MATOKEO KIDATO CHA NNE 2012 YAANZA KUPITIWA UPYA...

Wanafunzi wakifanya mtihani wa Kidato cha Nne mwaka jana.
Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) limeanza kazi ya kupanga upya daraja la ufaulu kwa wanafunzi wa kidato cha nne waliomaliza mwaka jana na ambao matokeo yao yamefutwa.

Limesema baada ya kupokea barua ya kufanya hivyo juzi mchana, wameanza kazi ili kuhakikisha matokeo hayo yanatolewa mapema kwa kufanya kazi usiku na mchana hata mwishoni mwa wiki.
Akizungumza na mwandishi jana, Ofisa Habari wa NECTA, John Nchimbi alisema wamepokea maelekezo kwa barua na kufanyia kazi ili kujitahidi ndani ya muda mfupi matokeo yawe yametoka.
Nchimbi alikiri kuwapo kwa kasoro katika matumizi ya mfumo huo mpya wa usahihishaji, kwani hawakushirikisha wadau wengi kabla ya kuanza kutumia, lakini lengo la Baraza lilikuwa jema katika kukuza elimu nchini
“Kutokana na tangazo hili, wanafunzi hawa wote hawana matokeo tangu juzi, hivyo wasubiri matokeo mapya yatakayotangazwa, na waelewe wazi kuwa si lazima waliofeli wafaulu wote,” alisema.
Aidha, wadau wengine wa elimu walitoa mawazo yao kuhusu uamuzi huo na kueleza kuwa usahihishaji kwa mfumo huo ungeendelea, ili kukuza kiwango cha elimu, kwani inaonekana kiwango kinazidi kushuka.
Walitaka waliofeli wangerudia mitihani ili kukuza uelewa, jambo ambalo ni la kawaida kuliko kurudi katika mfumo wa zamani.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana, alitaka wanasiasa kuacha kuingilia uhuru wa wanataaluma, kwani mfumo huo mpya una sababu hai za kukuza elimu.
Alieleza kuwa ni vema kuangalia upya mfumo mzima wa elimu, kwani umevurugika kwa wanaomaliza kwa viwango tofauti hawapati elimu inayostahili.
Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba, alisema kuacha mfumo huo mpya si suluhisho, kwani kufanya vibaya kutaendelea na hivyo ni vema kuangalia tatizo.
Alibainisha kuwa wapo waliofeli na kutaka kusahihishiwa upya lakini wakafeli zaidi  hivyo ni vema kuangalia mustakabali wa elimu kwa kujali mifumo yote ya elimu ili kupata suluhisho.
Juzi Serikali ilitoa kauli yake ya kufutwa kwa matokeo ya mitihani ya kidato cha nne mwaka jana ambayo yalitangazwa na Necta na kuonesha idadi kubwa ya wanafunzi kufeli.
Hatua hiyo ililazimisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuunda tume iliyoongozwa na Profesa Sifuni Mchome kuchunguza kiini cha mserereko wa wanafunzi wa kidato cha nne kufeli kila mwaka na kuja na mapendekezo hayo.
Hata hivyo, Tume hiyo inaendelea na kazi yake ili kupata suluhisho la kudumu la tatizo hilo ambalo linaathiri mustakabali wa nchi katika nyanja za elimu.

No comments: