HUU NDIO UJUMBE MZITO ALIOTOA ABSALOM KIBANDA BAADA YA KUREJEA NCHINI...

Absalom Kibanda akizungumza na umati wa watu waliofika kumlaki kwenye uwanja wa ndege wa JNIA, Dar es Salaam, jana.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda, amerejea nchini na kuasa waandishi wa habari, kuhakikisha  tukio kama lililomkuta haliwakuti wanahabari wengine.

Kibanda ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa New Habari Limited (2006), aliwasili nchini jana na kupokewa na umati wa wanahabari na wadau wa habari hali iliyomfanya, ashindwe kujizuia kutoa machozi  kwa uchungu uliochangamana na furaha.
Hali ilikuwa mshikemshike katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), baada ya Mhariri huyo kutokeza huku akipungia mikono, hali iliyozua kelele za shangwe na vilio na simanzi.
“Ndugu zangu, marafiki zangu nimetokwa na machozi hapa si kwa kuwa nalia kwa uchungu au niko kwenye maumivu la hasha, ni kwa sababu nimeguswa na mshikamano mlionionesha, niliondoka hapa nikiwa na hali mbaya, leo hii jamani nimerejea salama,” alisema Kibanda alipozungumza uwanjani hapo. 
Alibainisha kuwa amerejea salama na kutokana na tukio lililomkuta hana maumivu moyoni wala halaumu mtu.
“Nawahakikishia Watanzania sina maumivu ya moyo wala kulaumu mtu, kila kitu kinatokea kwa sababu zake, nimeguswa sana na mshikamano huu mlionionesha leo, naamini hamtaishia hapa kwa kuwa sisi waandishi wa habari tuna wajibu wa kulinda Taifa letu liepukane na matukio kama haya yaliyonikuta,” alisisitiza.
Alizungumzia hali aliyokuwa nayo wakati akiondoka nchini baada ya kushambuliwa, kuwa haikuwa nzuri kwani alikuwa akipoteza fahamu mara kwa mara na hata alipowasili Afrika Kusini, madaktari walimtaarifu kuwa alikuwa na hali mbaya.
Alisema kwa sasa tasnia ya habari iko kwenye kiza kizito kutokana na matukio mfululizo ya wanahabari kujeruhiwa na kuuawa, yakiwamo tukio lake mwenyewe, David Mwangosi wa Channel Ten kuuawa, Said Kubenea wa Mwanahalisi kushambuliwa kwa tindikali na waandishi wengine.
Alisema hali hiyo imejidhihirisha wazi kwenye ripoti ya uchunguzi kuhusu kutekwa na kujeruhiwa kwake iliyofanywa na TEF ambayo imedhihirisha wazi kuwapo kwa hali ya utata kuhusu tukio lililomkuta.
“Jamani matukio haya yote; la kwangu la akina Mwangosi si ya bahati mbaya, la Kubenea nililishuhudia, lakini masikini sikujua kama na mimi yatanikuta haya, naomba tuhakikishe kama wanahabari tukio hili la Kibanda linakuwa la mwisho,” alisisitiza.
Alisema tukio la kushambuliwa kwake Machi 6 ambalo lilimwacha na ulemavu wa jicho, kidole na kumvunja mifupa kadhaa mwilini, mikakati yake na namna lilivyofanywa halina tofauti na lililomkuta Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Steven Ulimboka.
Kuhusu hatua zilizochukuliwa na vyombo vya Dola kuhusu waliomfanyia unyama huo hadi sasa, Kibanda alisema baada ya kukutwa na mkasa huo, viongozi wakuu akiwamo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova na Mkuu wa Polisi nchini IGP Said Mwema, walimtembelea.
“Wote hawa walinihakikishia kuwa watafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha wahusika wote walionifanyia unyama huu wanafikishwa kwenye mikono ya sheria, lakini pia walimtuma hadi mpelelezi mkuu Afrika Kusini ambaye alinihoji,” alisema Kibanda.
Alitaka Watanzania wasimlilie bali walilie Taifa kwa kuwa hadi sasa pamoja na mfululizo wa matukio hayo hakuna hatua madhubuti zilizochukuliwa dhidi ya wahusika.
“Kwa hili naomba niseme mwenyewe, sitaki kusemewa na iwapo Mungu atanipa uzima nitaendelea kusema, kama binadamu anaweza kumng’oa jicho mwenzake, kumkata kidole na kumng’oa meno hatuna budi kuhakikishia Taifa letu linaondokana na matukio kama haya,” alisema.
Naye Katibu wa TEF, Neville Meena, alisema kwa niaba ya wanahabari nchini ni jambo la kushukuru kwamba hatimaye Kibanda amerejea nchini salama na kwa sasa kazi iliyobaki ni kuhakikisha wanahabari wote wanakuwa na mshikamano zaidi.
“Kama wanahabari tunataka kuona usalama wetu unapewa kipaumbele, lakini kubwa zaidi jambo la msingi kwa sasa ni vyombo vya Dola kutia nguvuni wahusika wote wa matukio haya, kwani kwa hali ilivyo wanahabari wote hatuko salama,” alisema.
Machi 6, Kibanda alivamiwa wakati akirejea nyumbani kwake Mbezi Juu, Dar es Salaam, na watu wasiofahamika na kumjeruhi vibaya kwa kumng’oa meno, kucha na kumharibu jicho la kushoto hali iliyosababisha akimbizwe Afrika Kusini kwa matibabu zaidi.

No comments: