KUSHOTO: John Magufuli. KULIA: Baadhi ya malori yanayobeba mizigo kwenda nje ya nchi. |
Serikali imewaruhusu wamiliki wa malori kugoma kufanya biashara yao, kama hawakubaliani na sheria iliyopo ya kutoza wanaozidisha mizigo, ila wahakikishe wanagomea majumbani kwao na si barabarani.
Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli alisema hayo jana jijini Dar es Salaam, alipokuwa akitoa ufafanuzi wa mgomo baridi, ulioitishwa na Chama cha Wamiliki wa Malori (TATOA), uliopangwa kuanza jana kupinga tozo hiyo.
Alisema wanaotaka kuendelea na mgomo huo, wanaweza kuendelea, lakini wahakikishe hawaleti usumbufu kwa watumiaji wengine wa barabara.
Msemaji wa TATOA, Elias Lukumay katika tamko lake la kuitisha mgomo mwishoni mwa wiki, alisema kuwa mwaka 2006, Serikali ilitoa msamaha, kwamba haitatoza magari yenye uzito usiozidi asilimia tano, juu ya viwango vilivyowekwa kwa mujibu wa sheria baada ya kubaini umuhimu wa msamaha huo.
Katika tamko hilo, Lukumay alisema kabla ya kufikiwa msamaha huo, Serikali iliunda kamati iliyofanya ziara katika mizani na kubaini zina upungufu wa kutofautiana matokeo ya vipimo.
Mbali na upungufu wa mizani, Lukumay alisema pia kamati hiyo ilibaini kuwa ubovu wa barabara na matuta, umekuwa ukisababisha mizigo kuhama na kuzidisha uzito sehemu moja ya gari.
Alifafanua kuwa kuhama kwa mizigo, kunakosababishwa na matuta na ubovu wa barabara, husababisha ekseli, au muunganiko mmoja wa matairi unaotumika kupima uzito, kulemewa na kujikuta uzito ukiongezeka kutoka mizani moja kwenda nyingine, hata kama hakuna mzigo ulioongezeka.
Kutokana na uamuzi huo wa Serikali kwamba kuanzia Oktoba mosi mwaka huu, imefuta msamaha uliokuwa umetolewa awali kwa magari yaliyokuwa yanapimwa na kukutwa na ongezeko lisilozidi asilimia tano juu ya tani 56, iliyowekwa kwa mujibu wa Sheria, wameamua kuegesha magari yao popote yatakapokuwepo, ili wasiharibu barabara na wasigombane na Dk Magufuli.
Pamoja na kauli hiyo ya Lukumay, Dk Magufuli alisema kuwa na endapo Tatoa watatekeleza azma yao hiyo, itakuwa nafuu kwa barabara ambazo zimekuwa zikiharibiwa, kutokana na kuzidi uzito.
"Kama wanataka kugoma wafanye hivyo, mbona vyuo vikuu vinakuwa na migomo na hata mtoto nyumbani ukitaka kumlisha chakula anagoma, wanaweza kufanya hivyo kwa kuegesha magari yao majumbani na si barabarani.
"Itakuwa vizuri sana wakigoma, maana watafanya barabara zetu zicheke," alisema Dk Magufuli.
Dk Magufuli alisema ni kikundi cha wenyemalori wachache, ndio waharibifu wa barabara na kuwataka kuiga kampuni zingine kama Bakhresa na Dar Express, ambazo alisema hata siku moja hawazidishi uzito.
"Ninaweza kuwataja, maana wengine katika haka kakikundi, ndio wanaongoza kwa kujaza mizigo. Sisi tunasema kuwa tunaendelea kulinda barabara ambazo fedha za wananchi zinatumika kujenga. Hivyo kikundi hiki hakiwezi kuendelea kupata faida kubwa kupitia barabara," alisema.
Juzi madereva wa malori ya mizigo walifunga barabara ya Morogoro kwa zaidi ya saa 15, baada ya kukaidi agizo la Serikali na kusababisha usumbufu kwa watumiaji.
"Barua ndiyo iliyowapa nafuu hiyo, na sisi tumeirudisha kwa barua. Hakuna sheria inayovunjwa kwa barua, ila sheria ndiyo inayoweza kufuta sheria. Sheria ipo na tutaendelea kuisimamia. Baadhi ya kundi hilo ni wanasiasa wapeleke muswada bungeni kubadilisha," alisema.
"Sheria iliyopo inaruhusu mtu kuja kukataa rufaa kwa Waziri kama ameona sheria iliyopo haifai na kama hakuridhika na uamuzi utakaotolewa anatakiwa kwenda mahakama ya juu. Wanaweza kwenda mahakamani tukutane huko huko," alisema.
Magufuli alisema Tanzania ndio nchi pekee inayoongoza kwa kuruhusu mizigo ya ukubwa wa mpaka tani 56 kuliko nchi zinazoendelea, ambapo kwa Umoja wa Ulaya uzito ulioruhusiwa ni tani 40 hadi 45 wakati Marekani imeruhusu tani 36 tu.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema hali iliyojitokeza Jumamosi, haitajitokeza tena, kwa kuwa wamejipanga kudhibiti hali hiyo. Alionya kuwa watakaoegesha magari barabarani, watachukuliwa hatua kali za kisheria.
"Tutahakikisha mgomo hauleti usumbufu kwa watumiaji wengine wa barabarani na hii ndio kazi yetu," alisema na kuongeza kuwa mpaka sasa hajapewa taarifa ya mgomo huo, zaidi ya kusikia na kusoma kwenye vyombo vya habari.
Mwandishi alitembelea barabara ya Morogoro kuangalia kama mgomo huo umefanyika. Lakini, barabara ilikuwa nyeupe huku mizani ya Kibaha, ikionekana kufanya kazi yake kwa mabasi na malori kuingia na kupima mizigo yao.
1 comment:
Ukila na Kipofu usimshike mkono akigundua kuna mtu atacharuka Serikali ndiye Kipofu.
Post a Comment