MARAIS EAC WAKUTANA KUANGALIA ITIFAKI YA SOKO LA PAMOJA

Marais wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wanafanya mkutano maalumu kesho mjini hapa kutathmini shughuli za jumuiya, ikiwemo kupitia maombi ya Sudan Kusini na Somalia kujiunga.
Katika mkutano huo wa siku moja, miongoni mwa mambo yatakayopewa kipaumbele ni pamoja na kutathmini hatua iliyofikiwa kuhusu utekelezaji wa Itifaki ya Soko la Pamoja lililoanza rasmi Novemba 2009.
Itifaki ya Soko la Pamoja inaruhusu uhuru wa bidhaa, watu, ajira, huduma pamoja na mitaji kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine ama kuishi au kufanya shughuli pasipo vikwazo.
Soko la Pamoja ni hatua ya pili katika ushirikiano wa kiuchumi ndani ya EAC, ikiwa imetanguliwa na Umoja wa Forodha uliotiwa saini 2005.
Hatua ya tatu ni Umoja wa Fedha uliotiwa saini Kampala, Uganda, Novemba, mwaka jana.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Sekretarieti ya EAC, marais hao  watapokea marekebisho ya muundo wa kufikia hatua ya Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki, hatua ambayo ni ya mwisho katika lengo kuu la mtangamano wa EAC.
Mkutano huo pia utapitia maombi ya nchi za Sudan Kusini na Somalia kujiunga na EAC.

No comments: