MAHAKAMA YA RUFANI YAMREJESHEA UBUNGE HILARY AESHI...

Mheshimiwa Hilary Aeshi.
Mahakama ya Rufaa, imemrudisha bungeni na kumtangaza Hilary Aeshi kuwa mbunge halali wa Sumbawanga Mjini, baada ya kutengua hukumu ya Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga iliyomuondoa madarakani.

Hatua hiyo inatokana na rufaa mbili zilizowasilishwa na Aeshi pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), kupinga hukumu hiyo iliyotolewa na Jaji Bathuel Mmila.
Hilary alivuliwa wadhifa huo Aprili 30, mwaka jana kutokana na kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea wa kiti hicho kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Norbert Yamsebo.
Akisoma uamuzi uliotolewa na jopo la majaji Edward Rutakangwa, Stephen Bwana na Profesa Ibrahim Juma, Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufaa, Zahra Maruma alisema hawakubaliani na uamuzi wa Jaji Mmila, kwa kuwa Yamsebo hakuthibitisha tuhuma dhidi ya Aeshi.
Alisema, Mahakama baada ya kutathimini upya ushahidi katika kesi ya msingi, imebaini kuwa Yamsebo hakuthibitisha madai yake bila kuacha shaka kama inavyohitajika kisheria.
Alisema, Mahakama imebaini kuwa kulikuwa na mkanganyiko katika ushahidi wa Yamsebo pamoja na mashahidi wake na kuwa Mahakama Kuu ilikosea kusema kuwa mkanganyiko huo haukuwa na athari.
Aidha katika tuhuma za rushwa, ambayo Yamsebo alidai kuwa mawakala wa Aeshi waligawa fedha katika mkutano uliofanyika katika Shule ya Msingi Kantalamba Mazoezi, mashahidi hawakueleza kama kweli Aeshi alihusika na tuhuma hizo.
Alisema, Jaji alikosea kutoa uamuzi kwa kutumia ushahidi wa shahidi mmoja, aliyedai alishuhudia ugawaji wa fedha hizo lakini hakuwatambua watu waliopewa fedha hizo hata wanakijiji wenzie isipokuwa mawakala hao.
Akizungumza nje ya Mahakama, Aeshi alisema kuwa hatimaye mahakama hiyo imetenda haki, na kuwataka wakazi wa jimbo lake watulie kwa sababu anarudi kuwatumikia.
Alisema alipokuwa nje, mambo mengi yalikuwa yamesimama, lakini  sasa anarejea jimboni kwake kuwatumikia wananchi waliomchagua kihalali kama Mahakama ilivyosema.
Kwa upande wake, Yamsebo alidai amesikitishwa na hukumu hiyo kwa kuwa walitoa malalamiko ya kweli, lakini Mahakama imeamua kumpa Aeshi ushindi hivyo hana la sema zaidi ya kumshukuru Mungu.

No comments: