MAHAKAMA YA RUFAA YAMREJESHEA UBUNGE DK DALALY KAFUMU...

Dk Dalaly Kafumu.
Mahakama ya Rufaa nchini imetengua uamuzi ya Mahakama Kuu na kumrudishia ubunge Dk Dalaly Peter Kafumu (CCM) wa Jimbo la Igunga baada ya kuridhika na hoja za upande wa mrufani kuwa Jaji aliyesikiliza shauri hilo hakuzingatia matakwa ya kisheria.

Akisoma  uamuzi huo jana, Mwenyekiti wa Jopo la Majaji wa Mahakama hiyo, Jaji Nathalia Kimaro akisaidiana na Jaji William Mandia na Jaji Semistrocles Kaijage, alisema mlalamikiwa hakulipa ada ya Mahakama kama sheria ya uchaguzi inavyoelekeza.
Aliongeza, kuwa awali wakati shauri hilo namba 10/2011 likifunguliwa Mahakama Kuu, Jaji hakusikiliza pingamizi la mrufani, kwamba hakukuwa na ada iliyolipwa, hivyo hakupaswa kuendelea na usikilizwaji wake.
 “Kutolipwa ada ama kukosekana kumbukumbu yoyote katika jalada la Mahakama inayoonesha kitu kuwekwa kama kinga, ilikuwa ni sababu tosha ya kutosikiliza shauri hilo,” walisema majaji hao katika uamuzi wao.
Katika hoja zake, Wakili wa Serikali, Gabriel Malata za kutaka uamuzi wa Mahakama Kuu utenguliwe, aliwaambia majaji wa Mahakama ya Rufaa, kuwa Jaji aliyesikiliza kesi hiyo alikosea kuisikiliza bila mlalamikaji kutimiza matakwa ya kisheria.
Malata alidai, kuwa mlalamikaji hakulipa ada ya Mahakama kiasi cha Sh milioni moja alizotakiwa kutoa au hati ya nyumba kabla kesi hiyo haijasikilizwa kama sheria ya uchaguzi kifungu namba 111 kinavyoelekeza.
Wakili Malata aliongeza kuwa kwa vile mjibu rufaa Joseph Kashindye wa Chadema na wenzake hawakutekeleza masharti hayo, usikilizwaji wa shauri hilo pamoja na mwenendo mzima ukiwamo uamuzi, vyote vilikuwa batili.
Aliongeza kuwa malalamiko yaliyopelekwa mahakamani ni ya kutengeneza, kwani hayakupata kuwasilishwa katika Kamati ya Maadili ya Uchaguzi kama walivyofanya juu ya suala la Mbunge wa Tabora Mjini Ismail Aden Rage, ambaye alitozwa faini ya Sh 100,000 kwa kutembea na silaha kwenye mkutano.
Hoja hizo na zingine zilipingwa na Wakili wa mjibu rufaa, Profesa Abdallah Safari ambaye aliitaka Mahakama ya Rufaa kuzitupilia mbali na kwamba Mahakama iliyosikiliza kesi hiyo iliridhika kuwapo ukiukwaji wa sheria wakati wa uchaguzi wa jimbo la Igunga ndipo ikatengua matokeo.
Kukatwa rufaa hiyo kulitokana na uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kutengua matokeo ya uchaguzi mdogo wa Jimbo la Igunga mkoani hapa, baada ya kubainika kuwa uchaguzi huo ulitawaliwa na vitendo vya rushwa, kampeni chafu na vitisho dhidi ya wapiga kura.
Jaji Mary Shangali wa Mahakama Kuu, Agosti 21 mwaka jana, alitangaza kutengua matokeo hayo baada ya Mahakama hiyo kuridhika na hoja saba zilizowasilishwa na upande wa mlalamikaji, kati ya hoja 19 zilizowasilishwa mahakamani hapo.
Kesi hiyo ilifunguliwa na mlalamikaji aliyekuwa mgombea wa Chadema, Kashindye, ambaye aliwakilishwa na Profesa Safari akipinga matokeo kwa madai ya kuwapo ukiukwaji wa sheria ya uchaguzi.
Upande wa utetezi  uliwakilishwa na  mawakili Mohamed Salum Malik na Malata kutoka ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Igunga na mawakili Anthony Kanyama na Kamaliza Kayaga waliokuwa wakimtetea Dk Kafumu.
Jaji Shangali alitaja baadhi ya kasoro zilizotengua matokeo hayo kuwa ni pamoja na ahadi  iliyotolewa na Waziri wa Ujenzi,  Dk John Magufuli, kuhusu  ujenzi wa daraja la Mbutu ambalo alidai kama wananchi hawataichagua CCM daraja hilo halitajengwa, wakati kipindi hicho kulikuwa na shida kubwa ya usafiri eneo hilo.
Alisema kitendo pia kilichofanywa na Mbunge wa Tabora Mjini Rage, hakikuwa cha uungwana kwani alitumia lugha ya uongo kwa lengo la kupotosha wapiga kura ambapo alidai mgombea wa Chadema amejitoa katika uchaguzi huo.
Akizungumza na mwandishi baada ya uamuzi huo nje ya Mahakama jana, aliyekuwa mjibu rufaa   Kashindye alikubali na kuridhika huku akiwalalamikia mawakili wake kwamba hawakumwelekeza kufanya hivyo. “Sikujua, sikuelezwa, hili ni tatizo la kiufundi hivyo silaumu,” alisema  Kashindye.
Umati wa wana Chadema ambao ulijaa ndani ya chumba cha Mahakama uliondoka kwa huzuni eneo hilo   wakikubali matokeo huku wengine wakisema “tukajipange kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao.”
Dk Kafumu hakuwa mahakamani alipotafutwa kwa simu, alisema hukumu iliyotolewa ndiyo haki kamili kwani mwanzo alikuwa na wasiwasi na Jaji yule lakini alionekana anaogopa kuangushwa.
Alisema amerejeshewa ubunge wake ili kutumikia wananchi wa Igunga bila kujali itikadi ya chama chochote cha siasa kwani waliompa kura na waliomnyima, wote ni wananchi wa Igunga.
Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Igunga, Costa Olomi, alisema ushindi wa Kafumu ni wa wananchi wote wa Igunga si wa chama kwani ni kwa ajili ya maendeleo ya Igunga na Mkoa wa Tabora. Alisema baada ya kurejeshewa ubunge wake, CCM imepanga mapokezi makubwa ya kumpokea Mei 12.

No comments: