WANAOKAMIA URAIS 2015 KUPITIA CCM SASA KUDHIBITIWA...

Philip Mangula.

Wanachama wa CCM wanaofanya kampeni za chini kwa chini kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, wataanza kudhibitiwa kuanzia ngazi za chini kichama, imeelezwa.

Katika kuhakikisha udhibiti huo unafanikiwa, chama hicho kitafungua majalada maalumu ambamo taarifa za kila mmoja atakayekaidi amri hiyo taarifa zake zitahifadhiwa.
Utaratibu huo unalenga kukusanya ushahidi wa wakaidi wa agizo la chama hicho la kuwataka kutofanya kampeni za aina yoyote hadi muda mwafaka utakapofika.
Hayo yalibainishwa jana Dar es Salaam na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula alipotoa ufafanuzi wa masuala yanayoendelea katika chama hicho na kueleza kuwa wanachofuata ni kanuni na si uamuzi wa mtu.
Alisema wanafuatilia wanachama wao kwa kuweka kumbukumbu kuanzia kata ili kuangalia wanaoanza kampeni mapema za udiwani, ubunge na urais.
“Katika majalada hayo tutaweka kumbukumbu ya aliyofanya ikiwamo sehemu ya kurasa kwenye magazeti na ikiwa alifanya kampeni au mkutano watakuwa na ushahidi kwa kuhoji waliohudhuria na kuweka  kumbukumbu,” alisema. 
Mangula alisema wanafanya hivyo ili kupata ushahidi watakapokuwa wakifanya uamuzi kwa mujibu wa kanuni, ikiwa ni pamoja na kutokubaliwa kugombea nafasi yoyote ndani ya chama kwa kipindi ambacho Kamati Kuu itaona kinafaa.
Alisema kwa mujibu wa kanuni, kampeni zinatakiwa kufanywa baada ya Juni 2015  utekelezaji wa Ilani ya chama hicho ya sasa utakapokuwa umekamilika na kuandaliwa nyingine.  
Akizungumzia makundi ndani ya chama hicho, alisema ni mwiko kuwa na makundi kwa mujibu wa kanuni kwani yanavuruga umoja ndani ya chama.
“Ukiangalia Somalia makundi ndiyo sababu ya mapigano, kwani yalianza kama makundi ya maneno lakini baadaye yakawa makundi ya silaha,” alisema.
Aliongeza kuwa, wanaojenga makundi kwa kuzunguka na kujitangaza wanafanya kinyume cha kanuni kwani nao watachukuliwa hatua stahiki, huku akisisitiza kuwa, watu wa aina hiyo wakiachwa watagawa chama na kukidhoofisha.
Kuhusu malalamiko ya uchaguzi wa chama hicho kuwa kuna baadhi yao walitumia rushwa ili kushinda katika uchaguzi wa mwaka jana, alisema jambo hilo halijazikwa na  kwamba atakayethibitika kushinda kwa rushwa atang’olewa.
Alisema muda wa miezi sita uliopangwa kushughulikia malalamiko hayo ulimalizika jana, lakini imeongezwa miezi sita kwa kuwa Kamati iliyohusika ilichelewa kuanza kutokana na Kamati Kuu ambayo imeunda kamati ndogo, kuundwa Februari mwaka huu.
Alisema yalipokewa malalamiko 94 na baada ya kuyachambua, yamebaki 35 yanayofanyiwa kazi.

No comments: