JWTZ YAKANUSHA TAARIFA MABOMU KURUSHWA KUTOKA NCHI JIRANI...

Moja ya aina za mabomu.
Watu wasiojulikana wanadaiwa kutumia jina la Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kusambaza ujumbe wenye kuleta taharuki nchini, ukidai yapo mabomu yaliyorushwa nchini kutoka nchi jirani.

JWTZ  katika taarifa yake jana imesema pamoja na kwamba ujumbe huo haukutolewa nao, pia hakuna mabomu hayo nchini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Habari na Uhusiano, Makao Makuu ya Jeshi, ujumbe  huo pia ulifikishwa kwao.
Ujumbe huo wa simu umenukuliwa na JWTZ ukisema, ‘Habari zilizotufikia hivi punde. Mtanzania yeyote, kaa makini usiokote kitu chochote ambacho una shaka nacho, kuna bomu zimerushwa toka nchi jirani Malawi zaidi ya 30 zenye uzito usiopungua tani 100. Hivyo basi uonapo kitu kipo kama chupa la chai chenye rangi ya fedha. Usiguse.  Piga namba 0756 000042. SMS hii tuma kwa watu uwezavyo. Imetolewa na JWTZ’.
“JWTZ inapenda kuwaondoa wananchi hofu kutokana na taarifa hiyo. Kwanza, ujumbe huo haujatolewa na JWTZ.  Jeshi haliwezi likatumia mfumo huo wa SMS kuwapa wananchi wake taarifa za hatari kama hizo. Aidha, JWTZ hutangaza kupitia vyombo rasmi kama vile Magazeti, Radio na Televisheni,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Katika ufafanuzi zaidi, jeshi hilo limesema  bomu la tani 100 ni zito mno na  halijawahi kutengenezwa duniani. JWTZ imefafanua zaidi kwamba, “na kama lipo bomu, haifahamiki  litarushwa vipi, kwa kutumia ndege au Mzinga?”.
“Lakini pia, mzinga wa aina hiyo haupo duniani kote na wala hakuna ndege yenye uwezo huo, hasa kwa bomu lenye umbile dogo kama hilo (Chupa ya Chai).”
Jeshi limesisitiza kwamba habari hizo hazina ukweli kisayansi wala kiuhalisia au fikra za kawaida. Limeomba wananchi kupuuza taarifa hizo kutokana na kuwa za uongo.
 Limehakikishia wananchi kwamba kama kungekuwepo taarifa za namna hiyo, lisingewajulisha kwa simu za mkononi.
Akizungumza na mwandishi kuhusu matumizi mabaya ya simu za mkononi, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Senso amehadharisha wananchi juu ya kushiriki kusambaza meseji mbaya zinazolenga kuchochea au kusababisha uhalifu.
“Mwananchi hata ukitumiwa na mtu mwingine, na wewe usisambaze maana na wewe unajiweka kwenye mkumbo wa kukamatwa,” alisema Senso.
Alisema, polisi inaendelea na ukamataji wa watu wanaojihusisha na usambazaji wa ujumbe wa simu wa kuchochea, kuhamasisha vurugu na vitisho. 
Wakati wapo waliofungwa kutokana na kutiwa hatiani kwa vitendo hivyo, Senso alifahamisha gazeti hili kwamba wapo watu kadhaa mkoani Lindi na Mtwara ambao kesi zao zinaendelea kuandaliwa ili sheria ichukue mkondo wake.
Hivi karibuni, mkazi wa Mburahati, Nassoro Mohamed (25) alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kwa kosa la kutoa taarifa za uongo na kutuma ujumbe wa maneno ya kuudhi kwa Waziri wa Mambo ya Ndani Emmanuel Nchimbi na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Said Mwema.
Wakati wakijadili bajeti ya Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia iliyowasilishwa jana bungeni na Profesa Makame Mbarawa, baadhi ya wabunge walikemea matumizi mabaya ya teknolojia mpya kwa kufanya uchochezi, sanjari na kutukana.
Mbunge wa Viti Maalumu, Leticia Nyerere (Chadema) alisema wengi wanaofanya vitendo hivyo, hawafahamu kama wanaweza kukamatwa kwa kutumia teknolojia mpya.
Alisema wapo watu ambao wanadhani wakijifungia vyumbani na kutumia kompyuta kutuma ujumbe wowote, hawawezi kukamatwa.
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba akijibu hoja mbalimbali za wabunge, alionya watu wanaojifungia na kutengeneza meseji za uchochezi, watanaswa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Wakati Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ikiwa imetangaza kwamba namba za simu za mikononi mpya na zisizosajiliwa, zitafungiwa, Mkurugenzi wa mamlaka hiyo, Profesa John Nkoma alisema kampuni za simu pia zinapaswa katika usajili kuhakikisha vitambulisho vinakuwa na picha halisi za waombaji wa laini.
Profesa Nkoma alikuwa akizungumza na mwandishi  juu ya matumizi mabaya ya simu za mkononi yanayofanywa na watu mbalimbali kwa kutumia laini ambazo zimesajiliwa lakini kwa majina ya uongo.

No comments: