WAAGIZAJI SARUJI WAIANGAMIZA NCHI KIMAPATO...

Serikali imekuwa ikipoteza mapato yake kutokana na kodi inayokwepwa na waagizaji wa saruji nchini.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi na kuthibitishwa na vyanzo ndani ya Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA), umebaini kwamba kwa mwaka hasara ambayo imekuwa ikipatikana kutokana na mchezo huo mchafu inafikia jumla ya Sh bilioni 26.5 kwa mwaka.
Udanganyifu huo umekuwa ukifanyika kwa waagizaji hao ambao ni wafanyabiashara maarufu nchini wakimiliki kampuni tatu kubwa, kwa kudanganya makadirio ya shehena inayoingizwa bandarini  na katika mipaka katika maeneo ya Dar es Salaam, Mtwara, Mbeya, Arusha na Zanzibar.
Kampuni hizo ambazo majina yao kwa sasa yanahifadhiwa, ziko Tanzania Bara na Zanzibar. “Tunaweza kuona wazi kabisa, udanganyifu unaofanywa na waagizaji hao wakubwa katika kodi wanazokwepa kwa kudanganya kiwango na thamani ya mzigo wanaoingiza nchini,” kinasema chanzo chetu cha habari.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa kwa miezi mitatu tu ya Februari, Machi na Aprili kama sampuli, jumla ya tani zilizoagizwa na wafanyabiashara hao ni 135,000 kutoka Pakistani na Kenya.
Mchanganuo unaonesha kuwa tani 94,000 ziliingizwa Dar es Salaam kutoka Pakistani, zilizoingia Mtwara ni tani 5,608 pia kutoka Pakistani, tani 7,460 ziliingia Arusha kutoka Kenya, tani 2,777 ziliingia Kanda ya Ziwa pia zikitoka Kenya ambapo tani 1,843 ziliingia Mbeya zikitoka Zambia huku 23,531 zikiingia Zanzibar kutoka Pakistani.
Kulingana na uchunguzi huo, saruji hiyo imekuwa ikiingia nchini kutoka kampuni za Lucky Cement na Mapple Leaf zote za Pakistani.
Wakati waagizaji wadogo nchini wamekuwa wakiwasilisha thamani ya mzigo kwa kati ya dola 90 na 100 za Marekani kwa tani ikilinganishwa na thamani halali inayotambuliwa Pakistani, imebainika kwamba kwa Zanzibar waagizaji wanawasilisha thamani ya dola 58 kwa tani.
Dar es Salaam kampuni tatu ambazo majina tunayo, zinawasilisha thamani ya kati ya dola 52 na 80 huku kampuni ya Mtwara ikiwasilisha thamani ya dola 59.
Matokeo yake, kodi ya uagizaji bidhaa kwa saruji inatozwa asilimia 25 tu, huku ada ya ukaguzi ikiwa ni asilimia mbili na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ikitozwa asilimia 18 tu.
Hali hiyo pia inaifanya TRA kutoza kodi ya asilimia 25 kwa saruji, wakati kodi halali kwa mujibu wa gazeti la Serikali iliyotangazwa Juni mwaka jana, inapaswa kuwa asilimia 35 ya thamani ya mzigo.
“Ipo mifano mingi ya udanganyifu kwa kila muamala unaofanywa kulingana na kiwango cha bidhaa inayoingia nchini, unaweza kuona kontena linasomeka kuwa na tani 23.3 wakati lina tani 28, matokeo yake kunakuwa na makadirio ya chini kwa takribani asilimia 20 ya kodi,” kilisema chanzo hicho.
Kwa kipindi hicho cha miezi mitatu ya Februari hadi Aprili kulikuwa na hasara ya kodi kwenye saruji kama ifuatavyo katika miji ya Dar es Salaam, Zanzibar na Mtwara:
Tani 11,175 zilikadiriwa kodi ya dola 60 badala ya 90, hivyo thamani ya jumla iliyotangazwa ikawa dola 6,670,500 badala ya dola 10,005,750. Asilimia 20 ya mzigo ilitolewa makadirio ya chini, hivyo thamani halali ingepaswa kuwa dola 12,006,900.
Mchanganuo wa ukusanyaji kodi, unaonesha kuwa kinachokusanywa leo ni dola 6,670,500X25% sawa na dola 1,667,625 wakati kinachotakiwa kukusanywa ni dola 12,006,900X35% sawa na dola 4,202,415; hapo tofauti ni dola 2,534,790.
Katika ada ya ukaguzi kinachokusanywa leo ni dola 6,750,500X2% sawa na dola 133,410 wakati kinachotakiwa kukusanywa ni dola 12,006,900X2% sawa na dola 240,138, hivyo tofauti kuwa dola 106,728.
Kwa upande wa VAT, kinachokusanywa leo ni (dola 6,750,500+1,667,625+133,410)X18% sawa na dola 1,524,876 huku zinazotakiwa kukusanywa ni (dola 12,006,900+4,202,415+240,138)X18% sawa na dola 2,960,901 tofauti ikiwa dola 1,436,026.
Hivyo hasara katika ukusanyaji kodi ya Serikali katika kipindi hicho cha miezi mitatu ni dola 4,077,544.

No comments: