RASIMU YA MWONGOZO UUNDAJI MABARAZA YA KATIBA YATOLEWA...

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 2005.
Tume ya Mabadiliko ya Katiba imetoa rasimu ya mwongozo wa uundwaji wa mabaraza ya Katiba yatakayoundwa na kuendeshwa na taasisi, asasi, vyama na makundi ili kujadili na kutoa maoni kuhusu rasimu ya Katiba itakayoandaliwa na Tume.

Kwa  mujibu wa rasimu hiyo iliyotolewa jana na kusambazwa katika mitandao ya kijamii ikiwamo tovuti www.katiba.go.tz) na ukurasa wa facebook wa Tume, mwisho wa wananchi na wadau kuwasilisha maoni yao kuhusu mwongozo huo ni Mei 19.
Rasimu hiyo inafafanua, kuwa uundaji wa mabaraza ya Katiba ya asasi, taasisi na makundi hayo unapaswa kutegemea Katiba, kanuni na randama ya asasi husika.
“Miongoni mwa asasi, taasisi na makundi ya watu wenye malengo yanayofanana yanayoweza kuunda mabaraza ya Katiba ni kama jumuiya ya kidini, chama cha siasa, asasi ya kiraia, taasisi ya elimu ya juu, chama cha wanahabari,” inasomeka rasimu itakayochapishwa katika magazeti ya Habari Leo, Zanzibar Leo na Mwananchi ya leo na kurudiwa katika magazeti hayo Jumatatu.
Kwa mujibu wa Tume, asasi nyingine zinazoweza kuunda mabaraza hayo ni Taasisi ya Elimu ya Juu, Chama cha Wafanyakazi, Chama cha Wakulima, Chama cha Wafugaji, Baraza la Watoto, Taasisi ya Wafanyabiashara, Baraza la Wanawake, Taasisi ya Wanataaluma, Baraza la Vijana, Baraza la Wazee na kundi au makundi ya watu wenye malengo yanayofanana au yenye mahitaji maalumu katika jamii.
Katika rasimu hiyo, Tume inapendekeza asasi zinazotarajia kuunda mabaraza kutoa taarifa ya maandishi kwake kuhusu kusudio la kuunda, kuendesha na kusimamia mabaraza ya Katiba.
“Taarifa hiyo itawasilishwa katika ofisi za Tume ya Mabadiliko ya Katiba moja kwa moja makao makuu, mtaa wa Ohio, Dar es Salaam au ofisi ndogo Zanzibar au kutumia posta (S.L.P. 1681, Dar es Salaam au S.L.P. 2775, Zanzibar) au barua pepe katibu@katiba.go.tz),” inasomeka sehemu ya rasimu hiyo.
Mabaraza ya Katiba yanaundwa kwa mujibu wa kifungu cha 18 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83. Kwa mujibu wa kifungu cha 18(6) cha sheria hiyo, Tume inaweza kuruhusu asasi, taasisi na makundi ya watu wenye malengo yanayofanana, kuandaa mikutano kwa ajili ya kutoa fursa kwa wanachama kutoa maoni juu ya rasimu ya Katiba na kisha kuwasilisha maoni hayo kwa Tume.

No comments: