TUCTA KUPIGANIA 'PAYE' ISHUKE KUTOKA ASILIMIA 13 HADI 9

Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), limeazimia kuendelea kupigania kushushwa kwa Kodi ya Mshahara (PAYE) kutoka asilimia 13 inayokatwa hivi sasa hadi asilimia tisa, ili   mfanyakazi apate ahueni ya maisha.
Katibu Mkuu wa Tucta, Nicholas Mgaya, alisema hayo jana Dar es Salaam wakati akizungumzia maadhimisho ya Mei Mosi  yatakayoambatana na wiki ya wafanyakazi itakayoanza rasmi leo.
Maadhimisho ya Mei Mosi yatafanyika nchini kesho kutwa ambapo kitaifa yatafanyikia jijini Dar es Salaam na mgeni rasmi atakuwa Rais Jakaya Kikwete.
Mgaya alisema mbali na kupunguzwa kwa kodi, Tucta inayo mambo mengine mawili inayopanga kupigania ili ujumbe ufike serikalini na kupatiwa suluhu.
Suala la pili alitaja kuwa ni kila mfanyakazi kupatiwa malipo mazuri awapo kazini, jambo alilosema wamekuwa wakiliomba mara kwa mara na hadi sasa halijakamilika.
“Kila mfanyakazi ni mstaafu mtarajiwa, hivyo ni vyema waajiri waandaliwe malipo mazuri, ili mfanyakazi atakapostaafu awe na kiwango cha maisha kitakachomsaidia katika maisha yake,” alisema Mgaya.
Pia wamejipanga kupigania mifuko ya pensheni, ilipe kiwango sawa cha kiinua mgongo tofauti na sasa ambapo baadhi ya mifuko inalipa kiwango kidogo na mingine inalipa kiwango kikubwa.
 “Ifikie wakati sasa kusiwepo na utitiri wa mifuko, bali ivunjwe na kubaki miwili yaani wa binafsi na wa umma ambayo mengine yanabakia yakijitangaza tu,” alisema Mgaya.
Mgaya alilitaja jambo lingine kuwa ni fidia kwa wafanyakazi ambapo alishauri kuundwe kwa mfuko ambao utawezesha mfanyakazi atakayeumia kazini, kulipwa fidia ambayo  itamsaidia.
Kuhusu mabadiliko ambayo yametokea tangu maadhimisho yaliyopita ya Mei Mosi, Mgaya alisema ni kupungua kwa kodi kutoka asilima 14 kwenda 13 ambayo alisisitiza kwamba  wafanyakazi wanaomba sasa ifikie asilimia tisa.
Mwandishi alimtafuta Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudentia Kabaka na Naibu wake, Makongoro Mahanga, wazungumzie mpango huo wa Tucta, lakini simu zao ziliita bila majibu.

No comments: