WANAOPINGA MUSWADA WA MABADILIKO YA KATIBA WASHAURIWA KURUDI MEZANI...

Peter Mziray.
Vyama vya siasa vinavyopinga Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba vimeshauriwa kurudi kwenye meza ya mazungumzo vikiaswa kuwa malumbano katika majukwaa ya kisiasa hayawezi kuleta suluhu.

Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa vyenye usajili, Peter Mziray alisema jana kwamba baraza hilo kwa kushauriana na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa wako tayari kukutanishwa katika meza ya mazungumzo na ngazi husika akiwamo Rais.
“Baraza la Vyama vya Siasa linavishauri vyama vinavyopinga Muswada uliopitishwa na Bunge kurudi kwenye mazungumzo...kama hoja zao ni nzito kwa nini wasionane na Rais kama walivyofanya mwanzo?” Alihoji Mziray alipozungumza mjini hapa na waandishi wa habari.
Alisema viongozi wa vyama vya siasa walipotofautiana na kutoridhika katika hatua za mwanzo, walikwenda Ikulu na kuonana na Rais Jakaya Kikwete ambaye aliwapokea kwa busara kubwa na kusikiliza hoja zao.
Mziray ambaye pia ni Mwenyekiti wa PPT, alisema kimsingi Baraza la Vyama vya Siasa halipingi viongozi wa vyama hivyo kufanya ziara na kuitisha mikutano ya hadhara mawazo yao.
Lakini alisema malengo mazuri ya wanasiasa si malumbano katika majukwaa ya kisiasa ambayo madhara yake ni makubwa baada ya kushawishi wananchi katika hoja ambazo si za msingi.
“Huwezi kufanikisha jambo la busara kwa njia ya shari...mifano ipo mingi, angalia leo hii Misri iko wapi?” alihoji.
Vyama vya siasa vinavyopinga Muswada uliopitishwa na Bunge ukisubiri kusainiwa na Rais, ni Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi. Viongozi wa vyama hivyo wameungana na kuandaa mikutano nchi nzima.
Wajumbe wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini walikutana hapa na kuzungumzia masuala mbalimbali yakiwamo vyanzo vya uvunjifu wa amani na matamshi ya wanasiasa katika majukwaa, yenye kuhatarisha amani ya nchi na utulivu.
Mkutano huo ambao vyombo vya habari havikuruhusiwa kuingia,  ulihudhuriwa na viongozi wa vyama vya siasa 21 vyenye usajili, CCM ikiwakilishwa na Makamu Mwenyekiti, Philip Mangula ambapo  Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi alikuwapo.
Aidha, Mziray alisema Baraza lake limepokea malalamiko kutoka  CCM na CUF kuhusu kauli zenye kuhatarisha amani na utulivu zinazotolewa na wanasiasa majukwaani.
“Ni kweli tumepokea malalamiko kutoka CUF kuhusu kauli za viongozi zinazotolewa katika mikutano ya hadhara... CCM nao wamelalamika na watatuletea ushahidi kwa njia ya kanda za video,” alisema Mziray.
Hivi karibuni, CCM na CUF ambao wanaunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, wamekuwa wakilumbana katika majukwaa ya kisiasa kuhusu suala la muundo wa Muungano.
Baraza la Vyama vya Siasa nchini limeundwa ikiwa ni matokeo ya mwafaka wa kisiasa wa CCM na CUF ambao lengo lake ni kumaliza migogoro ya kisiasa nchini.
Baraza hilo lina zaidi ya miaka saba sasa na linatambuliwa rasmi na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kama jukwaa la  kupatia ufumbuzi migogoro katika vyama vya siasa nchini.

No comments: