HAKIMU ACHOSHWA NA JAMHURI KESI YA AKINA MATTAKA

Hakimu Mkazi Augustina Mmbando amesema upande wa Jamhuri unamkwaza kwa kitendo cha kuchelewesha kesi ya kulisababishia Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) hasara ya Dola 143,442.75 za Marekani, inayomkabili Mkurugenzi mstaafu wa kampuni hiyo David Mattaka na wenzake.
Mbali na Mattaka washitakiwa wengine ni Kaimu Ofisa Mkuu wa Kitengo cha Fedha, Elisaph Ikomba na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Ndani, William Haji.
Mmbando alisema hayo jana wakati kesi hiyo ilipotajwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa lakini upande wa Jamhuri kuomba iahirishwe kwa kuwa shahidi hayupo.
Hakimu Mmbando alisema, kesi hiyo ni ya muda mrefu tangu mwaka 2011, lakini upande wa Jamhuri wanamkwaza kwa sababu ya kuichelewesha kwa kutokuleta mashahidi mahakamani.
Upande wa utetezi uliiomba Mahakama iamuru upande wa Jamhuri utoe orodha ya mashahidi walionao na kama hawana wafunge ushahidi  ili kesi iendelee kwa washitakiwa kuanza kujitetea.
Hakimu Mmbando ambaye alisema hana uwezo wa kufunga ushahidi na kuwalazimisha wataje orodha ya mashahidi wao, aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 16 mwaka huu.
Washitakiwa wanadaiwa kula njama, matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia Serikali hasara ya dola 143,442.75 za Marekani kwa kuagiza magari 26 chakavu kwa gharama ya dola 809,300 kutoka Kampuni ya Bin Dalmouk Motors ya Dubai bila kutangaza zabuni ya ushindani.
Aidha wanadaiwa kuruhusu kununuliwa kwa magari hayo bila mkataba wa ununuzi ambao umewekwa saini na wahusika na kuthibitishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kuisababishia Serikali hasara baada ya kushindwa kulipia kodi na kuchukua mkopo kwa ajili ya kuyakomboa na kuyatunza.

No comments: