MAHAKAMA YAMWACHIA HURU MTOTO RAMA 'MLA VICHWA'...

Ramadhani Suleiman 'Rama mla kichwa' (kulia) na mama yake mzazi, Khadija (katikati) walipofikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza.
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imemuachiwa huru Ramadhani Suleiman (Rama mla kichwa) aliyekuwa anakabiliwa na kesi ya mauaji, baada ya kubaini hana akili timamu.

Jaji Rose Temba alitoa hukumu hiyo jana kutokana na ripoti ya Dk Mdeme Erasto iliyowasilishwa mahakamani hapo kuonesha kuwa, wakati mshitakiwa huyo anatenda kosa hilo hakuwa na akili timamu.
Ramadhani, ambaye alishitakiwa pamoja na mama yake Khadija Suleiman, alidaiwa kukutwa na kichwa cha mtoto Salome Yohana (3) katika eneo la Hospitali ya Taifa Muhimbili kikiwa katika mfuko wa plastiki maarufu kama rambo.
Jaji Temba alisema mshitakiwa alitenda kosa la mauaji, lakini kwa kuzingatia ripoti ya uchunguzi wa akili, mahakama haiwezi kumtia hatiani hivyo aliamuru mshitakiwa huyo awe chini ya uangalizi wa madaktari wa Hospitali za magonjwa ya akili na watatakiwa kuripoti maendeleo ya afya yake kwa Waziri wa Katiba na Sheria.
Aidha mahakama ilimwachia huru mama mzazi wa mshitakiwa huyo, Khadija, kwa kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) hakuwa na haja ya kuendelea kumshitaki.
Awali Wakili wa utetezi, Yusuph Shehe alidai kuwa mahakama ilitoa amri ya mshitakiwa kwenda hospitali kuchunguzwa kama ana akili na ripoti ya daktari iliwasilishwa mahakamani hapo na kubainisha kuwa hakuwa na akili timamu, hivyo aliomba mahakama imfutie mashitaka.
Akiwasomea maelezo ya awali washitakiwa hao, Wakili wa Serikali Cecilia Mkonongo alidai kuwa Aprili 25 mwaka 2008 saa 2:25 usiku, Salome (marehemu) alikuwa anacheza na Ramadhan pamoja na mtoto Paschal Lucas lakini baadaye alipotea katika mazingira ya kutatanisha.
Alidai saa 2:30 usiku baba wa Salome, Yohana Mussa alikwenda kwa dada yake aitwaye Furaha ambapo Salome alikuwa akiishi, alipohoji mtoto wake yupo wapi ndipo wakaanza kumtafuta bila mafanikio, wakaamua kutoa taarifa kwa balozi.
Aliendelea kudai kuwa, asubuhi ya Aprili 26 mwaka 2008, wakiwa  njiani kwenda kituo cha polisi walipewa taarifa kuwa kuna kiwiliwili cha mtoto kimeonekana katika choo cha nyumba ya washitakiwa, walipokwenda walikuta mwili wa Salome ukiwa chini bila kichwa.
Mkonongo alidai wakiwa katika eneo la tukio, polisi walipata taarifa kuwa kuna mtu amekamatwa na kichwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, walikwenda wakiwa na askari na ndugu wengine na kukitambua kichwa hicho.
Ilidaiwa kuwa, Ramadhani alikamatwa na mlinzi wa Hospitali hiyo akiwa na kichwa hicho na kudai anakipeleka kwa shangazi yake anayefanya kazi ya usafi katika hospitali hiyo.
Aprili 29 mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi na ripoti ya daktari ilionesha,  chanzo cha kifo chake hakikujulikana lakini, ilidai Salome alikatwa na kitu chenye ncha kali na alikuwa na michubuko mwilini.
Rama alipohojiwa na askari, alikiri kukutwa na kichwa hicho na kudai mama yake ndiye aliyemuua Salome kwa kutumia shoka na alikuwa anapeleka kichwa kwa shangazi yake.
Mama wa mshitakiwa huyo (Khadija)  alipohojiwa alikiri mwili wa marehemu kukutwa kwenye choo chake na ukiwa umefungwa na shati la Ramadhani.
Baada ya uamuzi huo kutolewa, ndugu wa marehemu waliangua kilio, na walipotoka Upendo Dunstan (mama wa marehemu) na shangazi yake Furaha Mussa walikuwa wakiangua kilio huku baba wa mtoto akilia huku ameshika kiuno nje ya mahakama hiyo. Washitakiwa walirudishwa rumande kwa ajili ya kukamilisha taratibu, baada ya kusota rumande kwa zaidi ya miaka mitano.

No comments: