DALADALA WAHIMIZWA KUWA PAMOJA KUINGIA DART

Wamiliki wa daladala wametakiwa kuongeza kasi ya kuunda umoja wao wa usafirishaji utakaokwenda sambamba na mradi wa mabasi yaendayo haraka kujiweka katika nafasi nzuri ya kuingia katika biashara utakapoanza.
Kauli hiyo imetolewa na Ofisa Mfawidhi wa Sumatra Kanda ya Mashariki, Conrad Shiyo  jijini Dar es Salaam jana.
Alisema muda wa kuanza kwa usafiri wa mabasi chini ya DART,  umekaribia hivyo ni vyema wenye daladala wakajipanga kuingia kwa wakati.
Alisema wakati wowote mwishoni wa mwezi huu,  tarehe ya kuanza kwa usafiri huo itatajwa hatua itakayositisha usafiri wa daladala katika barabara za mradi huo.
“Tunaamini kujiunga katika kampuni  kutawawezesha kuendelea kutoa huduma kama tulivyokubaliana kwa mujibu wa sheria, muda unazidi kwenda kabla ya kuanza kwa mradi wa DART ni vyema wakazingatia ujumbe huu,” alisema Shiyo.
Barabara zitakazohusika na usafirishaji huo kulingana na ujenzi  unaoendelea ni Morogoro kuanzia Kimara hadi Kivukoni pamoja na barabara ya Kawawa kuanzia eneo la Magomeni hadi Morocco.

No comments: