VURUGU ZAFUMUKA KAMBI YA UJENZI SUMBAWANGA

Polisi mjini hapa wamelazimika kutumia risasi za moto kutawanya wafanyakazi wa Kampuni  ya Aaarsleef /Bam International inayojenga  kwa kiwango  cha lami kipande cha barabara  cha Laela - Sumbawanga waliofunga barabara eneo la Kianda.
Wafanyakazi hao walifunga barabara wakipinga kitendo cha walinzi wa kampuni hiyo kumzuia mwenzao mmoja wakimtuhumu kutaka kuiba mafuta.
Kwa mujibu  wa  mashuhuda wa  mkasa huo  wafanyakazi hao wa kambi ya ujenzi ya  Kianda  wilayani  Sumbawanga walileta usumbufu mkubwa wakipinga walinzi  wa  kampuni hiyo  kumkamata  opereta  wa tingatinga, aitwaye Gabriel Daniel (34) mkazi wa eneo la Bomani , Manispaa  ya Sumbawanga.
Kufuatia  dhahama hiyo  wafanyakazi  hao  wenye  hasira  waliteketeza kwa moto magari  makubwa  manne. Magari hayo ni pamoja  na Scania  Tipper lenye namba  za usajili T 755 CAV, Iveco lenye  namba  za usajili T 116 AYT , gari aina ya Artego  lenye nambari  za usajili T 839 na gari aina  ya Artois  yenye namba za usajili T 936.
Watu wawili wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kuhusika na tukio hilo.Watuhumiwa hao ni Emanuel Sanga (34)  mkazi  wa  Mkoa wa Iringa  na Ngasa Mathias (40) mkazi wa wilayani Chunya, Mbeya.

No comments: