NAMIBIA WATAKA KUJENGA MNARA WA KIKWETE KONGWA

Rais mstaafu wa Namibia, Sam Nujoma amemwambia Rais Jakaya Kikwete kuwa sherehe za Muungano zimethibitisha Tanzania inao uwezo wa kutosha wa kijeshi wa kukabili shambulio lolote kwa Afrika kutoka nje ya bara.
Nujoma, ambaye alieleza furaha yake ya kurejea nchini ambako aliishi wakati wa kutafuta uhuru wa Namibia, alisema hayo katika mkutano wake na Rais Kikwete.
“Maonesho yale ya kijeshi yamethibitisha kuwa Tanzania inao uwezo wa kukabiliana na kuzuia shambulio lolote dhidi ya Bara la Afrika ambalo linapitia upande huu wa Bahari ya Hindi – mnalo jeshi lenye nguvu ya maji, jeshi lenye nguvu la anga na jeshi lenye nguvu la nchi kavu,” alisema Nujoma.
Katika mazungumzo, Nujoma alimweleza Kikwete wazo la Serikali ya Namibia na chama tawala cha nchi hiyo cha SWAPO la kutaka kujenga mnara na sanamu ya heshima ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Wanataka kuuweka Kongwa, Mkoa wa Dodoma, ambako SWAPO walianzia maisha yao katika Tanzania wakati wanaendesha vita ya ukombozi dhidi ya makaburu.
Kiongozi huyo mstaafu alikuwa miongoni mwa viongozi na wajumbe maalumu waliowakilisha nchi zao katika sherehe za miaka 50 ya Muungano ambao juzi Rais Jakaya Kikwete alikamilisha saa 24 za mikutano mfululizo nao juzi.
Wengine aliokutana nao kwa nyakati tofauti ni  Rais mstaafu wa Zambia, Rupiah Banda, Makamu Mwenyekiti wa Bunge la China, Chen Changzhi, Waziri wa Habari na Mawasiliano wa Algeria, Abdulkadir Messahel na Waziri wa Serikali za Mitaa wa Angola,  Bernito de George Beltazar.
Alikutana pia na Waziri wa Mambo ya Ndani na Wanyamapori wa Sudan Kusini, Aley Anjieng Aleu na Makamu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Geraldine Fraser - Moleketi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Ikulu, Rais Kikwete alikamilisha mikutano hiyo kwa kukutana na kufanya mazungumzo na Rais mstaafu wa Zambia, Banda, usiku wa juzi.
Banda alimpongeza Rais Kikwete kwa kuandaa sherehe nzuri na za kuvutia, hasa onesho la halaiki ya watoto pamoja na gwaride na maonesho ya silaha za kijeshi.
Kwa upande wake, Changzhi  alieleza kuwa ilikuwa heshima pekee kwake kuhudhuria sherehe hizo za miaka 50 na kumwalikisha Rais Xi Jingping  wa China na kuwa sherehe hizo zilikuwa za mvuto uliokuwa wa kawaida kijeshi na kiraia.

No comments: