Baadhi ya masoko yanayouza vyakula vya nafaka. |
Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), imesema mfumuko wa bei wa Taifa kwa Aprili mwaka huu, umepungua hadi kufikia asilimia 9.4 kutoka asilimia 9.8 ya Machi mwaka huu.
Aidha, uwezo wa Sh 100 ya Tanzania kununua bidhaa na huduma, umeendelea kupungua.
Kwa sasa, kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii wa NBS, Ephraim Kwesigabo, Sh 100 ya sasa, inaweza kununua bidhaa za Sh 70.62 za Septemba 2010 na si zaidi.
Kwesigabo alisema hayo jana alipokuwa akizungumzia kupungua kwa mfumuko wa bei kwa Aprili. Alifafanua kwamba hali hiyo inamaanisha kuwa, kasi ya upandaji wa bei za bidhaa na huduma kwa mwezi huo imepungua, ikilinganishwa na kasi ya kupanda kwa bei kwa Machi.
Aidha, alisema mfumuko wa bei za vyakula na vinywaji baridi, umepungua hadi asilimia 10.2 Aprili mwaka huu, kutoka asilimia 11.1 kwa Machi mwaka huu.
“Badiliko la bei za bidhaa za vyakula majumbani na migahawani, limepungua hadi asilimia 9.7 Aprili mwaka huu, ikilinganishwa na asilimia 10.7 Machi mwaka huu,” alisema.
Kwesigabo alisema kasi ya ongezeko la bei kwa bidhaa zisizo za vyakula, imeongezeka hadi asilimia 8.9 kwa Aprili mwaka huu, kutoka asilimia 8.5 Machi.
Alisema mfumuko wa bei, ambao haujumuishi vyakula na nishati kwa Aprili mwaka huu, umeongezeka hadi asilimia 6.5, ikilinganishwa na asilimia 5.9 ya Machi.
Pia mfumuko wa bei ya nishati kwa Aprili, umepungua hadi kufikia asilimia 21.6, ikilinganishwa na asilimia 22.6 ya Machi.
No comments:
Post a Comment