Dk Emmanuel Nchimbi. |
Serikali imesema kuanzia sasa haitakuwa na kigugumizi kukabiliana na wachochezi wa chuki za kidini miongoni mwa Watanzania na kukiri kuwa hali imefikia hapo kutokana na Serikali kulegalega kwa dhana ya uhuru wa kuabudu.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi alipofunga mkutano wa siku mbili wa viongozi wa dini Dar es Salaam juzi usiku.
Alisema tukio la kurushwa bomu kanisani mkoani Arusha limetikisa viongozi wote wa nchi kwa kuwa wahusika walikuwa na lengo la kuwafarakanisha lakini hawakufanikiwa.
Aliongeza kuwa kwa tukio hilo walitarajia Wakristo wangelipiza kisasi lakini haikuwa hivyo ila walichofanikiwa ni kutia chuki nyoyoni mwa Watanzania.
Alisema nchi imefika hapa, kutokana na kupuuza viashiria kwa kuendekeza uhuru wa kuabudu, katika masuala mbalimbali ikiwamo mihadhara.
“Tumefika hapa sababu tumelegea vya kutosha, nitakuwa Waziri wa ajabu kukubali Taifa lipasukie mikononi mwangu, kabla sijapasua wachochezi,” alisema.
Pia Serikali iliagiza Jeshi la Polisi kuacha kucheka na watu wanaotumia mihadhara au mahubiri kueneza chuki bali liwakamate na kuwafikisha mahakamani.
Nchimbi alisema kiongozi sehemu yoyote kutakakofanyika mihadhara bila hatua kuchukuliwa atafukuzwa kazi.
“Kila sehemu kuna viongozi wa kipolisi wa mtaa na wilaya…kukiwa na mikutano hiyo ya kuchochea siku mbili hatua haijachukuliwa, unakwenda na maji,” alionya Waziri.
Alitaka viongozi wa dini kuwakatisha tamaa wanasiasa wanaotaka uongozi kupitia kwao, kwani wanapandikiza mbegu ya chuki katika jamii.
Aliwasihi waumini wafike katika nyumba za ibada kusali na si kufanya siasa na wakubaliane kwa kauli moja kumkataa ‘mdudu’ huyu wa chuki.
Nchimbi alibainisha wazi kuwa Tanzania imejeruhiwa na kutoka damu, hivyo ni lazima kuponya majeraha hayo na kwa kufanya hivyo “lazima mtasikia vilio, kwani sasa hatutakuwa na kigugumizi.”
Alisema awali kulikuwa na watu wanaokaa siku nzima - asubuhi mpaka jioni - na kuzunguka nchi nzima kutukana wenzao wa dini nyingine, bila kujiuliza wanapata wapi fedha za kuishi.
“Tusaidieni kuondoa sumu ya chuki ndani ya watu, kwa kuwaeleza waumini wenu makanisani na misikitini kuwa chuki ni sumu kali, wafundisheni, wasihini na hata kuomba,” aliwaomba viongozi hao wa dini.
Alisema kuna mabingwa wa kugawa watu ambao wametumia vyama vya siasa na kuanguka kwa uchumi lakini hawajafanikiwa na sasa wanatumia usafiri wa dini kugombanisha.
Nchimbi alisema barabarani si rahisi kubaini nguvu iliyopo ya chuki za kidini lakini kwa mitandao ya kijamii, mbegu inadhihirika na ikiendelea hivyo, baada ya mwaka mmoja hakutakuwa na Tanzania.
Hivyo aliwasihi vijana katika mitandao ya kijamii wajiepushe na lugha za chuki na kusambaza ujumbe mfupi katika simu za mkononi zinazochochea chuki za kidini, kwani sasa Serikali itaanza kuwakamata.
Alisema polisi hawawezi kufanya doria ya wananchi kupendana kwani mapenzi ya watu yako ndani ya dhamira zao, hivyo ni lazima kuendeleza utamaduni wa kupendana na kutunzwa kwa muda mrefu.
Akimshukuru Waziri Nchimbi, Shehe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Salum, alitaka viongozi wa dini kuendeleza ushirikiano na kuahidi kusaidiana na Serikali kudhibiti viashiria vya chuki miongoni mwa jamii.
No comments:
Post a Comment