Jaji Joseph Warioba. |
Baada ya kazi ya kukusanya maoni juu ya muundo wa Katiba mpya kwa takribani mwaka mmoja, hatimaye mchakato wake unatarajiwa kuingia katika hatua nyingine keshokutwa.
Siku hiyo, Tume ya Mabadiiko ya Katiba inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba, inatarajiwa kuzindua Rasimu ya Katiba, ukiwa ni mwendelezo wa mchakato wa kupata Katiba mpya kabla ya uchaguzi mkuu mwaka 2015.
Hayo yameelezwa na Katibu wa Tume hiyo, Assa Rashid katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana akisema uzinduzi huo utafanyika katika viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam.
“Rasimu hiyo, itazinduliwa Jumatatu, kuanzia saa 8 mchana,” ilielezea sehemu ya taarifa hiyo iliyoonesha kuwa uzinduzi huo utarushwa moja kwa moja na vituo vya redio vya TBC Taifa na ZBC (Shirika la Utangazaji Zanzibar).
Pia vituo vya televisheni vya TBC 1 na ZBC TV na vituo vingine vya redio na televisheni vitafanya hivyo.
Alisema rasimu hiyo imetokana na maoni ya wananchi, viongozi na makundi waliyowasilisha kwa Tume kupitia mikutano, barua pepe, ujumbe mfupi wa simu za mikononi na nyinginezo.
Alisema Tume inaomba wananchi na wadau kufuatilia uzinduzi huo kwa makini kupitia vyombo hivyo vya habari.
No comments:
Post a Comment