WANAFUNZI 98,000 WA VYUO VYA ELIMU YA JUU KUPATIWA MIKOPO...

Baadhi ya wanafunzi na wageni wakipata maelezo kutoka kwa mhusika kwenye banda la Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu.
Wanafunzi 98,025 wa vyuo vya Elimu ya Juu nchini wanatarajiwa kupata mikopo mwaka ujao wa fedha, ambapo Sh bilioni 306 zimetengwa kwa ajili hiyo.

Ikilinganishwa na idadi ya wanafunzi walionufaika na mikopo hiyo mwaka wa masomo 2012/13, lipo ongezeko la takribani asilimia 2.4.
Mwaka uliopita Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu nchini ilikopesha  wanafunzi 95,594 kati ya 98,773 waliokuwa wameomba hadi Aprili 30.
Wizara hiyo imeomba Bunge liidhinishe matumizi ya Sh 689,681,055,000 kwa mwaka ujao wa fedha na kati ya hizo Sh bilioni 306 ni kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi hao.
Akisoma makadirio ya wizara yake bungeni jana, kwa mwaka wa fedha 2013/14, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Dk Shukuru Kawambwa alisema katika mwaka huo wa fedha, Serikali kupitia Bodi itatoa mikopo kwa wanafunzi hao wakiwamo waombaji 35,649 wapya na 62,376 wanaoendelea.
Pia alisema Bodi itakusanya marejesho ya mikopo ya Sh bilioni 28.8 kati ya Sh bilioni 44.2 zinazotarajiwa kukusanywa.
Alisema  Bodi itafungua ofisi Kanda ya Ziwa, Mwanza na kuziimarisha ofisi za Kanda za Zanzibar na Dodoma kwa kuziunganisha na Mfumo wa Utoaji Mikopo uliopo makao makuu ya Bodi ili kuziwezesha kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
"Ilifanikisha urejeshwaji wa Sh 10,128,238,670 za mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu. Hii ni asilimia 56 ya lengo la Sh bilioni 18 la mwaka 2012/13," alisema Dk Kawambwa.
Wizara hiyo iliomba Bunge liidhinishe matumizi ya Sh 689,681,055,000 kwa mwaka ujao wa fedha na kati ya hizo Sh bilioni 306 ni kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu.
Pia Waziri Kawambwa alisema katika mwaka ujao wa fedha Wizara yake kupitia Idara ya Elimu ya Ualimu itaratibu udahili wa jumla ya wanachuo 15,601, ambapo 8,690 ni wa cheti na 6,911 wa stashahada na kufanya jumla ya wanachuo wote katika vyuo vya ualimu vya Serikali kuwa 25,300 ikilinganishwa na 25,133 wa mwaka 2012/13.
Kwa upande wake, akisoma maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii, mjumbe wa Kamati hiyo, Zabein Mhita alisema pamoja na Serikali kutenga Sh bilioni 306 kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu Kamati imebaini utaratibu unaotumika kutoa mikopo hiyo haukidhi mahitaji ya wanafunzi waliotoka katika familia zenye vipato duni.
"Kamati inashauri Serikali iboreshe mfumo wa kupata wahitaji wa mikopo ili kuweza kujumuisha watoto wanaotoka katika familia zenye vipato duni.
"Juhudi za makusudi zitumike kuongeza makusanyo ya mikopo iliyokwishatolewa tangu mwaka 1991, kwani kiasi cha takribani Sh bilioni 8.8 zilizokusanywa (hadi Februari) na Bodi kati ya matarajio ya Sh bilioni 18 zilizotarajiwa kukusanywa kwa mwaka 2012/13.
"Serikali ianzishe Mfumo Maalumu wa Elimu kwa kuunganisha Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu na Sheria ya Mamlaka ya Elimu Tanzania kwa ajili ya kutoa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu nchini. Mfuko huo maalumu utabainisha vyanzo vya mapato kuhudumia mikopo hiyo," alisema Mhita.

No comments: