DALALI MBARONI DAR KWA UBOMOAJI MADUKA MTAA WA SAMORA...

Baadhi ya maduka yaliyoko kando ya Mtaa wa Samora.
Badala ya kusherehekea Idd el-fitri, baadhi ya wafanyabiashara katika mtaa maarufu wa Samora, Dar es Salaam walilazimika kuitumia siku ya jana kuhamisha bidhaa zao kutokana na amri ya kutakiwa kuhama katika majengo hayo yanayomilikiwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).

Hata hivyo, ubomoaji wa majengo hayo katika makutano ya mitaa ya Samora na Mkwepu ulisitishwa na polisi ili kuchunguza uhalali wa ubomoaji huo na kumshikilia Mkurugenzi wa kampuni ya Fosters Auctioners & General Traders, Joshua Mwaituka (43) aliyebandika tangazo la kubomoa.
Katika mtaa huo wenye maduka  zaidi ya 40 yakiwemo Shivacom ambaye ni wakala mkubwa wa kampuni ya simu, maduka matatu ya kubadilishia fedha, JM Studio, Flovar 4u, Modella na mengineyo kuligubikwa na vurugu huku vibaka wakipata nafasi ya kuiba milango na madirisha ya majengo hayo.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Mkurugenzi wa Hoteli ya Alcove, Sanjay Kanabar alisema katika hoteli hiyo ina wafanyakazi zaidi ya 40 ambao kwa sasa lazima wapumzike mpaka apate nafasi ya kufungua hoteli nyingine.
Alisema siyo kama wanakataa kuhama, bali walitakiwa kupewa hata miezi mitatu ili waweze kujipanga kufunga hoteli hiyo ambapo kwa sasa anakusanya vifaa na kuviweka katika maghala yake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi alisema kutokana na kuonekana suala hilo linaweza kusababisha uvunjifu wa amani imewalazimu kusitisha ubomoaji huo ili kuangalia kama unafanyika kihalali au la.
"Tumesitisha mpaka tuzungumze na wakala hawa na kuona namna ya kusimamia suala hili ili lisisababishe uvunjifu wa amani na wizi kwa vibaka huku tukisisitiza kufanyika kwa kufuata taratibu za utoaji notisi kwa wafanyabiashara," alisema.
Minangi pia alikiri kumshikilia Mwaituka kutokana na matusi na maneno ya jeuri aliyotoa kwa polisi wakati akiwa eneo la tukio walipofika ili kudhibiti uvunjifu wa amani usitokee.
Jumatano, wakala huyo wa udalali alitoa tangazo la kuwataka wafanyabiashara hao kuondoka katika majengo hayo kwa amri ya mahakama ili kubomoa majengo hayo leo alfajiri kutokana na kuwa ni hatarishi na hayafai kutumika kuishi binadamu.

No comments: