PRECISIONAIR YAWAHAKIKISHIA ABIRIA SAFARI ZA ZANZIBAR...

Moja ya ndege za Precisionair.
Uongozi wa Shirika la Ndege la Precisionair (PW), umewahakikishia wateja wake kuwa inaendelea na safari zake visiwani Zanzibar kama kawaida.

Akizungumza na mwandishi juzi, Ofisa Mtendaji Mkuu wa PW, Sauda Rajab, alisema taarifa kwamba Bodi ya Mapato ya Zanzibar (ZRB) imezuia ndege za shirika hilo kutua visiwani hapo si za kweli.
Alisema hakuna hali kama hiyo na kwamba safari zinaendelea kama zinavyopangwa na tatizo lililokuwapo baina ya pande hizo mbili lilishatatuliwa katika mkutano uliofanyika Aprili 29 na kwamba PW inaendelea kupata ushirikiano mkubwa kutoka ZRB.
“Kilichotokea ni tatizo la mawasiliano tu baina ya pande hizi mbili lakini tunafarijika kwamba baada ya mazungumzo yetu, hivi sasa tunaweza kwa uhakika kusema, kwamba tunaendelea na bishara kama kawaida na tunakukaribisheni wateja wetu kuendelea na mipango yenu ya kusafiri na PW,” alisema Sauda.
PW ambayo imo katika orodha ya Soko la Hisa la Dar es Salaam, inafanya safari zake katika viwanja 18 ndani na nje ya nchi, ikiwa ndilo shirika linaloongoza nchini kwa kufanya safari nyingi za ndege ndani na nje ya nchi.
Hivi sasa ina ndege tisa aina ya ATR na mbili aina ya Boeing baada ya mwaka jana kuongeza ndege mbili za ATR.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari juzi, ZRB ilisema imezuia ndege za PW kutua na kuruka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar, kutokana na kutolipa zaidi ya Sh bilioni 37.2 zinazotokana na malimbikizo ya malipo ya ada ya huduma ya uwanja wa ndege.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, amri hiyo ilitolewa na Kamishna wa ZRB, Abdi Faki, Aprili 25 kutokana na malimbikizo hayo.

No comments: