HALMASHAURI TARIME YATUMIA SHILINGI BILIONI 3.2

Halmashauri ya Mji wa Tarime mkoani Mara imekusanya na kutumia Sh bilioni 3.274 katika robo mwaka hadi Machi mwaka huu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji, Venance Mwamo alitoa taarifa hiyo ya makusanyo na matumizi katika kikao cha Baraza la Madiwani, kilichofanyika mjini hapa hivi karibuni.
Katika kikao hicho, Diwani wa  Kata ya Sabasaba, Christopher Chomete alitakiwa kuomba radhi baada ya kudaiwa kusoma taarifa za nyaraka za uongo.
 Diwani wa Viti Maalumu, Salma  Abubakar  ndiye aliyemshutumu kusoma taarifa alizodai ni za halmashauri mama ya wilaya ya Tarime, zikituhumu viongozi.
Kwa mujibu wa diwani huyo wa viti maalumu, alishutumu viongozi wa halmashauri hiyo ya mji, akiwemo mkurugenzi wake  kwa ubadhirifu wa fedha. 
Salma ambaye alikuwa ameketi karibu naye, alisema diwani huyo anatumia nyaraka za uongo kuvuruga madiwani wa halmashauri ya mji na kuleta uchochezi.
Mwenyekiti wa Baraza, Daud Wangwe alimwagiza Diwani Chomete kuomba radhi kwa kusoma taarifa za uongo na kushutumu viongozi wa halmashauri hiyo kwa ubadhirifu, huku akijua kuwa taarifa anazosoma si za kweli.
“Kitendo cha diwani mwenzetu Chomete cha kutusomea taarifa za uongo katika kikao hiki na kuanza kushutumu viongozi wa halmashauri bila ya kuwa na uhakika na taarifa zake ni cha kudhalilisha baraza letu hata hawa wananchi walikuja hapa kutusikiliza wanatushangaa kwa kusema uongo ndani ya kikao," alisema Salma.
Katika kikao hicho, Mkuu wa wilaya hiyo  John Henjewele aliagiza viongozi wa halmashauri kuhakikisha wanakamilisha haraka ukarabati wa chumba cha X-Ray.
Mashine ya X ray ilitolewa mwaka jana na Kampuni ya North Mara Barrick kwa Hospitali ya Wilaya hiyo, lakini hadi sasa haijafungwa.

No comments: