RAIS KIKWETE ATUMA RAMBIRAMBI AJALI YA BASI SINGIDA

Rais Jakaya Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Singida, Parseko Kone kutokana na vifo vya watu 19, wakiwemo polisi wanne na viongozi watatu wa Kijiji.
Watu hao walikufa katika ajali ya barabarani, iliyosababishwa na basi la Kampuni ya Sumry,  lenye Nambari ya Usajili T. 799 BTE, lililokuwa likitoka Kigoma kwenda Dar es Salaam.
Ajali hiyo ilitokea usiku wa kuamkia juzi katika Kijiji cha Utaho Wilaya ya Ikungi mkoani Singida baada ya kuwagonga watu  hao, waliokusanyika katika eneo,  ambako ajali nyingine ilikuwa imetokea.
Polisi waliopoteza maisha katika ajali hiyo, walikuwa wanatoa msaada katika ajali nyingine, iliyotokea katika eneo hilo, ambapo mwendesha baiskeli aligongwa na lori na kufariki papo hapo.
Kwa mujibu wa Taarifa ya Ikulu, iliyotolewa jana, Rais alisema: “Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za vifo vya watu 19 wakiwemo askari Polisi wanne na Viongozi watatu wa Kijiji cha Utaho katika Wilaya ya Ikungi mkoani Singida.  Vifo hivi vimetupotezea kama Taifa nguvu kazi muhimu kwa ujenzi wa nchi yetu na hakika vimeacha simanzi na huzuni kubwa kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu”.
Rais Kikwete alimuomba  Kone, kumfikishia salamu zake za rambirambi na pole nyingi kwa watu wote, waliopotelewa na ndugu na jamaa zao, kutokana na ajali hiyo.
Aliwahakikishia wafiwa kuwa yuko pamoja nao katika kuomboleza msiba huo mkubwa.
“Ninamuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema awawezeshe kupona haraka na kurejea katika hali zao za kawaida watu wote waliojeruhiwa katika ajali hiyo ili waweze kupona haraka na kuungana tena na ndugu na jamaa zao”, alisema Rais Kikwete.

No comments: