Freeman Mbowe. |
Kambi ya Upinzani bungeni, imeonesha ukomavu unaolenga kudumisha amani, mshikamano na mustakabali wa nchi katika medani ya siasa za Tanzania.
Hali hiyo ilibainika jana baada ya vyama vikubwa vya upinzani, Chadema na CUF kuamua kuombana radhi kutokana na kuchafuka kwa hali ya hewa bungeni juzi, kulikofanywa na Msemaji wa Kambi ya Upinzani wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Ezekiel Wenje (Chadema-Nyamagana).
Chadema kupitia kwa Mwenyekiti wake ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe (Hai) iliomba radhi kwa CUF na Bunge kutokana na kutoa maneno yaliyothibitika kuiudhi CUF kwa kuihusisha na sera za kiliberali zinazounga mkono ushoga, usagaji na ndoa za jinsia moja.
Kwa upande wake, CUF nayo ilikubali na kuomba radhi kwa kumtamkia maneno makali na yasiyo na staha, Wenje aliyesoma hotuba ya kambi hiyo iliyokuwa na maneno hayo.
Hatua hiyo ilisababisha Naibu Spika, Job Ndugai kuahirisha kikao cha Bunge mara mbili juzi, na kusababisha mjadala wa hotuba ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje kwa mwaka ujao wa fedha, iliyowasilishwa bungeni na Waziri Bernard Membe kukatizwa.
Baada ya jitihada za awali za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge chini ya Kaimu Mwenyekiti wake Mbunge wa Manyoni Mashariki, John Chiligati, juzi kukwama kumshawishi Wenje kuiomba radhi CUF na kuondoa maneno ya kuudhi katika kurasa za saba na nane za hotuba hiyo, hatimaye Kamati hiyo ilimaliza suala hilo katika mjadala uliofanyika kuanzia saa 7.30 mchana juzi hadi saa 2.30 usiku.
Akisoma maazimio ya kikao hicho cha usuluhishi bungeni jana, Chiligati alisema kikao mbali na kushirikisha wajumbe wa Kamati hiyo pia kilihusisha marafiki wa Kamati hiyo, akiwamo Mbowe na Mbunge wa Mpanda Mjini, Said Arfi kwa upande wa Chadema huku CUF ikiwakilishwa na Mnadhimu Mkuu wao, Rashid Ally Abdallah na Rajab Mbarouk.
“Kikao hiki kilifanyika kwa kutanguliza mbele maslahi ya nchi na si ya vyama, kurejesha hali ya amani, utulivu, mshikamano, upendo na udugu ndani ya Bunge, lakini pia ili kuokoa bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa iliyokwama kutokana na suala hili,” alisema Chiligati.
Alisema katika kikao hicho Mbowe alisisitiza kilichoandikwa kwenye hotuba yao kwamba CUF ni mwanachama wa Umoja wa Kimataifa wa Kiliberali ambao moja ya sera zao ni kuheshimu uhuru wa mtu binafsi yakiwamo masuala ya ushoga, usagaji na ndoa za jinsia moja.
“Mbowe pia kupitia kikao hiki alitoa madai kwamba katika zogo hilo, CUF pia waliidhalilisha Chadema, kwa kumrushia maneno makali na ya kashfa Wenje, lakini pia kwa kuchana na kutupa kitabu chao cha hotuba na kuwa kutokana na vurugu hizo kikao cha Bunge kiliahirishwa.
“Wao CUF kupitia kwa Mbarouk walikiri kuwa CUF ni wanachama wa Umoja wa Kiliberali, lakini akasema hatua hiyo haina maana kwamba wanafuata na kuzikubali sera zote za umoja huo ikiwamo ya ushoga, usagaji na ndoa za jinsia moja na kwamba suala hilo halipo katika Katiba ya CUF wala katika maandiko yoyote yanayokihusu chama hicho,” alisema Chiligati.
Chiligati alisema pamoja na hoja hizo, CUF pia walisema Tanzania kama nchi ilishatoa msimamo wake juu ya suala la ndoa za jinsia moja kwa kupinga suala hilo na kuhoji itakuwaje wao kama chama wakubaliane na jambo ambalo nchi haikubaliani nalo na hivyo kuomba maneno hayo kufutwa na CUF kuombwa radhi.
“Baada ya mjadala huo, kwa pamoja tulikubaliana kuwa Chadema ili kujenga mshikamano na kuondoa uhasama waondoe maneno hayo yaliyoanzia ukurasa wa saba hadi wa tisa kwa vile hata kama walisema kwa nia njema, lakini yaliumiza na kuikera CUF.
“Halafu pia ili kujenga mshikamano na umoja, tulikubaliana Chadema waiombe radhi CUF kwa maneno yale hata kama yamefutwa, kwa vile tayari yalishatolewa na kuwaumiza CUF. Pia tulikubaliana Chadema waombe radhi kwa Naibu Spika kutokana na Wenje kukataa kuiomba radhi CUF alipoagizwa kufanya hivyo na Naibu Spika.
Pia Chadema waombe radhi kwa wabunge wote kwa usumbufu walioupata kutokana na kuahirishwa mara mbili kwa kikao cha Bunge,” alisema Chiligati.
Kwa upande wa CUF, alisema makubaliano yaliyofikiwa yalikuwa ni kwa chama hicho kuomba radhi kwa wabunge kutokana na maneno makali na lugha ya matusi waliyoitoa dhidi ya Wenje, waombe radhi pia kwa Chadema kwa kuchana na kutupa hotuba yao, waombe radhi kwa Naibu Spika na wabunge kwa lugha ya matusi na vurugu walizofanya na kusababisha kikao cha Bunge kuahirishwa mara mbili.
Baada ya maelezo hayo, Chiligati alimwomba Ndugai kuwapa nafasi Mbowe kuomba radhi kwa niaba ya Chadema na Rashid kuomba radhi kwa niaba ya CUF. Ndugai alitekeleza agizo hilo.
Akiomba radhi kwa niaba ya CUF, Rashid alisema CUF iliamua kulimaliza suala hilo kwa njia ya usuluhishi kwa kuzingatia maslahi ya nchi na ya wanachama wake.
Alikiri kwamba kutokana na maneno hayo ya Wenje, wabunge wa CUF damu iliwachemka na hivyo walitoa maneno makali na lugha mbaya na kuwaomba wote waliokwazwa na kitendo hicho kuwasamehe.
Mbowe kwa upande wake, aliomba radhi kwa CUF, Naibu Spika na kwa wabunge wote akisema anafanya hivyo ili kudumisha amani, mshikamano, umoja na upendo miongoni wa wabunge.
Alisema maneno hayo hayakutolewa na Wenje bali kambi nzima ya Upinzani Bungeni na kwamba baada ya majadiliano wamekubali kuomba radhi kwa vile hakuna maana kwa vyama kuangalia maslahi binafsi badala ya kuangalia maslahi ya nchi na Watanzania.
Aliposimama baada ya tukio hilo, Ndugai aliwashukuru wawakilishi hao wa vyama vyote viwili kwa kukubali kutekeleza maagizo hayo akisema maneno yao yamerejesha amani, mshikamano, upendo na utulivu bungeni.
Aliposimama baadaye, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema alisoma sehemu ya shairi la Shaaban Robert linalozungumzia upendo akidhihirisha kufurahishwa na hatua iliyofanywa na Chadema na CUF kuhusu sakata hilo.
Hata hivyo, hatima ya Wenje kuhusu sakata hilo hasa kwa kuzingatia kuwa chanzo cha sintofahamu hiyo kutokana na kukaidi maagizo ya Kamati na ya Kiti haikuwekwa wazi.
No comments:
Post a Comment