WIMBI LA WAVUVI KUUAWA ZIWANI LATIKISA SENGEREMA

Kumekuwepo na wimbi la wavuvi kuvamiwa, kunyang'anywa  mali zao na kuuawa na wahalifu katika Ziwa Victoria wilayani Sengerema.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo, amesema hali hiyo inatishia usalama.
Alibainisha  hayo mwishoni mwa wiki kwenye mkutano wa hadhara, uliofanyika katika kijiji cha Buyagu wilayani Sengerema katika ziara yake ya kutembelea Miradi ya Uhifadhi wa Mazingira (LVEMP II).
Aliwataka wananchi kuimarisha ulinzi kwenye maeneo yao kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, kutokana na wavuvi kuvamiwa na kuporwa mali zao, ikiwemo mitumbwi na injini.
"Watu hawa wamekuwa wakipita na kuishi kwenye maeneo yetu, hivyo suala la ulinzi ni letu sote kwa kuwabaini wahalifu na kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ili wachukuliwe hatua za kisheria," alisema.
Ndikilo alisema wageni wanaopita vijijini  na kutiliwa shaka, taarifa zao lazima ziripotiwe mapema ili kuhakikisha jamii inalindwa na kuwa salama wakati wote.
"Nawaonya wote wanaodhani kuwa Ziwa Victoria eneo la Sengerema ni la kufanyia uhalifu, Jeshi la Polisi limejipanga vizuri kuhakikisha ulinzi na usalama katika maeneo ya ziwa," alisema.
Alisema wahalifu wanaotaka kuifanya Sengerema kuwa shamba la bibi, hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
Alisema Tanzania ni nchi ya amani na utulivu na yenye upendo kwa watu wake. Lakini, alisema wapo watu wachache, wanaotaka kuvuruga Tanzania kwa sabau zao binafsi.
Ndikilo alisema kwa kuwa Jeshi la Polisi mkoani lina boti mbili ziendazo kasi, atazungumza nao ili wasaidie kuweka  ulinzi katika eneo la Nyakalilo Wilaya ya Sengerema, ambako matukio ya uvamizi  yamekuwa yakitokea mara kwa mara.
Akiwa katika kijiji cha Buyagu, Mkuu wa Mkoa aliongoza zoezi la kuteketeza magugu maji yaliyoopolewa ziwani na kikundi cha kudhibiti magugu maji kilichoanzishwa Oktoba mwaka  2012. Hadi sasa  kikundi hicho kimeopoa tani 19 za magugu maji na kuziteketeza.
Awali, Katibu wa kikundi hicho, Revocatus  Nkilijiwa alisema kikundi hicho kilinunua boti na injini yake kusaidia doria kupunguza uvuvi haramu na kusaidia uvuvi na usafirishaji.

No comments: