Bernard Membe. |
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, amesema atakuwa
tayari kuwania urais mwaka 2015, iwapo wananchi wataona anafaa na kumtaka
afanye hivyo.
Alisema
hayo juzi wakati akijibu maswali ya mwandishi wa habari hii mjini
hapa, baada ya kumalizika kwa kongamano la vyuo vya elimu ya juu
mkoani hapa, lililofanyika katika ukumbi wa St. Dominic.
Membe
aliyekuwa mgeni rasmi katika kongamano hilo, alisema ingawa muda wa kufanya
uamuzi kuhusu mwaka 2015 bado na chama hakijatoa utaratibu, lakini atasubiri
ushauri wa Watanzania.
"Naomba
kurudia, mimi nilishapata kuueleza umma kuwa
muda haujafika wa kutangaza kugombea urais ...ila nasema hivi
natarajia sana ushauri wa Watanzania.
“Iwapo
Watanzania wataniona nafaa na kunitaka nigombee, nitapima mawazo yao
na iwapo ni wananchi wengi watakaoniunga mkono kutaka nigombee, basi
nitachukua fomu na kuijaza ili nigombee nafasi hiyo kwani sauti ya wengi ni
sauti ya Mungu," alisema Waziri Membe.
Membe
alisema hali ya kisiasa nchini inakwenda vibaya kutokana na kila
mtu kuzungumza mambo bila kujitathmini.
Alisema
mbaya zaidi hata baadhi ya wabunge wa CCM, nao wamekuwa si
msaada kwa chama, kutokana na kuzungumza mambo dhidi ya Serikali na chama.
Membe alisema amepata kukaa
bungeni kwa zaidi ya miaka 15 tangu Bunge la Spika Pius Msekwa, hadi
sasa chini ya Spika Anne Makinda, ila anachokiona ni baadhi
ya wabunge kukosa maadili na kuzungumza mambo bila kuzingatia kanuni
za Bunge, jambo ambalo ni hatari zaidi.
Alisema Bunge linalotazamwa
na Watanzania, ni lazima liwe la mfano wa kuigwa na
lenye kuzingatia maadili katika kuzungumza, lakini sasa hali
siyo hiyo, ndio maana Bunge linaendelea kupoteza mwelekeo.
"Bunge linapoteza mwelekeo
kutokana na mawazo ya baadhi ya wabunge wanaofikiri
wakisema ovyo na kutumia lugha kali katika kuzungumza,
wao ndio wanaonekana ni wabunge bora kitu ambacho
hakipo.
“Mbunge
ni pamoja na kujiheshimu na kutumia lugha nzuri katika kuwakilisha wapiga
kura wako bungeni," alisema.
Membe alisema
kutotumia busara katika kujadili mambo bungeni, si ubunge mzuri na
bora watambue wazi kuwa wananchi wao wanawatazama na hukumu yao
itatolewa mwaka 2015 katika uchaguzi mkuu kama hicho wanachokifanya, ni
kuwakilisha wananchi au kujiwakilisha.
"Nawaomba wabunge wawe
wazalendo, wawakilishe wananchi waliowatuma badala ya kuligeuza Bunge kama
sehemu ya kuonesha ujuzi wa kuzungumza ovyo.
“Nasema
tuogope wananchi, mwaka 2015 watatoa adhabu kwa kila mbunge na kwa sasa
wananchi wanasikiliza na kutazama ila muda ukifika watakuacha," alisema.
Alisema wabunge
wengi ni vijana na wanafikiri kusema vibaya juu ya CCM ndio ubunge bora, ila
watu watafanya uchunguzi wa kutembelea jimbo la mbunge husika
na kuangalia amefanya nini katika jimbo lake na watampima kwa
kazi aliyofanya na si ukali bungeni.
Alisifu baadhi ya wabunge wa CCM, kwamba
wamekuwa msaada mkubwa kwa wananchi
katika majimbo yao, kwa chama na Serikali chini ya Rais Jakaya Kikwete,
kwa kusukuma mbele maendeleo ya Taifa, ila baadhi yao wapo kwa
ajili ya kuonesha uwezo wa kusema ovyo.
No comments:
Post a Comment