NIMR KUTENGENEZA DAWA KWA TEKNOLOJIA YA CHEMBEHAI

Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), imesema inatarajia kuanza kutengeneza dawa za binadamu zitokanazo na mimea kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya kutumia chembe hai ya mimea bila kukata mti husika.
Hayo yamebainishwa wakati wa kutiliana saini ya mkataba wa maridhiano kati ya NIMR na Kampuni ya UNHWA ya Jamhuri ya Watu wa Korea Kusini iliyofanyika jana jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa NIMR, Mwele Malecela alisema  utekelezaji wa makubaliano hayo utaifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza kutumia teknolojia hiyo.
"Kwa sasa hali ya kiwanda chetu kwa upande wa vifaa haijakaa sawa, hivyo tutachukua hatua katika kuhakikisha tunahamishia teknolojia hiyo hapa nchini," alisema.
Alisema kwa sasa, taasisi yake itakuwa ikifanyia majaribio dawa zinazotengenezwa na kampuni hiyo kwa kuyapa kipaumbele magonjwa ya Ukimwi na saratani.
"Juzi wenzetu hawa walitembelea kiwanda chetu cha Mabibo na maabara na wametupa moyo kuwa pamoja na kuwa ndio tunaanza tunaweza kufika mbali katika kutengeneza dawa za binadamu kwa kutumia mimea.
Aidha, Malecela alimshukuru Rais Jakaya Kikwete kwa kufuatilia na kuunga mkono juhudi za utafiti. Alisema teknolojia hiyo itasaidia Watanzania kupata dawa bora na nzuri kwa kutumia mimea.
Mkurugenzi wa UNHWA, Youngwoo Jin alisema, "Kwa ushirikiano wetu tunaweza kupiga hatua katika hili."

No comments: