SENSA 2012 YAFICHUA IDADI KUBWA YA WATANZANIA NI WATOTO...

Baadhi ya watoto wa Kitanzania wakiwa darasani.
Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 inaonesha kuwa sehemu kubwa ya idadi ya watu  nchini ni watoto wenye umri wa chini ya miaka 15 na vijana.

Sensa hiyo inaonesha kuwa idadi ya Watanzania ni milioni 45, kati yao wanawake ni milioni 23 na wanaume milioni 21.9.  Tanzania Bara ina wanaume milioni 21.2 na wanawake milioni 22.4 na Zanzibar ina wanaume 630,677, wanawake 672,892.
Takwimu zilizotangazwa jana za Mgawanyo wa Watu kwa Umri na Jinsi zinaonesha asilimia 44  ni   wenye umri wa chini ya miaka 15. Kiasi hicho kinaelezwa kuwa juu kidogo ya wastani wa nchi za Afrika ambao ni asilimia 41. Uzinduzi huo ulifanywa na Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd.
Mkurugenzi wa Idara ya Takwimu ya Taifa, Albina Chuwa alisema kwa mujibu wa utafiti wa Mama na Mtoto wa mwaka 2010 kiwango cha uzazi nchini ni wastani wa watoto 5.4 kwa kila mama mwenye umri wa kuzaa. Alisema asilimia 27 ya wanawake ambao wameolewa ndio wanaotumia uzazi wa mpango wa njia za kisasa.
Takwimu hizo pia zinaeleza kuwa kwa kila watu 10 wa Tanzania, wanne ni vijana  ambao umri wao ni kati ya miaka 15 na 35. Idadi ya kundi hilo ni asilimia 35 ambao idadi yao ni milioni 16. Mkoa wa Dar es Salaam una asilimia kubwa zaidi ya vijana huku Singida ikiwa na asilimia ndogo zaidi ya watu walio katika kundi hilo.
Sensa hiyo imebaini kuwa asilimia 52.2 ya watu nchini wana umri wa kufanya kazi ambao ni kati ya miaka 15 na 64 .  "Takwimu hizi zinaonesha kuwa rasilimali watu kwa ajili ya kuzalisha na kuongeza uchumi na kupunguza umasikini si tatizo nchini.”
Chuwa alisema kinachotakiwa ni watu kutumia fursa zilizopo kufanya kazi kwa bidii ili kuinua uchumi wa nchi. Alitaja mkoa unaoongoza kwa kuwa na watu wengi wa kufanya kazi kuwa ni  Dar es Salaam ambako kwa kila watu watatu, wawili wana umri wa kufanya kazi huku Simiyu  ikiwa na idadi ndogo ambayo ni asilimia 45.5.
Takwimu hizo zimebainisha kuwa idadi ya watu wenye umri wa miaka 60 na zaidi ambao ni wazee ni  milioni 2.5 sawa na asilimia 5.6. Mkoa unaoongoza kwa kuwa na wazee wengi ni Kilimanjaro ambao una asilimia 9.7 , Dar es Salaam ikiwa na wazee wachache sawa na asilimia 3.5.
Kundi la watu wanaoishi mijini limeongezeka hadi watu milioni 13.3 sawa na asilimia 30 na kuacha   wanaoishi vijijini wakiwa asilimia 70. Hii inaonesha kuwa idadi ya watu vijijini imepungua huku  mijini wakiongezeka kutoka asilimia 20 hadi 30.
Kutokana na takwimu hizo, uwiano wa watu wenye umri tegemezi unaendelea kuwa juu na kulingana na matokeo ya sensa hiyo karibu watu 92 hutegemea watu 100 wenye umri wa kufanya kazi.
Mkoa wa Simiyu una uwiano wa juu ambao ni  119.7, Mara ina 113.2, Geita na Rukwa 112.9 huku uwiano wa chini kabisa ukiwa Dar es Salaam yenye 50.8.
Balozi Idd  alisema kwa matokeo hayo ameziagiza wizara, idara na taasisi za Serikali kuboresha sera zilizopo kwa kutumia takwimu hizo kupanga mipango ya maendeleo.
"Takwimu hizi zimetufungua macho na masikio kwa kuonesha hali halisi ya idadi ya watu nchini, hivyo ziwe kichocheo cha kupanga maendeleo sahihi kwa wananchi wa Tanzania," alisema Balozi Idd.
Alisema takwimu hizo hazitakuwa na manufaa endapo hazitafikia walengwa. "Natoa mwito kwa viongozi wa Serikali zote mbili kutumia na kusambaza matokeo haya katika ngazi zote za utawala kwa kutumia lugha nyepesi ambayo inaeleweka kwa wengi ili kuwezesha wadau kupanga mipango sahihi ya maendeleo."

No comments: