SERIKALI YAPANGA KUANZISHA MAHAKAMA ZA KESI NDOGO...

Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe.
Serikali ina mpango wa kuanzisha mahakama ndogo zitakazoshughulikia kesi ndogo pekee kama vile matatizo ya Wamachinga na wizi mdogo, ili kutoa fursa kwa mahakama nyingi kushughulikia kesi kubwa na kupunguza mlundikano wa kesi.

Aidha, Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, imeshauri Serikali iangalie uwezekano wa kubadili mfumo wa uandishi wa sheria zake sasa na kuziandika kwa lugha nyepesi inayoeleweka, ikiwa ni pamoja na kuondokana na maneno magumu ili wananchi wazielewe na kuzitumia kirahisi.
Mwenyekiti wa Tume hiyo, Aloybius Mujulizi, alisema hayo mjini hapa jana wakati akikabidhi taarifa ya mapitio ya mfumo wa madai Tanzania na tamko la Sheria za Kimila kwa Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe.
Alisema wakati wakifanyia kazi marekebisho ya mfumo huo wa madai na tamko la sheria za kimila walipata fursa ya kuhusisha wananchi ambao waliainisha upungufu unaogusa mfumo wa usimamizi wa haki katika kesi za madai nchini na kutoa mapendekezo.
Alisema kati ya mapendekezo hayo ni pamoja na wananchi hao kutaka mfumo wa uandishi wa sheria hizo ubadilishwe, ili wapate fursa ya kuzisoma na kuzielewa sheria zote zinazogusa haki na maslahi yao.
“Kwa hiyo imependekezwa kuwa sheria zisomeke na zieleweke kirahisi zaidi bila kuwa na sentensi ndefu zisizoeleweka, kwa kuwa sheria nyingi ni ngumu kueleweka na zenye maneno magumu, hali ambayo inawanyima haki wananchi wengi,” alisema Mujulizi.
Aidha, alisema wananchi wengi walilalamika kuwa sheria nyingi zimeandika kwa lugha ya Kiingereza, lugha ambayo inazungumzwa na wachache, hivyo wengi wao wanashindwa kuzielewa.
Pia alisema hivi sasa wananchi wengi wenye madai ya msingi wanasita kupeleka mashauri yao mahakamani kwa kuhofia gharama kubwa za kupata mawakili, ikiwa ni pamoja na gharama kubwa za kesi.
“Ilipendekezwa kuwa gharama za kufungua kesi za madai nazo ziangaliwe upya, wananchi wengi wanalemewa na gharama kubwa kupeleka kesi zao mahakamani, pia mapendekezo yametolewa ya kupunguzwa kwa muda wa kesi kuanza na kumalizika,” alisisitiza.
Alisema maoni hayo mengi yalitolewa na kupendekezwa na wananchi na wadau katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Mbeya, Mwanza na Dodoma.
Akizungumzia mfumo huo wa madai, alisema Tume hiyo ilipitia mapendekezo na upungufu uliopo kwenye sheria hiyo ya madai kutokana na ukweli kuwa mfumo mzuri wa kesi za madai katika Taifa lolote la kistaarabu, huwezesha kuwepo na utaratibu mzuri wa utatuzi wa migogoro ya kibiashara na kuondoa urasimu na vikwazo katika eneo la haki.
Katika mapitio ya tamko la sheria za kimila, Mujulizi alisema katika sheria hizo walibainisha sheria za mila ambazo hazikujumuishwa katika tamko la kimila na kuzijumuisha, ikiwamo sheria ya kutambua mkondo wa ukoo wa mama.
Akipokea ripoti za marekebisho ya sheria hizo, Chikawe alisema ripoti hizo atazisoma kwa kina na kufanyia kazi mapendekezo yote yaliyotokea kwa kuzingatia maslahi ya Watanzania.
“Kuna umuhimu wa kesi hizi kufanyiwa marekebisho mara kwa mara, unajua kule bungeni sisi tunapitisha sheria kisha tunazitupa uraiani, sasa chombo hiki kazi yake ni kufuatilia utekelezaji wa sheria hizo na kama zinaendana na hali halisi, mfano tu kwa sasa nchi yetu haifanyi vizuri katika eneo la kasi za biashara,” alisema.
Hata hivyo, alisema kwa sasa Serikali inaangalia uwezekano wa kuunda mahakama ndogo, ili ziweze kushughulikia kesi ndogo kama zile za Wamachinga, wizi wa kuku ili kutoa fursa kwa mahakama zingine kubwa kushughulikia kesi kubwa na kupunguza msongamano.

No comments: