UJENZI WA BOMBA LA GESI MTWARA-DAR ES SALAAM KUENDELEA...

Profesa Sospeter Muhongo.
Serikali imewasilisha bungeni hotuba ya bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka ujao wa fedha, huku ikisisitiza kuwa azma ya kujenga bomba la kusafirisha gesi ya asili kutoka Mtwara kuelekea Dar es Salaam  iko pale pale.

Hotuba hiyo pia imeelezea kuongezeka kwa kiwango cha umeme kinachozalishwa na kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa, kuongezeka kwa mapato yatokanayo na sekta ya madini na  mpango wa kupeleka umeme kwenye makao makuu ya wilaya mbalimbali nchini.
Mbali ya kugusia maeneo hayo, katika historia tangu Uhuru, asilimia 90 ya bajeti hiyo ya Wizara kwa mwaka ujao wa fedha imeelekezwa kwenye miradi ya maendeleo, huku asilimia 10 ikielekezwa katika matumizi yakiwemo ya mshahara.
Akiwasilisha hotuba hiyo bungeni mjini hapa jana, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, alisema  hatua za awali za ujenzi wa mitambo ya kusafirisha gesi asili kutoka Mtwara zimeanza.
Alisema ujenzi wa miundombinu inayokwenda sambamba na mradi huo utaleta manufaa makubwa kwa Taifa na kwamba hadi sasa Mikoa ya Lindi na Mtwara imepata manufaa mbalimbali yatokanayo na miradi ya gesi asilia.
“Manufaa hayo ni pamoja na tozo ya asilimia 0.3 ya mauzo ya gesi asilia, huduma za jamii kama zahanati, shule, umeme, maji na ufadhili wa mafunzo katika Vyuo vya VETA na sekondari.
Alisema manufaa mengine yatakayopatikana ni pamoja na ujenzi wa viwanda mbalimbali  vikiwemo Kiwanda cha Saruji cha Kampuni ya Dangote ambacho ujenzi wake umeanza, Kiwanda cha mbolea, mtambo wa kufua umeme wa megawati 400 kupitia kampuni ya Symbion na ujenzi wa njia ya kusafirishia umeme ya msongo wa kilovoti 220 kutoka Mtwara hadi Songea.
“Aidha Kampuni ya Schlumberger ya Houston, Marekani imejenga karakana kubwa Mtwara ambayo itakuwa inatengeneza vifaa vya uchimbaji, utafutaji na uendelezaji wa rasilimali za mafuta na gesi badala ya kupeleka nje ya nchi,” alisema Waziri.
Alisema taratibu za kupata umiliki wa maeneo ya ujenzi wa viwanda vyenye kutumia gesi asilia zinaendelea katika Mikoa ya Lindi na Mtwara na kwamba ujenzi huo utaongeza fursa za ajira kwa Watanzania na kukuza mapato ya serikali.
Mradi wa ujenzi wa bomba hilo lenye urefu wa kilometa 532 na kipenyo cha inchi 36 likiwa na uwezo wa kusafirisha futi za ujazo za gesi asilia milioni 784 kwa siku, ulizinduliwa na Rais Jakaya Kikwete Novemba 8, mwaka jana.
Katika sekta ndogo ya umeme, Waziri Muhongo alisema katika kipindi cha mwaka wa fedha uliopita, Serikali iliendelea kuboresha upatikanaji wa umeme ambapo hadi kufikia Aprili mwaka huu uwezo wa mitambo ya kufua umeme ulikuwa ni megawati 1,438.24, ikilinganishwa na uwezo wa megawati 3,375.75 uliofikiwa Juni, mwaka jana.
Alisema hadi kufikia Desemba 31, mwaka jana kiasi cha umeme kilichozalishwa na kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa kilikuwa megawati 5,759,756 ikilinganishwa na megawati  5,153,400 mwaka 2011 sawa na ongezeko la asilimia 11.8.
Alisema tatizo la wizi na uharibifu wa miundombinu ya umeme nchini, kwa muda mrefu umekuwa sugu kutokana na wahusika kubuni njia mbalimbali za kufanya uharibifu huo na kulisababishia Shirika la Umeme nchini (Tanesco) na nchi hasara ya Sh milioni 966.18 hadi ilipofika Aprili mwaka huu.
Waziri Muhongo alisema Serikali kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (REA) imeendelea kupeleka umeme katika Makao Makuu ya Wilaya na maeneo ya vijijini na kwamba upelekaji wa umeme katika Makao Makuu ya Wilaya za Namtumbo, Ruvuma na Nkasi mkoani Rukwa umekamilika.
“Aidha Serikali kupitia REA imeendelea kuwezesha utekelezaji wa Mradi Kabambe wa Awamu ya Kwanza wa Kusambaza Umeme Vijijini katika Mikoa 16 ya Tanzania Bara ambapo gharama za mradi huo ni Sh bilioni 129,” alisema Waziri Muhongo.
Alisema upelekaji umeme katika Makao Makuu ya Wilaya ya Nyang’hwale umefikia asilimia 77  na utagharimu Sh bilioni 4.59 na kwamba Mkandarasi wa kupeleka umeme Makao Makuu ya Wilaya za Bukombe na Mbogwe ambaye ni Kampuni ya Eltel Networks TE AB ya Sweden amepatikana.
Alisema tathimini ya zabuni za kuwapata makandarasi wa kutekeleza awamu ya Pili ya Mpango Kabambe wa Usambazaji Umeme Vijijini chini ya REA itakamilika mwishoni mwa Mei mwaka huu ambapo chini ya mpango huo umeme utapelekwa katika Makao Makuu ya Wilaya 13 za Buhigwe, Busega, Chemba, Itilima, Kakonko, Kyerwa, Mkalama, Mlele, Momba, Nanyumbu, Nyasa na Uvinza kwa Sh bilioni 70.
Waziri Muhongo alisema katika mwaka uliopita wa fedha, Wizara iliendelea kutekeleza mipango mbalimbali ya kukuza shughuli za utafutaji, uchimbaji na biashara ya madini nchini.
Alisema katika kipindi hicho, Wizara pia iliimarisha usimamizi wa Sekta ya Madini ili kuongeza mchango wake kwenye pato la Taifa. Alisema kiwango cha ukuaji wa shughuli za kiuchumi za uchimbaji madini kilifikia asilimia 7.8 katika mwaka 2012 ikilinganishwa na asilimia 2.2 mwaka 2011 na hivyo pato la Taifa kuongezeka hadi asilimia 3.5 kutoka asilimia 3.3.
Alisema katika kuimarisha usimamizi wa biashara ya madini, Serikali kupitia Wakala wa Ukaguzi wa Madini (TMAA) imeanzisha madawati maalumu ya kukagua madini yanayosafirishwa nje ya nchi kupitia Viwanja vya Ndege vya Kimataifa vya Julius Nyerere, Dar es Salaam, Kilimanjaro na Mwanza.
“Madawati hayo yamesaidia katika kubaini na hatimaye kuwakamata  watu wasio waaminifu wanaosafirisha madini nje kinyume cha sheria. Kwa kipindi cha kuanzia Oktoba, 2012 hadi Aprili 2013, madini yenye thamani ya Sh bilioni 13.12 yalikamatwa yakisafirishwa nje,” alisema.
Waziri Muhongo aliliomba Bunge kupitisha bajeti ya Sh trilioni 1.1 kwa mwaka ujao wa fedha, ambapo kati yake Sh bilioni 992.2 sawa na asilimia 90 ni kwa miradi ya maendeleo na Sh bilioni 110.2 sawa na asilimia 10 tu ni kwa matumizi ya kawaida.

No comments: