Sehemu ya wabunge wanaounda Bunge la Jamhuri ya Muungano wakifuatilia kikao mjini Dodoma. |
Baada ya kubaini kuwa wao ndio chanzo cha uvunjifu wa amani kutokana na kauli zao bungeni, wabunge wameona haja ya kuangalia upya sheria, ikiwamo ya kinga ambayo inawapa uwezo wa kutoa kauli hizo.
“ Pande zote za wabunge zimekuwa zikitoa lugha za chuki ndani ya Bunge kwa kisingizio cha kinga, hili halifai, halifai, halifai, sisi tunaanzisha wimbo humu ndani na watu wanaitika. Tuzuie kauli za chuki ndani na nje ya Bunge,” amesema Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi na Usalama, Anna Abdallah.
Akitangaza jana azimio kuhusu tukio la kulipuliwa bomu Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Arusha Jumapili, Anna alisema wabunge wengi wamekuwa wakitoa lugha za chuki kwa kisingizio cha demokrasia na kuwakumbusha kuwa hakuna demokrasia isiyo na mipaka.
“Hakuna haki utakayoipata kwa kuvunja haki ya mwingine, huwa najiuliza ni kwa nini kikundi kinaanzishwa kuipinga BAKWATA (Baraza Kuu la WaislamuTanzania) na kinasajiliwa?” alihoji.
Kuhusu shambulizi hilo, aliitaka Serikali kuchukua hatua dhidi ya viashiria vyote vya uvunjifu wa amani.
Kwa azimio hilo, Bunge liliitaka Serikali kuhakikisha uchunguzi wa kina unafanywa na kuwatia nguvuni wahusika wote wa tukio hilo na kisha kuwafikisha kwenye vyombo vya kisheria, ili kuwapa wananchi matumaini ya kujumuika na kuabudu kwa uhuru bila hofu ya usalama wao.
Alisema katika miaka ya karibuni, zimekuwapo dalili za uvunjifu wa amani na utulivu ambapo baadhi ya viongozi wa dini wamekuwa wakijeruhiwa, kuuawa na baadhi ya nyumba za ibada kuchomwa moto.
“Hali hii imekuwa ikiwatia hofu wananchi wa imani na hali zote na kuhoji kiini cha matukio haya, tukio la mlipuko wa bomu limeongeza hofu miongoni mwa Watanzania na kuendelea kutikisa misingi ya amani, utulivu na mshikamano miongoni mwao,” alisema Anna.
Alisema pamoja na kazi nzuri ya Serikali kukamata baadhi ya watuhumiwa, Bunge liliitaka Serikali na vyombo vya Ulinzi na Usalama kuhakikisha wanatumia uwezo uliopo kuchunguza kwa kina na kuchukua hatua stahiki haraka.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira alisema hakuna mtu aliyehusika na mlipuko huo atakayepona na wote watashughulikiwa bila kujali hadhi zao.
Alitaka Watanzania kwa sauti moja kushinda vitendo vya kigaidi na kutolea mfano Marekani ambao baada ya matukio ya ugaidi waliungana bila kujali tofauti za kidini na kisiasa.
“Hakuna dini inayoogopa Mungu itakayounga mkono tukio lile na kama ipo basi wanaabudu kingine na si Mungu, na kuna chama au dini itafurahia hili labda kama hawatumikii wananchi,” alisema.
Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Zitto Kabwe (Chadema) alisema ongezeko la matukio hayo ni dalili kuwa nchi ina nyufa zinazotumiwa na maadui katika kuvuruga na kugawa Watanzania.
Alisema wakati umefika wa kuangalia sheria za nchi ili kuzuia lugha za chuki.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, pamoja na kulaani tukio hilo, alisema kauli za viongozi wa dini na siasa zinakuwa kichocheo cha chuki katika jamii.
Akitolea mfano, Simbachawene alisema: “Tuangalie, hapa tunaweza kugombana, lakini tukitoka tunakumbatiana na kula pamoja, vivyo hivyo viongozi wa dini ambao wanaweza kupanga mambo yao pamoja, lakini kuna watu tunaowapelekea ujumbe ndio wanaoathirika na kujikuta wakitumika.”
Aidha, Simbachawene alitoa mwito kwa Watanzania kuwa ni vizuri kuangalia sheria za uhuru wa kuabudu na kutangaza dini na uhuru wa kufanya mihadhara.
Mbunge wa Mkanyageni, Mohamed Habib Mnyaa (CUF), alisema muda mrefu wananchi wamekuwa wakifurahia kwa amani na utulivu na hivi sasa chokochoko zinazojitokeza zinaweza kuipeleka pabaya nchi ikiwa wananchi hawatakuwa makini katika kudhibiti hali hiyo.
“Nahadharisha kuwa kama kuna baadhi ya watu kupitia mgongo wa siasa wanataka kutumia Waislamu pekee wanajidanganya na kama kuna watu kupitia siasa wanaweza kutumia makanisa kutawala nchi, hii haiwezekani,” alisema Mnyaa.
Aliomba vyombo vya ulinzi na usalama kuwa makini na kuacha kudhani kuwa huenda majanga hayo yanatokana na kauli za kwenye miadhara kwa kuwa kuna uwezekano zikachochewa na mataifa ya nje.
Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), aliitaka Serikali kutokuwa na kigugumizi katika kuchukua hatua kwenye majanga makubwa kama hayo na kuwa ipo haja kwa Serikali kusimamia Katiba na vyombo vya Dola kutekeleza wajibu wao bila kuegemea upande wowote.
Mbatia alionya wanasisasa wanaotumia muda mwingi kuanzisha chokochoko kwa viongozi wa dini na kuwa ni wajibu wa viongozi wa siasa wa pande zote, kutopenda kupata madaraka kwa kutumia damu ya Watanzania.
Mbunge wa Viti Maalumu, Fakharia Khamis Shomar (CCM), alitaka Watanzania kuungana katika kupambana na tatizo hili na kutaka wahusika kuchukua hatua za kisheria stahiki ambazo zitaridhisha kila mtu.
Mbunge wa Vunjo, Augustino Mrema (TLP), alitaka vyombo husika vinavyotoa vibali vya uanzishwaji wa makanisa na vikundi vya dini kufuatilia kinachofanywa na watu hao.
“Siamini kwa Wakristo wanaohubiri wana sifa za kufanya hivyo, na pia tupige marufuku mihadhara yenye mwelekeo wa kashfa na matusi na yeyote atakayehusika apigwe marufuku na anyang’anywe leseni, natoa siku saba jambo hili lishughulikiwe.”
Mbunge Viti Maalumu, Getrude Rwakatare (CCM), alisema mashambulio hayo yamekuwa yakijitokeza kutokana na Serikali kuchukua hatua dhaifu na kuitaka ichukue hatua kwa ukamilifu na kupendekeza kupitia upya sheria hizo ili kunusuru nchi.
Wakati huo huo, Spika Anne Makinda aliongoza jopo wa wabunge 23 jana kwenda Arusha kuwapa pole wafiwa na majeruhi.
Sambamba na hilo, wabunge walikubaliana kutoa posho yao ya siku moja ikiwa ni mchango wao kwa waathirika wa tukio hilo.
No comments:
Post a Comment