TMA: MSIDHARAU TAARIFA ZA UTABIRI WA HALI YA HEWA

Watanzania wametakiwa kutodharau tafiti na taarifa, zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), kwani mabadiliko ya mara kwa mara ya hali ya hewa yanayotokea yanaweza kuleta madhara.
Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk  Agnes Kijazi alipokuwa akizungumzia mafanikio ya mamlaka yake katika miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, wakati wa maonesho ya Muungano kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam.
Alisema mvua za msimu zinazonyesha sasa zinahitaji taarifa za mara kwa mara ili kujitahadharisha na majanga kama mafuriko yanayotokea kutokana na kudharau taarifa hizo.
Alisema wanategemea kwamba,  mvua hizo zitanyesha hadi mwezi Juni ambapo zitakuwa za kipindi na hivyo Watanzania wahamie maeneo yaliyosalama kuepusha majanga hayo.
"Tunatoa taarifa kutokana na mabadiliko yanayotokea, endapo muelekeo wa mvua hizi zitabadilika basi tunatoa taarifa kwa vyombo vya habari kama mvua hizo zitakuwa na ukubwa gani ili kujiandaa," alisema Kijazi.
Aidha, alisema hadi kufikia miaka 50 ya Muungano, wamefanikiwa kuwa na mitambo ya kisasa ambayo inaunganisha nchi zote za Muungano na kutoa taarifa iliyosahihi.
Alisema huduma za kiutabiri zimeboreshwa kwa asilimia 80 sambamba na kutoa taarifa juu ya mvua kubwa, upepo mkali na ukubwa wa mawimbi baharini.
Aliongeza kuwa Zanzibar imepewa cheti cha kutambua mchango wa mamlaka kwa huduma za baharini na maafa.
"Tumefanikiwa kufanikisha ubora wa anga kufikia kiwango cha kimataifa na Zanzibar ni mojawapo ya kituo kilichokidhi viwango hivyo na tumefungua kituo cha hali ya hewa katika bandari ya Zanzibar" aliongeza.
Pia alisema wamefanikiwa kuongeza wafanyakazi 574 kati yao wanasayansi 435 na kada ya wahudumu wasaidizi 139.
Alisema wameanzisha vyuo vya Hali ya Hewa Kigoma na Dar es Salaam, pia wameboresha mifumo ya usambazaji wa taarifa hizo.
"Muungano umefanikisha mambo ambayo yangeweza kuleta shida hapo baadaye na hivyo kwa kushirikiana na Zanzibar tunatoa taarifa zilizosahihi na kutoa tahadhari kwa watumiaji wa bahari zote," alisema Kijazi.

No comments: