pamoja na Mwongozo wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Sera ya Kukabiliana na Maafa ya Zanzibar.
                      x.   Idara imelipia gharama za mafunzo ya muda mrefu (Shahada ya Pili) kwa wafanyakazi watatu (3) wa Idara. Wafanyakazi hawa wote wanasomea kada ya kukabiliana na maafa.

77.0   Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Idara imepanga kutekeleza malengo yafuatayo: -

                        i.   Kuweka mazingira mazuri ya kazi za Idara kwa ununuzi wa vifaa vya ofisi na samani.
                      ii.   Idara kwa kushirikiana na Washirikia wa Maendeleo (USAFRICOM, Benki ya Dunia na Kamisheni ya Bahari ya Hindi) itaendesha mafunzo mbalimbali ya kukabiliana na maafa kwa watendaji na wadau wa kukabiliana na maafa pamoja na kuendesha mazoezi mawili (2) ya kukabiliana na maafa.
                    iii.   Kuwajengea uwezo wafanyakazi wanne (4) wa Idara kwa kuwapatia mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu pamoja na kulipa stahiki za likizo kwa wafanyakazi sita (6).
                    iv.   Kuyafanyia matengenezo maghala mawili (2) na kununua vifaa vya kukabiliana na maafa kwa Unguja na Pemba.
                      v.   Kujenga uwezo kwa jamii katika kukabiliana na majanga na maafa kwa Shehia 10.
                    vi.   Kukamilisha sheria mpya ya kukabiliana na maafa.

78.0   Mheshimiwa Spika, ili Idara ya Kukabiliana na Maafa iweze kutekeleza malengo yake katika mwaka wa fedha 2014/2015, naliomba Baraza lako Tukufu kuidhinisha jumla ya Sh. 298,447,800 kwa matumizi ya Idara. Kati ya hizo Sh. 128,875,500 kwa ajili ya malipo ya mishahara, posho za wafanyakazi na mchango wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii na Sh. 169,572,300 kwa matumizi mengineyo. Aidha, naliomba Baraza lako Tukufu kuidhinisha jumla ya Sh. 1,322,880,000 kwa ajili ya Miradi ya maendeleo, Sh. 40,000,000 ikiwa ni mchango wa Serikali na Sh. 1,282,880,000 ni mchango kutoka washirika wa Maendeleo.


IDARA YA SHEREHE NA MAADHIMISHO YA KITAIFA

79.0   Mheshimiwa Spika, Idara ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa ina jukumu la kuratibu Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa pamoja na shughuli za kuwaenzi Viongozi wa Kitaifa. Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa yanayoratibiwa na Idara ni Sherehe za Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, Sherehe za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar pamoja na ushiriki wa Viongozi na wananchi wa Zanzibar katika Sherehe za Uhuru wa Tanganyika. Aidha, kwa upande wa shughuli za kuwaenzi Viongozi wa Kitaifa, Idara inaratibu mazishi ya Viongozi kama ilivyoainishwa kwenye Sheria ya Kuwaenzi Viongozi Nam. 10 ya Mwaka 2002, Hitma na Dua ya Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume pamoja na kutunza kumbukumbu za viongozi hao.

80.0   Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2013/2014 Baraza lako Tukufu liliidhinisha jumla ya Sh. 2,189,103,000 kwa Idara ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa. Hadi kufikia mwezi Machi, 2014 Idara iliingiziwa jumla ya Sh. 2,480,329,652 kwa kazi za kawaida ambazo ni sawa na asilimia 113.

81.0   Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2013/2014, Idara ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa imetekeleza malengo yafuatavyo:-

                      i.       Kuratibu kwa mafanikio makubwa maadhimisho ya Sherehe za Miaka 50 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ambazo zilikuwa za kipekee na za aina yake zilizofikia kilele tarehe 12 Januari 2014.
                    ii.       Idara imeratibu kwa mafanikio makubwa Sherehe za Miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar zilizofanyika katika uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam tarehe tarehe 26 Aprili 2014. Aidha, Idara imeratibu ushiriki wa viongozi na wananchi wa Zanzibar katika Sherehe za miaka 52 ya Uhuru wa Tanganyika zilizofanyika tarehe 09 Disemba, 2013. Kazi hii imefanywa kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu.
                  iii.       Idara imeratibu Hitma na Dua ya Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume iliyofanyika Afisi Kuu ya CCM, Kisiwandui tarehe 7 Aprili, 2014.
                  iv.       Idara imeendelea kukusanya taarifa na kumbukumbu za Marehemu Sheikh Abeid Amaan Karume.
                    v.       Idara imenunua vifaa vya sherehe ikiwemo zulia jekundu na bendera pamoja na kuendelea kulifanyia matengenezo Ghala la Idara lililopo Mwanakwerekwe Unguja.
                  vi.       Idara imewapatia mafunzo ya muda mrefu wafanyakazi wawili (2) wa Idara pamoja na kulipia stahiki   za wafanyakazi wawili (2) waliokwenda likizo.

82.0   Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2014/2015, Idara ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa imepanga kutekeleza malengo yafuatayo:-

                        i.         Kuweka mazingira mazuri ya kazi za idara kwa ununuzi wa vifaa vya ofisi na samani.
                      ii.         Kuwajengea uwezo wafanyakazi wawili (2) wa idara kwa kutoa mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu pamoja na kulipa stahiki za likizo kwa wafanyakazi wawili (2).
                    iii.         Kuratibu na kusimamia sherehe za Miaka 51 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
                    iv.         Kuratibu sherehe za Miaka 51 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na ushiriki wa viongozi na wananchi wa Zanzibar katika Sherehe za miaka 53 ya Uhuru wa Tanganyika kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu.
                      v.         Kuratibu Hitma na Dua ya Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume   (Siku ya Mashujaa).
                    vi.         Kuifanyia mapitio Sheria Namba 10 ya 2002 ya Kuwaenzi Viongozi pamoja na mambo yanayohusiana nayo.
                  vii.         Kuendelea kukusanya na kutunza kumbukumbu za Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume.

83.0   Mheshimiwa Spika, ili Idara ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa iweze kutekeleza malengo yake iliyojipangia kwa mwaka wa fedha 2014/2015, naliomba Baraza lako Tukufu kuidhinisha jumla ya   Sh. 871,615,500 kwa matumizi ya Idara. Kati ya hizo Sh. 87,259,800 kwa malipo ya mishahara, posho za wafanyakazi na mchango wa mfuko wa Hifadhi ya Jamii na Sh. 784,355,700 ni kwa matumizi mengineyo.

IDARA YA UPIGAJI CHAPA NA MPIGA CHAPA MKUU WA SERIKALI 

84.0   Mheshimiwa Spika, Idara ya Upigaji Chapa na Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali ina majukumu ya kuchapisha Miswaada ya Sheria, Gazeti Rasmi, risiti, hotuba za bajeti na nyaraka zote za Serikali pamoja na kuuza vifaa vya kuandikia kwa Taasisi zote za Serikali na watu binafsi.  Vile vile, Idara ina jukumu kuu la kuchapisha na kuhifadhi nyaraka za siri za Serikali.
85.0   Mheshimiwa Spika, Kwa mwaka wa fedha 2013/2014 Baraza lako Tukufu liliidhinisha jumla ya Sh. 546,868,000 kwa Idara ya Upigaji Chapa na Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali. Hadi kufikia mwezi Machi, 2014 Idara iliingiziwa jumla ya Sh. 288,754,082 kwa kazi za kawaida ambazo ni sawa na asilimia 53. Aidha, Idara iliidhinishiwa jumla ya Sh. 2,500,000,000 kwa kazi za maendeleo ikiwa ni mchango wa SMZ na hadi kufikia mwezi Machi, 2014 Idara iliingiziwa jumla ya Sh. 2,050,000,000 sawa na asilimia 82.

86.0   Mheshimiwa Spika, Idara ilipangiwa kuchangia jumla ya Sh.500,000,000 kwa mwaka wa fedha 2013/2014 katika Mfuko Mkuu wa Serikali. Hadi kufikia tarehe 31 Machi, 2014, Idara imechangia Sh. 14,623,400 sawa na asilimia 4. Mchango huu mdogo umetokana na kiwanda kupunguza uzalishaji kutokana na kuharibika kwa mashine pamoja na kuanza kwa zoezi la kuhamisha mashine na kufunga mashine mpya. Aidha, Idara inazidai baadhi ya taasisi za Serikali jumla sh. 42,480,000 za mapato ambazo ni sehemu ya mapato yanayotarajiwa kukusanywa katika kipindi cha Julai 2013 - Machi 2014.

87.0   Mheshimiwa Spika, Idara kwa Mwaka wa Fedha 2013/2014 imeweza kutekeleza kazi zifuatazo:
                        i.         Jumla ya wafanyakazi saba (7) wamepatiwa mafunzo ya muda mrefu na mfupi katika ngazi za cheti, diploma na shahada ya pili.
                      ii.         Idara inaendelea kutoa huduma ya machapisho mbali mbali zikiwemo kazi za uchapishaji wa sheria, Gazeti Rasmi ya Serikali, Katiba, madaftari ya mishahara, kalenda, na kazi nyengine za taasisi za umma na binafsi.
                    iii.         Idara imekamilisha matengenezo ya jengo jipya la kiwanda cha uchapishaji huko Maruhubi na tayari jengo hilo limeanza kutumika.
                    iv.         Idara imechapisha miswada ya sheria 11 na matoleo 1,400 ya Gazeti Rasmi la Serikali.
                      v.         Idara imenunua pamoja na kufunga kwa awamu ya kwanza mashine mpya nne (4) za aina ya dijitali.

88.0   Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha wa 2014/2015, Idara ya Upigaji Chapa na Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali imejipangia malengo yafuatayo:-

                        i.         Kuweka mazingira mazuri ya kazi za Idara kwa ununuzi wa vifaa vya ofisi na samani.
                      ii.         Kuwajengea uwezo wafanyakazi watano (5) wa Idara kwa kutoa mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu pamoja na kulipa stahiki za likizo kwa wafanyakazi saba (7).
                    iii.         Kutoa huduma za Uchapishaji wa nyaraka na Sheria za Serikali
                    iv.         Kutangaza huduma za Kiwanda kwa ajili ya kuongeza idadi ya wateja na mapato.
                      v.         Kukamilisha utaratibu wa kuanzisha Bohari Kuu ya Serikali ya vifaa vya Ofisi.

89.0   Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2014/2015, Idara ya Upigaji Chapa na Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali imekadiriwa kutumia jumla ya Sh. 482,066,600. Kati ya hizo Sh. 347,066,600 kwa matumizi ya mishahara ya wafanyakazi, michango ya ZSSF na Sh. 135,000,000 kwa matumizi mengineyo.

90.0   Mheshimiwa Spika, kwa upande wa mapato Idara imepangiwa kukusanya Sh. 600,000,000 kwa mwaka wa fedha 2014/2015.
OFISI KUU PEMBA

91.0   Mheshimiwa Spika, Ofisi  ya Makamu wa  Pili wa  Rais  Pemba  ina jukumu la kusimamia utekelezaji wa kazi  za Ofisi ya Makamu wa Pili  wa Rais  kwa upande wa Pemba.

92.0   Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2013/2014 Baraza lako Tukufu liliidhinisha jumla ya Sh. 452,817,000 kwa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Pemba. Hadi kufikia mwezi Machi, 2014 Idara iliingiziwa jumla ya Sh. 254,014,050 kwa kazi za kawaida ambazo ni sawa na asilimia 56.

93.0   Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha  2013/2014 Ofisi Kuu Pemba ilikuwa na  lengo la kusimamia  shughuli  za Idara zilizo chini ya  Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Kisiwani Pemba na imetekeleza kazi zifuatazo:

                        i.         Ofisi iliratibu na kufuatilia utekelezaji wa ziara 23 za Viongozi Wakuu wa Kitaifa.
                      ii.         Ofisi ilifanya Semina ya siku moja (1) kwa Maafisa Mipango wa Mawizara, Mikoa na Wilaya juu ya uandishi wa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala. (CCM)
                    iii.         Ofisi iliratibu  na  ilisimamia utekelezaji wa  miradi ya TASAF Pemba
                    iv.         Ofisi iliendelea kutoa mafunzo, kusimamia na kuratibu shughuli za kukabiliana na Maafa.
                      v.         Ofisi iliwapatia mafunzo wafanyakazi wanane (8) katika  kada mbali mbali.

94.0   Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2014/2015 Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Pemba itatekeleza malengo ya idara na taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais.

95.0   Mhesimiwa spika, ili Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Pemba iweze kutekeleza malengo yake iliyopanga naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe jumla ya Sh. 388,964,000 kwa matumizi ya Ofisi. Kati ya hizo Sh. 241,266,000 ni kwa malipo ya mishahara na posho za wafanyakazi na mchango wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii, na  Sh. 147,698,000 ni kwa matumizi mengineyo.

TUME YA UCHAGUZI YA ZANZIBAR

96.0   Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2013/2014 Baraza lako tukufu liliidhinisha jumla ya. Sh. 987,000,000 kwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Hadi kufikia mwezi Machi, 2014 Tume iliingiziwa jumla ya Sh. 827,303,454 kwa kazi za kawaida ambazo ni sawa na asilimia 84. Aidha, Tume iliidhinishiwa Sh. 3,594,000,000 kutoka kwa Washirika wa Maendeleo na hadi kufikia mwezi Machi, 2014 Tume ya Uchaguzi iliingiziwa jumla ya Sh. 768,165,455 sawa na asilimia 21.

97.0   Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2013/2014 Tume ya Uchaguzi imetekeleza malengo yafuatayo:-
        i.   Katika mwaka wa Fedha wa 2013/2014, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar iliendesha chaguzi ndogo mbili. Chaguzi hizo ni Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Kiembesamaki Wilaya ya Magharibi kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Ndugu Mansour Yusuf Himid aliyekuwa mwakilishi wa Jimbo hilo na uchaguzi Mdogo wa Wadi ya Kiboje Wilaya ya Kati iliyoachwa wazi kufuatia kifo cha Diwani wa Wadi hiyo Ndugu Mayunga Maftah Mayunga. Chaguzi zote mbili ziliendeshwa kwa salama na utulivu mkubwa.

      ii.   Tume imetoa elimu ya Wapiga Kura kupitia vyombo mbali mbali vya habari vya Redio na Televisheni, semina za Wanafunzi wa Skuli za Sekondari na kupitia vikundi vya Sanaa za Maonesho kwa Unguja na Pemba. Aidha, imeendelea kutoa elimu ya uandikishaji wa Wapiga Kura katika Shehia mbalimbali ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

    iii.   Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imeanza maandalizi ya awali ya kuchunguza idadi, majina na mipaka ya majimbo ya Uchaguzi kwa kuwapatia Wajumbe wa Tume ya Uchaguzi na Watendaji wake mafunzo kuhusu uchunguzi wa majimbo.  Mafunzo hayo yamefanyika kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza iliwahusisha  Maafisa Uchaguzi wa Wilaya za Unguja na Pemba na awamu ya pili iliwahusisha  Wajumbe wa Tume  na Sekretarieti.

    iv.   Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imeendesha kazi za uandikishaji wa Wapiga Kura wapya na uendelezaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga kura. Kazi hiyo ilianza katika mwezi wa Juni 2013 Mkoa wa Kaskazini Unguja na ilimalizika katika mwezi wa Novemba 2013, Mkoa wa Kusini Pemba. Zoezi hilo lilifanyika kwa kuwaandikisha wananchi wote waliojitokeza ambao wana sifa za kupiga kura kwa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar.  Jumla la wananchi 41,261 waliandikishwa (Kiambatisho Nam 5).

     
98.0   Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha  2014/2015 Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar  imepanga kutekeleza malengo yafuatayo:-

                 i.     Kuweka mazingira mazuri ya kazi za Tume kwa ununuzi wa vifaa vya ofisi na samani.
               ii.     Kuwajengea uwezo wafanyakazi watatu (3) kwa kuwapatia mafunzo ya muda mrefu na wafanyakazi (15) mafunzo ya muda mfupi pamoja na kulipa stahiki za likizo kwa wafanyakazi sita (6).
             iii.     Kuendeleza Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
             iv.     Kufanya uchunguzi wa idadi, majina na mipaka kwa majimbo yote 50 ya uchaguzi.
               v.     Kusimamia na kuendesha kura ya Maoni ya kuthibitisha Katiba iliyopendekezwa.
             vi.     Kufanya matayarisho ya jumla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

99.0   Mheshimiwa Spika, ili Tume ya Uchaguzi iweze kutekeleza majukumu yake kwa mwaka wa fedha 2014/2015, naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe jumla ya Sh.  1,314,100,000 kwa matumizi ya kawaida. Kati ya hizo Sh. 971,500,000  ni kwa  malipo  ya mishahara, posho na stahiki za wafanyakazi na Sh. 342,600,000  kwa matumizi mengineyo. Aidha, naliomba Baraza lako Tukufu kuidhinisha jumla ya Sh. 1,750,000,000 kwa ajili ya utekelezaji wa kazi za maendeleo kupitia mchango wa Washirika wa Maendeleo.

100.0  Mheshimiwa Spika, Tume ya Uchaguzi kupitia Mfuko Mkuu wa Serikali imepangiwa kutumia jumla ya Sh. 3,000,000,000 kwa ajili ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, kufanya uchunguzi wa idadi, majina na mipaka ya majimbo ya uchaguzi pamoja na kuendeleza Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

BARAZA LA WAWAKILISHI

101.0  Mheshimiwa Spika, Baraza la Wawakilishi Zanzibar limeundwa chini ya Kifungu cha 63 cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na majukumu ya msingi yanatajwa kwenye Kifungu cha 88 cha Katiba ambayo ni kama yafuatayo:-
             i.     Kutunga Sheria pale ambapo utekelezaji wa jambo unahitaji kuwepo kwa sheria hiyo.
           ii.     Kujadili shughuli za kila Wizara wakati wa kikao cha mwaka wa Bajeti katika Baraza la Wawakilishi.
         iii.     Kuuliza maswali mbalimbali kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika Baraza la Wawakililshi.
         iv.     Kuidhinisha na kusimamia Mipango ya Maendeleo ya Serikali katika njia ile ile ambayo Bajeti ya mwaka inaidhinishwa.

102.0  Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza majukumu hayo kwa mwaka wa fedha wa 2013/2014 Ofisi ya Baraza la Wawakilishi iliidhinishiwa jumla ya Sh. 14,852,000,000. Hadi kufikia mwezi wa Machi 2014 Baraza limeingiziwa Sh. 10,501,979,561 kwa kazi za kawaida sawa na asilimia 71.  Kwa upande wa fedha za Miradi ya Maendeleo Baraza la Wawakilishi liliidhinishiwa jumla ya Sh. 697,536,000 na hadi kufikia mwezi Machi 2014 Baraza limeiingiziwa Sh. 544,658,000 Sawa na asilimia 78.

103.0  Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2013/2014 Baraza la Wawakilishi limetekeleza kazi zifuatazo:-
        i.   Baraza limefanya Mikutano minne ya kawaida ambapo kwenye Mikutano hiyo jumla ya Miswada kumi (10) ya Sheria ilijadiliwa na kupitishwa na maswali 250 yameulizwa na kujibiwa. Mgawanyo wa Miswada na Maswali hayo ni  kama ifuatavyo:-

§  Mkutano wa Kumi na mbili wa Bajeti ya mwaka wa fedha wa 2013/2014 ulikuwa na Miswada miwili ya Sheria na jumla ya Maswali 75 ya msingi yaliulizwa na kujibiwa.
§  Mkutano wa Kumi na Tatu uliofanyika mwezi wa Oktoba, 2013 ulipitisha Miswada minne ya Sheria na jumla ya maswali 71 ya msingi yaliulizwa na kupatiwa majibu.
§  Mkutano wa Kumi na Nne uliofanyika mwezi wa Disemba 2013 ulipitisha Miswada Mitatu ya Sheria wakati jumla ya maswali 61 ya msingi yaliulizwa na kujibiwa. Aidha, kwenye Mkutano huo Baraza lilipokea na kuijadili Ripoti ya Kamati Teule ya Kuchunguza Migogoro ya Ardhi. Pia, kulikuwa na Hoja mbili za Wajumbe. Moja ni Hoja ya Mjumbe kuomba Ridhaa ya Baraza kwa ajili ya kuwasilisha Mswada wa Sheria ya Utawala wa Baraza, iliyowasilishwa na Mhe. Hamza Hassan Juma na Pili ni Hoja ya Mjumbe ya kuliomba Baraza kutoa Azimio Dhidi ya Vitendo vya Udhalilishaji wa Watoto, Zanzibar. Hoja ambayo iliwasilishwa kwenye Baraza na Mhe. Mgeni Hassan Juma
§  Mkutano wa Kumi na Tano uliofanyika mwezi wa Februari, 2014 nao ulipitisha Miswada miwili ya Sheria na jumla ya maswali 50 yaliulizwa na kujibiwa. Wakati huohuo, Baraza lilipokea Taarifa za Utekelezaji wa Maagizo ya Kamati za Baraza yaliyotolewa mwaka 2012/2013 na Kamati za Kudumu za Baraza ziliwasilisha Ripoti za Kazi kwa mwaka 2013/2014. Katika Mkutano huo pamoja na mambo mengine yaliyojadiliwa na kufikiwa maamuzi, Baraza liliunda Kamati Teule ya Kuchunguza Upotevu wa Nyaraka za Serikali katika Jengo la Nyaraka na Makumbusho. Kamati hiyo iliundwa ikiwa na Wajumbe watano. Hili liliibuka wakati wa kuwasilisha Ripoti za Kamati na lilitokana na Ripoti ya Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala. (Kiambatanisho Nam. 6)
      ii.   Kamati za Kudumu za Baraza zilifanya kazi zake za Kawaida za kufuatilia utekelezaji wa majukumu ya Serikali kupitia Wizara na Idara mbali mbali za Serikali. Aidha, Kamati Teule ya Baraza iliyopewa kazi ya kuchunguza Migogoro ya Ardhi nayo ilimaliza kazi yake na kuwasilisha Ripoti yake kwenye Baraza.
    iii.   Ofisi imewapatia mafunzo Wafanyakazi 16 katika fani za Sheria, Uchumi, Uhusiano wa Kimataifa, Utawala wa Biashara, Utawala wa Raslimali Watu, Ufundi, Teknolojia, Ununuzi na Ugavi, Ukutubi na Elimu, hii ni kwenye ngazi za Vyeti, Stashahada, Shahada, Shahada ya Uzamili na Shahada ya Uzamivu.
    iv.   Baraza limeshiriki katika Mkutano wa Jumuiya ya Makatibu Mezani (SOCAT) Dar-es-Salaam kwa lengo la  kuendeleza uhusiano wa Kimataifa wa kikanda baina ya Baraza na vyombo vyengine vya Kutunga Sheria na Umoja wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola.
      v.   Ofisi ya Baraza la Wawakilishi bado inaendeleza vipindi vyake vya kutoa elimu kwa Umma kupitia Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC) kwa upande wa Redio na Televisheni. Kwa kipindi cha mwaka 2013/2014 jumla ya vipindi 24 vya LIJUE BARAZA LA WAWAKILISHI vilirushwa hewani.
    vi.   Ofisi imefanya matengenezo makubwa ya majengo kwa Ofisi za Baraza Unguja na Pemba hasa yanayohusu miundo mbinu ya maji, tatizo ambalo sasa limepungua kwa kiasi kikubwa. Aidha, katika kupunguza matumizi ya umeme hasa kwa kuendesha vipoza hewa muda wote, mfumo wa muundo wa madirisha nao umeanza kubadilishwa ambapo badala ya kuwa na madirisha yasiyofunguka sasa yamewekwa yale yanayofunguka.
  vii.   Ofisi imefanya tathmini ya athari zinazotokana na nyufa ili kuweza kutafuta ufumbuzi wa kuziba nyufa hizo.  

104.0  Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2014/2015 Baraza la Wawakilishi limepanga kutekeleza malengo yafuatayo:-
                 i.  Kujenga Mazingira mazuri kwa kuwezesha kufanyika kwa Mikutano  minne (4) ya Baraza la Wawakilishi pamoja na kazi za Kamati katika kufuatilia Shughuli za Serikali na Kusimamia uwajibikaji wake
               ii.  Kutoa mafunzo ya kuongeza uwezo wa kitaalamu kwa Wajumbe na Wafanyakazi wa Baraza
             iii.  Kuweka  majengo yote ya Ofisi katika hali nzuri
             iv.  Kutoa taaluma kwa wananchi kuhusu utendaji wa Shughuli za Baraza kupitia vyombo vya Habari
               v.  Kuimarisha mahusiano kati ya Baraza na Mabunge mengine ya Umoja wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola.

105.0    Mheshimiwa Spika, ili Ofisi ya Baraza la Wawakilishi iweze kutekeleza malengo yake kwa mwaka wa fedha 2014/2015, naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe jumla ya Sh. 14,564,000,000 kwa matumizi ya Ofisi. Kati ya hizo Sh. 7,664,000,000 ni kwa malipo ya mishahara, posho za wafanyakazi, Stahiki nyengine na mchango wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii na jumla ya Sh. 6,900,000,000 kwa matumizi mengineyo. Kwa upande wa fedha za maendeleo naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe jumla ya Sh. 710, 615,000 ikiwa ni mchango wa Washirika wa Maendeleo.
UKUSANYAJI MAPATO

106.0    Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2013/2014, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais ilipanga kukusanya mapato ya jumla ya Sh. 544,400,000 kwa mchanganuo ufuatao:-
             i.  Idara ya Upigaji Chapa na Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali                   
                                                          Sh. 500,000,000
           ii.           Idara ya Uendeshaji na Utumishi
(Kodi ya Ukumbi wa Mikutano wa BLW wa zamani)    
   Sh.  38,000,000
         iii.           Idara ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa
(Kodi ya milango ya duka na mashamiana)     
      Sh.  6,000,000
  Jumla                                                     Sh. 544,000,000

107.0    Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Machi 2014 ukusanyaji halisi wa mapato ulikua ni jumla ya Sh. 16,519,200 Sawa na asilimia 4  kama ifuatavyo:-
    i.  Idara ya Upigaji Chapa na Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali 
             Sh. 14,899,200
  ii.  Idara ya Uendeshaji na Utumishi
(Kodi ya Ukumbi wa Mikutano wa BLW wa zamani)       __               
iii.  Idara ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa
(Kodi ya Milango ya duka na mashamiana)    
                                                                                  Sh.   1,620,000
       Jumla                                      Sh. 16,519,200

108.0    Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2014/2015, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais imepanga kukusanya mapato ya jumla ya Sh. 608,000,000 kwa mchanganuo ufuatao:-

  i.         Idara ya Upigaji Chapa na Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali
Sh. 600,000,000
ii.         Idara ya Uendeshaji na Utumishi
(Kodi ya Ukumbi wa Mikutano wa BLW wa zamani)        
Sh.     5,000,000
iii.         Idara ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa
          (Kodi ya mashamiana)                               Sh.    3,000,000
                Jumla                                           Sh. 608,000,000

109.0    Mheshimiwa Spika, muhtasari wa makadirio ya fedha kwa kazi za kawaida na za Maendeleo kwa mwaka wa fedha 2014/2015 ni kama unavyoonekana katika (Kiambatanisho Nam. 7A na 7B).HITIMISHO

110.0    Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii kumshukuru kwa dhati Mheshimiwa Mohamed Aboud Mohamed, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais kwa kunisaidia kutekeleza majukumu ya Ofisi yangu kwa ufanisi mkubwa. Aidha, nawashukuru kwa dhati watendaji wote wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wakiongozwa na Katibu Mkuu, Dkt. Khalid Salum Mohamed kwa juhudi zao katika kutekeleza majukumu yao.

111.0    Mheshimiwa Spika, natoa shukrani zangu za dhati kwa Wajumbe wote wa Baraza la Wawakilishi na shukurani za pekee kwa Mwenyekiti na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa kwa mashirikiano, maelekezo, ushauri na michango wanayotupa ambayo ilisaidia katika  utayarishaji wa hotuba hii. Aidha, napenda kuwashukuru sana Washirika wa Maendeleo (Development Partners) na nchi marafiki ambazo zinaendelea kuchangia katika kufanikisha utekelezaji wa malengo ya Ofisi yetu na ya nchi kwa jumla katika mwaka wa fedha 2013/2014. Miongoni mwao ni: AL-Yousef Foundation, Benki ya Dunia, Clinton Foundation, China, FAO, Finland, Norway, Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, India, Japan, Marekani, Mfuko wa Dunia wa Kupambana na Kifua Kikuu, Malaria na UKIMWI (Global Fund), Oman, UNAIDS, USAID, UNDP, UNICEF, UNFPA, WHO, WFP na WIPO. Vile vile, naishukuru sana Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa ushirikiano wao wa karibu sana na Ofisi yetu.  Pia nazishukuru Taasisi zisizo za Kiserikali kama ZAYEDESA, Jumuiya ya Wafanya Biashara, Wenye Viwanda na Wakulima kwa kuendelea kuisaidia Serikali katika kutoa huduma za jamii na kuiletea maendeleo nchi yetu. Pia, nawashukuru wananchi wote ambao wamefuatilia na kusikiliza Hotuba yetu hii.

112.0    Mheshimiwa Spika, Baada ya maelezo hayo, sasa  naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe Jumla ya Sh. 19,988,300,000 kwa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais na Taasisi zake (Tume ya Uchaguzi na Baraza la Wawakilishi) kwa matumizi ya kazi za kawaida na Sh. 6,343,495,000 kwa kazi za maendeleo (Kiambatanisho Nam. 7A na 7B). Mchanganuo halisi wa fedha hizo ni kama ifuatavyo:-


Kazi za Kawaida                                                  
i
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais
Sh.   4,110,200,000
ii
Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar
Sh.   1,314,100,000
iii
Ofisi ya Baraza la Wawakilishi
Sh. 14,564,000,000

Jumla Kuu
Sh. 19,988,300,000

Kazi za Maendeleo
i
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais
a
Kujenga Uwezo wa Kukabiliana na Maafa

Sh.  1,322,880,000
b
Mradi wa TASAF III
Sh.  1,550,000,000
c
Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo (CDF)

Sh.  1,010,000,000

Jumla Ndogo (OMPR)
Sh. 3,882,880,000

ii
Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar

Mradi wa kuwezesha Demokrasia (DEP)

Sh. 1,750,000,000

iii
Ofisi ya Baraza la Wawakilishi

Mradi wa Kuwezesha BLW (LSP)

Sh.  710,615,000

Jumla Kuu (Miradi)
Sh.  6,343,495,000


113.0    Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja,


MHE. BALOZI SEIF ALI IDDI
MAKAMU WA PILI WA RAIS,
OFISI YA MAKAMU WA PILI WA RAIS,
ZANZIBAR.

No comments: