Mtuhumiwa wa kesi ya ubakaji wa watoto, Jacob Mayani (28), juzi alifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Shinyanga kusomewa mashitaka mawili ya kutenda vitendo vyenye nia ya kusababisha madhara, kubaka na kulawiti watoto wenye umri wa kati ya miaka minane na kumi, wanafunzi wa shule za msingi.
Ilidaiwa na Mwendesha Mashitaka Mwanasheria wa Serikali, Solomon Lwenge mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Shinyanga Lidya Ilunda, kuwa mshitakiwa ambaye ni mkazi wa Mshikamano Manispaa ya Shinyanga alitenda makosa hayo.
Ilidaiwa kuwa katika Wilaya na Mkoa wa Shinyanga kwa nyakati na maeneo tofauti mshitakiwa alitenda makosa yenye nia ya kusababisha madhara makubwa kwa kuwabaka, kuwalawiti na kuwatoboa macho watoto watatu kinyume na kifungu cha 222 kifungu kidogo A cha kanuni ya adhabu sura ya 16 kama kilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2010.
Mshitakiwa anakabiliwa na mashitaka mawili ambayo yatatajwa na kusikilizwa katika kesi mbili tofauti. Kosa la kwanza ni kufanya vitendo vyenye nia ya kusababisha dhara kuu na kosa la pili ni la kuwabaka na kuwalawiti watoto watatu katika matukio na maeneo tofauti ya Manispaa ya Shinyanga.
Inadaiwa kuwa mshitakiwa aliwabaka na kuwatoboa macho watoto watatu katika maeneo ya Ndembezi, Ndala na Kitangili na kuwasababishia madhara makubwa watoto watatu ambao wawili kati yao walilazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando na mmoja katika Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga.
Mshitakiwa alikamatwa katika jaribio lake la kutaka kumbaka
mtoto wa wanne katika mtaa wa Mwasele Manispaa ya Shinyanga baada ya mtoto husika kumponyoka na kupiga kelele za kuomba msaada ambapo wasamaria walijitokeza na kumkamata mtuhumiwa na kisha kumfikisha Kituo cha Polisi.
No comments:
Post a Comment