Wilfred Rwakatare na wenzake wakitoka mahakamani. |
Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema,Wilfred Rwakatare na mwenzake Ludovick Joseph wamepata nafuu kidogo baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuwafutia baadhi ya mashitaka.
Mahakama Kuu ilifuta mashitaka yote matatu ya ugaidi, dhidi ya Rwakatare na Joseph.
Kutokana na uamuzi huo uliotolewa na Jaji Lawrence Kaduri, Rwakatare na Joseph walibakiwa na mashitaka ya jinai, chini ya Sheria ya Kanuni ya Adhabu, ambayo yanaruhusu dhamana.
Jaji Kaduri alifuta mashitaka hayo wakati akitoa uamuzi wa ombi la Rwakatare, la kutaka Mahakama hiyo ifanye marejeo ya mwenendo wa kesi ya ugaidi, inayomkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Ombi hilo, liliwasilishwa Machi 22, baada ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), kuwafutia mashitaka washitakiwa hao, kisha kukamatwa na kusomewa upya mashitaka hayo.
Akitoa uamuzi huo jana, Jaji Kaduri alisema hati ya mashitaka iliyofunguliwa na DPP, haielezi uhalisia wa kosa hilo na washitakiwa wanahusika vipi kufanya ugaidi.
“Hati ya mashitaka lazima itoe uhalisia wa kosa husika (ugaidi), ili haki itendeke, lakini maelezo yaliyoletwa na upande wa mashitaka, hayahusu kosa la ugaidi,” alisema.
Jaji Kaduri alisema anakubaliana na maelezo ya Wakili wa Lwakatare, Tundu Lissu, kuwa washitakiwa hawakufanya kikao cha kigaidi, kama inavyodaiwa, kwa kuwa walikuwa wawili na kikao cha kigaidi kinahusisha watu zaidi ya watatu, hivyo anafuta mashitaka yote yanayohusu ugaidi.
Washitakiwa hao walifutiwa mashitaka ya kupanga njama za kufanya kitendo cha ugaidi cha kumteka Mhariri wa gazeti la Mwananchi, Dennis Msacky, kupanga na kushiriki mkutano wenye lengo la kutenda kitendo cha ugaidi ambacho ni kumteka Msacky.
Mashitaka yaliyobaki dhidi ya washitakiwa hao, ni ya kuruhusu mkutano kati yake na Joseph, kufanyika nyumbani kwake katika eneo la King’ongo, Kimara Stop Over, kwa lengo la kuhamasisha vitendo vya ugaidi.
Kutokana na uamuzi huo, sasa washitakiwa hao wanadaiwa kupanga njama ya kutenda kosa la jinai la kutumia sumu kumdhuru Msacky, ambapo wanadaiwa kulitenda Desemba 28 mwaka jana King’ongo, Kinondoni, Dar es Salaam.
Kuhusu DPP kutumia madaraka vibaya kufuta mashitaka na kuyafungua upya, Jaji Kaduri alisema DPP hakukosea, kwa kuwa aligundua makosa yaliyokuwa kwenye kesi ya awali, likiwamo la washitakiwa kuruhusiwa kujibu mashitaka katika shauri ambalo halisikilizwi katika Mahakama hiyo.
Uamuzi huo uliibua furaha kwa wafuasi wa Chadema waliofika mahakamani hapo kusikiliza kesi hiyo.
Akizungumza nje ya Mahakama, Wakili wa Rwakatare, Peter Kibatala, alimpongeza Jaji Kaduri kwa kutoa uamuzi aliouita wa kihistoria na kuongeza kuwa hatua hiyo ni ushindi kwa Rwakatare, kwa kuwa mashitaka yanayomkabili yana dhamana.
Hata hivyo, mawakili wa Serikali, walidai kutoridhika na uamuzi huo kwa kuwa Jaji hakuwa na haki ya kufuta mashitaka hayo, hivyo watakata rufaa. Upelelezi wa kesi ya msingi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi umekamilika na itaendelea Mei 13.
No comments:
Post a Comment