MBUNGE ADAI MKURUGENZI MKUU WA NHC YUKO HATARINI KUUAWA...

Nehemiah Mchechu.
Baadhi ya watu wanaopinga juhudi za uongozi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kukabiliana na ubadhirifu, wamepanga kumwua Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Nehemia Mchechu, imeelezwa.

Akichangia hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi mjini hapa jana, Mbunge wa Viti Maalumu, Magdalena Sakaya (CUF), alifichua njama hizo akiwanyooshea vidole mafisadi waliokuwa wakitumia nyumba za NHC kujinufaisha kifedha.
Kutokana na kuwapo njama hizo, Mbunge huyo aliiomba Serikali kuchukua hatua za haraka za kumpa ulinzi mkurugenzi huyo ili asidhuriwe na watu hao.
Sakaya alisema vitisho hivyo pia vimeelekezwa kwa watendaji wengine wa shirika hilo wanaopambana na ufisadi huo.
“Mafisadi hawa walikuwa wamezoea kugeuza nyumba za NHC kama miradi yao kwa kupangisha wananchi wa kawaida na kuwanyonya na wakati mwingine kuzitumia kwa biashara.
“Kelele hizi ambazo zinasikika hata humu ndani ya Bunge zinatokana na hasira za mafisadi hawa walioshughulikiwa na Mkurugenzi Mkuu wa NHC na watendaji wake. Wanawapelekea watendaji hawa ujumbe wa kila aina wa vitisho, ikiwamo kumtishia Mkurugenzi kifo,” alisema Sakaya.
Akizungumzia gharama katika nyumba hizo, alisema hatua hiyo inatokana na Serikali kuondoa mkono wake katika ujenzi wa nyumba na kulifanya shirika hilo kutumia fedha zake lenyewe kujiendesha.
“Kwa vile hakuna fedha za Serikali pale, ni lazima NHC wajiendeshe kibiashara, vinginevyo watakufa. Ni lazima nyumba zao ziuzwe kulingana na bei ya soko, ili kuleta ushindani sokoni,” alisema.
Alisema miongoni mwa vitu vinavyoongeza gharama za nyumba hizo ni Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo kama itaondolewa na Serikali, itapunguza bei ya nyumba hizo.
Mbunge wa Viti Maalumu, Amina Makilagi ambaye pia ni Katibu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT-CCM), aliiomba Serikali kufanya uamuzi mgumu wa kufukuza kazi watumishi wa Idara ya Ardhi wanaojihusisha na rushwa na kujilimbikizia mali, vikiwamo viwanja.
Akichangia hotuba hiyo, Makilagi alisema ingawa Serikali ya CCM imeamini viongozi na kuwapa madaraka katika sekta ya ardhi, kuna walioamua kuichafua Serikali kwa kujihusisha na rushwa na ufisadi.
“Naiomba Serikali iwafukuze kazi mara moja maofisa hawa. Kitendo cha kuwahamisha maeneo ya kazi hakimalizi tatizo, bali kinazidi kuliongeza, maana watendaji hao wanapohamishiwa kwenye maeneo mengine huendelea na ubadhirifu,” alisema Makilagi.
Aliitaka pia Serikali kufanya juu chini ipate fedha za kupima ardhi nchi nzima akisema hatua hiyo itapunguza migogoro ya ardhi na kupanga mipango mizuri ya matumizi ya ardhi kuliko   sasa.
Mbunge wa Kibaha Vijijini, Jumaa Abuu (CCM) aliitaja Kampuni ya Mohamed Enterprises (METL), akisema imepora maeneo ya wananchi katika kata ya Soga Kipengele jimboni mwake na kuzusha mgogoro mkubwa huku Serikali ikishindwa kuchukua hatua stahiki.
Mbunge wa Igunga, Dalali Kafumu (CCM) alisema ni lazima Serikali itenge fedha ili kuipata Idara ya Upimaji na Ramani ili iboreshe ramani badala ya kutenga fedha kwa upimaji wa ardhi peke yake.
Alichachamalia viongozi wa Idara ya Ardhi, Igunga akisema wanapora maeneo ya wananchi na kujimilikisha au kuyauza kwa watu wenye fedha na kuwaacha wananchi wakiteseka.
Mbunge wa Viti Maalumu, Dk Mary Mwanjelwa (CCM) aliitaka Serikali kusaka na kuwafikisha mahakamani viongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala na wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, waliopindisha sheria na kuruhusu ujenzi holela wa jengo la ghorofa lililodondoka Dar es Salaam hivi karibuni. Bajeti hiyo ilipitishwa  jana.

No comments: