MTOTO AZINDUKIA CHUMBA CHA MAITI BAADA YA AJALI ILIYOTEKETEZA FAMILIA NZIMA...

Eisa akiwa amepakatwa na baba yake mkubwa, Shazada Hayat.
'Mtoto wa miujiza', ambaye alinusurika kwenye ajali ya gari ambayo iliua watu watano wa familia yake, alifungiwa kwenye mfuko wa kubebea miili ya wafu na kupelekwa chumba cha kuhifadhia maiti kabla ya madaktari kubaini kwamba alikuwa hai.

Mtoto huyo Eisa Hayat, mwenye umri wa mwaka mmoja, alikuwa manusura pekee wa ajali hiyo ya gari ambayo ilifuta kabisa familia ya Kiingereza wakati wakielekea kuhiji Makka.
Madaktari nchini Saudi Arabia walidhani mtoto huyo mchanga pia alifariki katika ajali hiyo ya gari na kumpeleka kwenye nyumba hiyo ya maiti.
Walikuwa wakijiandaa kumuweka kwenye jokofu ndipo walipoona mfuko huo ukitikisika.
Eisa, ambaye alinusurika kimiujiza pale babu yake alipotumia mwili wake kumkinga kutoka kwenye athari za kishindo hicho, baadaye alipelekwa hospitali amepona kabisa.
Baba yake mkubwa Shazada Hayat alisema: "Walifikiri: 'oh, mtoto huyo mdogo alikuwa amefariki, hakuna yeyote ambaye angeweza kupona katika ajali ile'.
"Hivyo walimchukua, wakamfungia kwenye mfuko na kumpeleka katika nyumba hiyo ya maiti. Aliishia kwenye chumba cha kuhifadhia maiti.
"Lakini wakati wakimuweka kwenye jokofu, alijigeuza. Walimvuta, na kumpakia kwenye gari la wagonjwa na kumkimbiza katika Hospitali ya Watoto ya Medina."
Eisa, ambaye ndio ameanza kuelekea miaka miwili, aliondoka na jamaa zake kutoka nyumba yao ya familia mjini Newport, South Wales, kwa ajili ya safari hiyo ya kidini.
Kizazi hicho cha tatu cha familia hiyo walikuwa wamesafiri maili 3,000 ndipo taksi hiyo waliyokuwa wakisafiria ilipopata ajali.
Eisa alipoteza wazazi wake wote, babu zake na shangazi pale dereva alipolala na gari hilo kuserereka nje ya barabara na kujibamiza katika  kingo za daraja.
Baba Isshaq na mama Bilques, wote wakiwa na umri wa miaka 33, walifariki kwenye ajali hiyo - huku Bilques akiwa mjamzito wa miezi saba.
Babu Shaukat, miaka 56, bibi Abia, miaka 47, na shangazi Saira Zenub, miaka 29, pia walifariki katika ajali hiyo.
Eisa alipelekwa kwenye nyumba hiyo ya maiti ambako alizinduka huku akiwa amezungukwa na watu asiowafahamu.
Aligundulika muda mfupi na kukimbizwa hospitali ambako alitibiwa kufuatia bega lake kuteguka, kuvunjika mkono na mbavu.
Eisa kwa sasa analelewa na jamaa zake kufuatia kukabiliana na ajali mbaya akiwa anakaribia miaka miwili na wanasema ni miujiza kwamba amenusurika.
Shazada, ambaye anafanya kazi ya Uanasheria, aliongeza: "Kushuhudia familia ya Eisa ikiteketea chini ya dakika zisizozidi 10, unafanya nini? Unaanzia wapi?
"Tunatakiwa kuhakikisha kwamba tunakuwa karibu naye kila wakati kama ambavyo wazazi wake wangefanya.
"Wakati ni mponyaji mkuu - unaweza kuponya baadhi ya sehemu lakini kawaida kila wakati kuna nafasi ya wazi kwa ajili yake.
"Eisa ni muhimu sana kwetu, ni kiungo pekee kilichobaki katika kupanua familia yake."
Kufuatia ajali hiyo ya Februari, Eisa amerejea Saudi Arabia kutembelea makaburi ya familia yake huko eneo la makaburi la Jannat-ul-Baqi, mjini Medina.

No comments: