CCM YAMKANA MWENYEKITI WAKE JUMUIYA YA WAZAZI...

Abdallah Bulembo (kushoto) na Nape Nnauye.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeikana kauli ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdallah Bulembo na kusema kauli ya  mwenyekiti huyo ni yake mwenyewe wala si msimamo wa chama.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi ndogo ya Makao Makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam jana, Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisema CCM kama taasisi ina imani kubwa na tume ya Warioba pamoja na wajumbe wake bila kuwabagua.
Hivi karibuni Bulembo alinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari akiwa mkoani Tanga na kudai kuwa, tume ya Jaji Warioba imeacha kutekeleza majukumu yake na kuingilia uhuru wa wananchi wa kutoa maoni.
Alisema msimamo wa CCM ni kwamba ni vizuri kama kuna mtu anataka kujadili hoja zinazotokana kwa mapendekezo yake binafsi asituhumu tume au kumjadili mtu binafsi ndani ya tume.
"Huu ni msimamo wa chama, haiwezekani tu mtu amshambulie mtu ndani ya Tume, hatuwezi kutuma mtu kushambulia tume isipokua mtu kama ameamua kwa hoja zake binafsi," alisisitiza Nnauye.
Nnauye aliwataka wanasiasa kuzingatia kuwa katiba inayoundwa ni ya watanzania wote sio ya wanasiasa pekee pia wanasiasa wajenge hoja na kuacha kuwanyooshea vidole watu ndani ya tume.
Alisema Tanzania ina watu zaidi ya milioni 40 sio rahisi katiba kumfurahisha kila mtu hivyo ni vizuri kuvumiliana hata kama kutakuwa na kutofautiana iwe bila kugombana, kushutumiana au kunyoosheana kidole.
"Tujenge hoja, tutetee hoja bila kutukanana, kuvunjiana heshima, kutuhumiana na CCM kama taasisi tunaahidi kutoa ushirikiano katika tume popote watakapohitaji kwa sababu tuna imani na tume, tuna imani na Jaji Warioba pamoja na wajumbe wote," alisema Nnauye.
Aliwataka watanzania kufuata sheria na taratibu walizojiwekea, kuvumilia na kuheshimiana ili mchakato huu wa kupata katiba uishe salama na wanasiasa kuepuka kuuteka mchakato huu.
Wakati huo huo, Katibu Mwenezi CCM wa Mkoa wa Dar es Salaam, Juma Simba alisema chama hicho kitafanya mkutano viwanja vya jangwani kesho mchana ambapo viongozi mbalimbali wa chama taifa na Serikali watakuwepo kuelezea mustakabali wa siasa na pia kuelezea namna wanavyotekeleza ilani.

No comments: