JAMII YATAKIWA KUPUNGUZA MATUMIZI YA DAWA ZA KULEVYA

Jamii imetakiwa kupambana na kupunguza matumizi ya  dawa za kulevya, ambazo zimekuwa zikiathiri nguvu kazi kwa vijana.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, wakati akizungumza na watendaji wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Ikulu, wakati akipokea mpango wa kazi wa robo Bajeti mwaka 2013-2014.
Alisema njia pekee ya kupambana na kupunguza matumizi ya  dawa za kulevya, ni jamii yenyewe kuhusishwa moja kwa moja ikiwemo kuanzisha nyumba zitakazotoa ushauri nasaha na kuachana na matumizi ya dawa za kulevya.
“Naiomba jamii kujitokeza kwa wingi kushiriki moja kwa moja katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa vijana wetu ambao wameathirika vibaya,” alisema.
Alipongeza watu waliojitolea kuanzisha nyumba zinazotoa ushauri nasaha kwa vijana na kuachana na matumizi ya dawa za kulevya na kurekebisha tabia zao Unguja na Pemba.
Alisema mchango wa nyumba hizo ni mkubwa na mabadiliko makubwa yamejitokeza kwa vijana waliokuwa wakitumia dawa za kulevya na kuacha moja kwa moja.
“Nimefurahishwa na mchango wa jamii kuanzisha nyumba za ushauri nasaha kwa vijana kuachana na matumizi ya dawa za kulevya, ambapo faida zake tumeziona moja kwa moja kwa sasa,” alisema.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Fatma Alhabib Fereji, alisema Wizara inaendelea na juhudi za kukabiliana na hatari ya matumizi ya dawa za kulevya kwa jamii.
Alizitaja juhudi hizo ikiwemo matayarisho ya Kanuni ya Sheria ya Dawa za Kulevya, ambayo kwa kiasi kikubwa itasaidia kudhibiti tatizo hilo kwa vitendo.
“Tupo katika mchakato wa kutayarisha Kanuni za kupambana na  dawa za kulevya ambazo kasi yake ni kubwa pamoja na matumizi yake kwa ujumla zaidi kwa vijana,” alisema.
Aidha alisema Wizara ipo katika hatua za kutayarisha muongozo kwa matumizi ya nyumba za kurekebisha tabia na kuachana na matumizi ya dawa za kulevya maarufu kwa jina la Sober house  ambazo tangu kuanzishwa kwake zimeleta mabadiliko makubwa.
Alisema kuwepo kwa kanuni na muongozo wa nyumba hizo kwa kiasi kikubwa kutasaidia kuhakikisha tatizo la matumizi ya dawa za kulevya linapungua na nyumba hizo kuwepo kwa mujibu wa sheria.
'Serikali inaridhishwa sana na kuwepo kwa nyumba za kurekebisha tabia kwa vijana kuachana na matumizi ya dawa za kulevya maarufu sober ambazo zimesaidia vijana wengi kuacha matumizi ya dawa za kulevya' alisema Fereji.
Hata hivyo, Fereji alikiri kuwepo kwa changamoto ya bandari ambazo sio rasmi kwa kiasi kikubwa ni chanzo cha uingizaji wa dawa za kulevya Zanzibar.
'Zanzibar hivi sasa zipo bandari bubu nyingi ambazo zinatumiwa kwa njia moja au  nyingine kuingiza dawa za kulevya na kusababisha taifa kuangamia' alisema Fereji.

No comments: