Abdallah Zombe. |
Mahakama ya Rufaa leo inatarajia kutoa uamuzi wa rufaa ya kupinga kuachiwa huru kwa aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Abdallah Zombe na wenzake wanane.
Hatua hiyo inatokana na jopo la majaji kubaini kasoro katika taarifa ya kusudio la kukata rufaa, kabla ya kuanza kusikiliza rufaa hiyo, iliyokatwa na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).
Aidha, Jopo la Majaji Edward Rutakangwa, Bathuel Mmila na Mbarouk Mbarouk, watatoa uamuzi huo baada ya mawakili wa Zombe, kuomba Mahakama kutupa rufaa hiyo kwa kuwa haikuwasilishwa kwa kufuata kisheria.
Katika ombi hilo la mawakili wa Zombe, Wakili Magafu alidai kwa mujibu wa kanuni, kama hakuna taarifa ya kusudio la kukata rufaa, maana yake rufaa hiyo haijawasilishwa na kwa kuwa taarifa hiyo haikuwasilishwa inavyotakiwa kisheria, anaomba Mahakama kuona hakuna kusudio hilo na kutupa rufaa hiyo.
Akibainisha upungufu uliopo kwenye taarifa hiyo, Jaji Mbarouk alisema katika taarifa hiyo, mawakili wamedai wanapinga hukumu iliyotolewa na Jaji wa Mahakama ya Rufaa, iliyotolewa katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Alisema taarifa hiyo, inaonesha kuwa hukumu hiyo ilitolewa na Mahakama ya Rufaa na Mahakama hiyo inaruhusiwa kusikiliza rufaa zinazotoka Mahakama Kuu pekee.
Majaji hao walisema kwa mujibu wa Katiba ya nchi, Ibara ya 119, Jaji yeyote wa Mahakama ya Rufaa, hana mamlaka ya kusikiliza kesi katika Mahakama Kuu au mahakama yoyote ya chini.
Aliongeza kuwa endapo Jaji wa Mahakama Kuu atateuliwa kuwa wa Mahakama ya Rufaa, ataendelea kusikiliza na kutoa uamuzi wa mashauri aliyokuwa akisikiliza, kabla ya kuteuliwa.
Mawakili wa Serikali walikiri kuwapo kwa kasoro hiyo na kuiomba Mahakama, iruhusu wafanye marekebisho katika taarifa hiyo na kuandika hukumu hiyo imetoka Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment